wildaftanzania.org · web viewhotuba ya mheshimiwa kassim m. majaliwa (mb), waziri mkuu wa jamhuri...
TRANSCRIPT
HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUZINDUA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KATIKA VIWANJA VYA JAMHURI DODOMA, TAREHE 25 NOVEMBA 2018
SALAMU
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Mhe. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Dkt. John Jingu, Katibu Mkuu anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Bw. Alvaro Rodriguez, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania;
Ndugu Hodan Addou, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wanawake (UN-Women);
Ndugu Ann Theresa Ndong Jatta, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO);
Mhe. Paul Sherlock, Balozi wa Ireland nchini;
Mhe. Sarah Cooke, Balozi wa Uingereza nchini;
Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali mliopo hapa;1
Ndugu Anna Meela Kulaya, Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF);
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la WiLDAF;
Ndugu Kees Groenendijk, Mkurugenzi wa Taasisi ya Huduma za Sheria (LSF);
Ndugu Francis Odokorach, Mkurugenzi wa Shirika la Oxfam;
Wawakilishi kutoka Balozi na Mashirika ya Kimataifa nchini;
ACP Mary Nzuki, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi Tanzania;
Wawakilishi wa Taasisi za Utafiti na Elimu ya Juu mliopo;
Wawakilishi wa Wafanyakazi na Watendaji kutoka Serikalini;
Wawakilishi kutoka Taasisi na Asasi za Kiraia na Binafsi mliopo;
Waandishi wa Habari;
Walimu na Wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo mbalimbali mliopo hapa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.2
Habari za Mchana.
UTANGULIZI
Ndugu Wananchi;
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
rehema kwa kutujaalia afya na uzima na kutuwezesha
kuhudhuria uzinduzi huu wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga
Ukatili wa Kijinsia 2018.
Pili, napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati
kwa heshima kubwa ambayo mmenipatia kwa kunialika kuwa
Mgeni Rasmi kwenye Uzinduzi wa kampeni hii.
Tatu, kipekee nitoe pongezi za dhati kwa Uongozi wa Mkoa
wa Dodoma kwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa Kampeni hii
Kitaifa. Hongereni sana kwa maandalizi mazuri!
Nne, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowafikishia salamu
zenu kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
3
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambao
kwa pamoja wanawatakia kampeni salama, ya amani na
yenye mafanikio yaliyokusudiwa.
UKATILI WA KIJINSIA
Ndugu Wananchi,
Ukatili wa Kijinsia ni kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha,
vinavyotesa, vinavyonyanyasa, vinavyokandamiza, visivyojali
haki za kuishi kwa binadamu anaweza kuwa wa kiume au
kike.
Ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi. Aidha, kwa
uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia tunamaanisha
vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi,
lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa
za kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
4
Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa
na mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile,
kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa.
Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi yakiwemo;
kumpiga mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu,
kumlawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika
mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi wanaohusika.
Mambo mengine yenye kuhusisha ukatili wa kijinsia ni mimba
na ndoa za utotoni na vitendo vingine vinavyofanana na
hivyo ambavyo vinafanyika mahali pa kazi, shuleni, mitaani,
majumbani na mitandaoni ambavyo kwa sehemu kubwa
huwaathiri zaidi wanawake na watoto.
Tafiti zinaonesha kuwa ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa
ambalo linaikabili Dunia na hutokea katika Nchi mbalimbali.
Kwa mfano, takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani
mwaka 2013 zinaonesha kuwa takriban asilimia 35 ya
wanawake Duniani wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wa
kupigwa au kubakwa katika kipindi cha maisha yao. 5
Aidha, taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuwahudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2017 zinaonesha
kuwa wanawake na wasichana wapatao milioni 750 Duniani
waliolewa wakiwa chini ya miaka 18. Halikadhalika, taarifa
hiyo inakadiria kuwa wasichana milioni 120 (yaani mmoja kati
ya wasichana 10) Duniani wamekumbana na vitendo vya
kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.
Kwa upande mwingine, wanawake na wasichana milioni 200
walifanyiwa vitendo vya ukeketaji katika Nchi 30 Duniani.
Vilevile, wasichana na wavulana wapatao milioni 246
wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wakiwa shuleni.
Ndugu Wananchi,
Kama zilivyo Nchi nyingine Duniani, Tanzania ni miongoni mwa
Nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu mwaka 2015/2016 kupitia Taarifa ya Idadi ya
Watu na Afya inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye
6
umri kati ya miaka 15 - 49 wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au
kingono katika kipindi cha maisha yao.
Kadhalika, asilimia 22 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15
- 49 walifanyiwa vitendo vya kingono kinyume na matakwa yao.
Kwa ujumla taarifa hiyo, inaonesha hakuna tofauti kubwa ya
mabadiliko katika jamii zetu kuhusu mitazamo na matendo ya
jamii zetu kuhusiana na Ukatili wa Kijinsia. Ni dhahiri kuwa bado
tuna kazi kubwa ya kuhamasisha jamii zetu kubadili fikra na
mitazamo inayochochea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
JUHUDI ZA SERIKALI KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA
Ndugu Wananchi,
Nimefahamishwa kuwa Kaulimbiu ya Kampeni ya Siku 16 za
Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu ni “FUNGUKA!
USALAMA WAKE: WAJIBU WANGU”. Kaulimbiu hii inatupa
jukumu sisi sote la kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake
anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza
7
ukatili wa kijinsia hususan dhidi ya wanawake na watoto katika
maeneo mbalimbali ikiwemo katika nyumba tunazoishi, mahali pa
kazi, shuleni na mahali pengine katika jamii zetu.
Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia hapa nchini, Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, imechukua hatua mbalimbali za kuzuia
na kutokomeza ukatili.
Hatua hizo ni pamoja na kuandaa Mpango wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/2018 -
2021/2022) ambao utekelezaji wake unaendelea. Mpango huo,
unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na
watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Mpango huo, ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya
Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya
Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya
8
Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998) ambayo imehuishwa
kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 kwa lengo la
kuhakikisha kuwa utu wa wanawake na watoto unalindwa pamoja
na Sheria ya Mtoto (2009) inayolinda haki za mtoto.
Aidha, utekelezaji wa Mpango huo utachangia katika utekelezaji
wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa
wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki
na ustawi wa mtoto.
Ndugu Wananchi,
Mpango huo jumuishi, unatekelezwa na wadau mbalimbali nchini
ikiwemo Wizara, Idara, na Wakala mbalimbali za Serikali,
Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa, Asasi za Kiraia, Sekta
Binafsi na wanajamii mmoja mmoja au katika vikundi. Serikali
inaamini kuwa mpango huo utasaidia sana wadau mbalimbali
kuchukua hatua stahiki zitakazopunguza au kuondoa kabisa
vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini.
9
Aidha, natoa wito kwa kila mwananchi na watekelezaji wengine
wa Mpango huo kutimiza wajibu wenu ipasavyo katika
kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa hapa nchini. Ni
imani yangu kuwa kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo,
ukatili wa kijinsia utabaki kuwa historia hapa nchini.
Ndugu Wananchi,
Juhudi nyingine ambazo zimefanywa na Serikali kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali ni kama zifuatazo:
Mosi: Kuanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya
Polisi ambapo hadi sasa madawati 417 yameanzishwa na
yanafanya kazi kwa lengo la kuwezesha huduma stahiki
katika vituo vya Polisi na kutenda haki. Huduma hii
imewezesha wahanga 58,059 kuripoti aina mbalimbali za
matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watu wazima na watoto,
ikiwemo ubakaji, ulawiti, vipigo na ukeketaji. Madawati
haya yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini
10
na kutoa taarifa za ukatili unapotokea kwenye maeneo
yao.
Kwa kuzingatia ukweli kuwa watu wenye ulemavu wana
mahitaji maalumu na kwamba ni wahanga wa ukatili wa
kijinsia naelekeza Jeshi la Polisi kuboresha Dawati hili ili
liweze kushughulikia kikamilifu masuala ya ukatili wa
kijinsia dhidi ya watu wenye ulemavu. Hivyo, kuanzia sasa
Dawati hilo liitwe Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na
Watu wenye Ulemavu.
Pili: Vituo vya Mkono kwa Mkono vya Kutoa huduma kwa
Wahanga wa Ukatili wa Kijinsia (One Stop Centres)
vimeanzishwa katika Mikoa sita ya Tanzania Bara. Mikoa
hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Mbeya,
Iringa na Shinyanga. Vituo hivi vinawezesha utoaji wa
huduma rafiki na za haraka kwa waathirika wa vitendo vya
ukatili na vinahusisha wataalamu mbalimbali ikiwemo
Maafisa wa Jeshi la Polisi, Wataalamu wa Ustawi wa
Jamii, Wanasheria na Madaktari kwa ajili ya utoaji wa
11
huduma za matibabu, unasihi, kipolisi na msaada wa
kisheria.
Tatu: Kuanzishwa kwa huduma ya simu bila malipo kwa watoto
wanaofanyiwa vitendo vya Ukatili na unyanyasaji (Child
Helpline) ili kutoa taarifa kwa haraka. Watoto ambao
hufanyiwa vitendo hivi huunganishwa na huduma
mbalimbali za kijamii kama Polisi, Hospitali, Ustawi wa
Jamii na Mahakama. Kwa kupitia huduma hii kwa mwaka
2017 jumla ya watoto 17,443 walipiga simu na
kuunganishwa na huduma stahiki mbalimbali.
Nne: Kupitia Serikali ya Awamu ya Tano, tumeanzisha na
kutekeleza Sera ya Elimumsingi Bila Malipo ili kusaidia
kuleta usawa wa fursa za kielimu kwa watoto wote wa kike
na wa kiume bila kujali uwezo wa kiuchumi wa familia.
Serikali ya Awamu ya Tano inatarajia kuwa utekelezaji wa
Sera hii siyo tu utapunguza mimba na ndoa za utotoni bali
pia utaondoa pengo la kijinsia katika elimu baina ya watoto
wetu wa kike na wa kiume.
12
Tano: Sambamba na utoaji wa elimu pasipo malipo kwa ngazi
husika, Serikali imewezesha Marekebisho ya Sheria ya
Elimu na kulifanya kosa la kumpa mimba mwanafunzi;
kuoa mwanafunzi au kuolewa na mwanafunzi wa shule za
msingi na sekondari kuwa kosa la jinai na pale
inapothibitika adhabu yake ni kifungo cha miaka 30.
Sita: Serikali imewezesha kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa
Kisheria ya mwaka 2017 kwa ajili ya kuwawezesha watu
wote wakiwemo wanawake na watoto kupata haki zao za
kisheria kupitia vyombo vya usimamizi wa Sheria
sambamba na kushughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia.
Saba: Serikali imeifanyia marekebisho Sheria ya Fedha za
Mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 2018 kwa lengo la
kuufanya uchangiaji wa asilimia 10 wa pato la ndani la
Halmashauri kwa ajili ya wanawake (asilimia 4), vijana
(asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2). Aidha,
marekebisho hayo yameondoa riba kwenye mikopo
inayotokana na fedha hizo.
13
Ndugu Wananchi,
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni nyingi na sitaweza kuzitaja
zote hapa. Lengo la juhudi hizi ni kuhakikisha kuwa wanawake,
wanaume, wasichana, wavulana na watu wenye ulemavu
wanakuwa na mazingira mazuri ya kujikwamua na kuondokana
na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, juhudi hizi za Serikali hazitaweza kuzaa matunda
mazuri iwapo hazitaungwa mkono na wananchi wenyewe pamoja
na wadau mbalimbali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna
changamoto ambazo Serikali peke yake haitaweza kuzimaliza
pasipo ushiriki wa wananchi. Changamoto hizo ni pamoja na
kuendelea kuwepo kwa mila na desturi zenye kuleta madhara
kama vile ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.
Changamoto nyingine ni umaskini miongoni mwa jamii;
mmomonyoko wa maadili; mapungufu katika malezi ya vijana na
watoto wetu kuhusu maisha yao hususan katika zama hizi za
sayansi, teknolojia na utandawazi pamoja na upungufu wa
14
makazi ya muda kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia
(yaani safe house).
ATHARI ZA UKATILI WA KIJINSIA
Ndugu Wananchi,
Napenda niwafahamishe kuwa, ukatili wa kijinsia hususan dhidi
ya wanawake na watoto unarudisha nyuma juhudi za Serikali za
kuhakikisha kuwa mapinduzi ya viwanda na kilimo yanafikiwa.
Hatuwezi kuwa na Taifa linalozalisha na kufikia malengo ya kuwa
Nchi ya uchumi wa kati iwapo muda mwingi unatumika kuamua
migogoro na kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia badala ya
kushiriki katika shughuli za uzalishaji.
Aidha, Serikali inatumia gharama nyingi katika kushughulikia
wahanga wa ukatili ambapo fedha hizo zingeweza kutumika
katika kutoa huduma nyingine za jamii. Kimsingi, Serikali ya
Awamu ya Tano haiwezi kuvumilia vitendo hivi kwa kuwa
vinaathiri maendeleo yetu na kusababisha uvunjifu wa amani.
15
Natumia fursa hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa wote kuhakikisha
wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake
na Watoto za ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji kama
inavyoelekezwa katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.
Vilevile, nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kuanzisha Programu za Kijamii za kutokomeza ukatili wa
kijinsia katika Halmashauri husika zitakazozingatia hali halisi na
kuzitengea bajeti programu hizo kama inavyoelekezwa kwenye
Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto.
MATARAJIO
Ndugu Wananchi,
Nimeelezwa kuwa, huu ni mwaka wa 27 wa maadhimisho ya Siku
16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia hapa Tanzania. Aidha,
maadhimisho haya yanafanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza hapa
Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya Nchi. Hivyo, ni
16
matumaini yangu kuwa kupitia Kampeni za aina hii kila mmoja
wetu na kila Taasisi itakuwa Balozi wa kuzuia na kutokomeza
ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, wanaume, wasichana na
wavulana hapa nchini.
Ndugu Wananchi,
Nawapongeza ninyi wananchi wote kwa kuona umuhimu wa
Kampeni hii na kushiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Kampeni hii.
Ni matarajio yangu kwamba kampeni hii ya Siku 16 za Kupinga
Ukatili wa Kijinsia – Kitaifa, italeta mabadiliko makubwa kupitia
jumbe mbalimbali zilizoandaliwa kupitia machapisho, nyimbo,
shuhuda na semina zitakazokuwa zinaendelea kutolewa kwenye
majukwaa mbalimbali katika kipindi chote cha kampeni.
Natoa wito kwa wadau wote kutumia kampeni hii kama jamvi la
kupata elimu na uelewa kuhusu namna ya kuzuia na kutokomeza
ukatili wa kijinsia kwa kuwa na sauti ya pamoja katika kukabiliana
na vitendo hivyo.
Ndugu Wananchi,
17
Kwa mara nyingine nawahakikishia kuwa Serikali itaendelea
kuboresha na kuweka mazingira salama kwa wananchi wote kwa
kutekeleza Sera, Sheria, Mikakati, Mipango na Miongozo
mbalimbali ili kutokomeza ukatili wa kijinsia hapa nchini.
Pia, nirudie tena kuwasisitiza na kuwataka wadau wote kuendelea
kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto (2017/2018 – 2021/2022). Ni matumaini
yangu kuwa kwa nguvu ya pamoja kati ya Serikali, Wadau wa
Maendeleo, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sekta Binafsi
tunaweza kupunguza na kuondoa kabisa vitendo vya ukatili wa
kijinsia katika jamii yetu.
HITIMISHO
Ndugu Wananchi,
Mwisho, natoa pongezi zangu za dhati kwa Wizara yenye
dhamana na jinsia, Shirika la Wanawake katika Sheria na
Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tawi la Tanzania, Mtandao wa
Mashirika yanayopambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) na
18
wadau wengine kwa kuandaa na kuratibu ufunguzi wa Kampeni
hii kwa mafanikio makubwa.
Halikadhalika, nawashukuru Wadau wa Maendeleo waliounga
mkono na kuweza kufanikisha Kampeni hii. Kwa hakika sitaweza
kumtaja kila mmoja lakini naomba niwataje wafuatao: Shirika la
Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wanawake (UN-Women);
Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Elimu, Sayansi, na
Utamaduni (UNESCO); Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID);
Ubalozi wa Ireland; Taasisi ya Huduma za Sheria (LSF); Shirika
la Oxfam na wengine wote waliofanikisha Kampeni hii.
Ndugu Wananchi
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Kampeni ya
Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka 2018
imezinduliwa rasmi leo tarehe 25 Novemba, 2018 kwenye
Viwanja hivi vya Jamhuri, jijini Dodoma.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
19