kutathmini nafasi ya mwanamke katika mashairi ya kiswahili: uchunguzi … · 2016. 5. 9. ·...
TRANSCRIPT
KUTATHMINI NAFASI YA MWANAMKE KATIKA MASHAIRI YA
KISWAHILI: UCHUNGUZI WA MASHAIRI YA SHAABAN ROBERT NA
MATHIAS MNYAMPALA
ALI EDRIS ALI
TASINIFU ILIYOWASILISHWA KWA AJILI YA KUTIMIZA SHARTI
PEKEE LA KUTUNUKIWA DIGRII YA UZAMILI (M.A KISWAHILI) YA
CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA
2014
ii
UTHIBITISHI
Mimi Profesa T.S.Y.M.Sengo ninathibitisha kuwa nimesoma tasinifu hii iitwayo
Kutathmini Nafasi ya Mwanamke katika Mashairi ya Kiswahili: Uchunguzi wa
Mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala na ninapendekeza ikubaliwe
na Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kwa ajili ya kukamilisha masharti ya Digrii ya
M.A. Kiswahili ya Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
__________________________
Sheikh, Daktari, Professa T.S.Y.M. SENGO
(Msimamizi)
____________________
Tarehe
iii
HAKI MILIKI
Hairuhusiwi kuiga au kunakili kwa namna yoyote sehemu yoyote ile ya tasinifu hii
kwa njia yoyote kama vile, kielektroniki, kurudufu nakala, kurekodi au njia yoyote
nyingine bila ya idhini ya mwandishi au Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa niaba.
iv
TAMKO
Mimi Ali Edris Ali, ninathibitisha kuwa tasinifu hii ni kazi yangu halisi na haijawahi
kuwasilishwa katika Chuo Kikuu kingine chochote kwa ajili ya kutunukiwa shahada
kama hii au nyingine yoyote.
……………………………………………..
Sahihi
……………………………………………..
Tarehe
v
TABARUKU
Kazi hii ninaitabaruku kwa Wananchi wote wa Libya ambao hivi sasa wapo katika
mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayosababisha mauaji ya raia wasio na hatia.
Kwa kazi hii ninawaomba wasitishe mapigano na warejeshe amani kama ilivyokuwa
zamani. Pia niaitabaruku kazi hii kwa mke wangu na mtoto wetu Aisha Ali Edris Ali na
kuwahusia kuwa wafanye jitihada katika kusoma ili wapate kufika katia ngazi ya elimu
niliyoifikia mimi na hata kunizidi Inshaallah.
vi
SHUKURANI
Hakuna apasae kushukuriwa wa kwanza katika mafanikio yoyote ya mwanadamu
isipokuwa Mwenyezi Mungu Subhana Wataala. Hivyo, shukurani zangu za kwanza
napenda kuzitoa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia afya njema katika
kipindi chote nilichokuwa ninaandika kazi hii. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kuijaalia familia yangu salama na amani katika kipindi hiki ambapo nchi yangu
ya Libya ipo katika machafuko ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa hili,
ninasema Alhamdulillah Rabi Laalamina.
Shukurani zangu za pili nazitoa kwa msimamizi wangu Sheikh, Daktari, Profesa T.
S. Y. M. SENGO kwa maongozi mema katika kipindi chote cha uandishi wa tasinifu
yangu. Msimamizi huyu ni hodari wa kusahihisha kazi kwa kusoma neno kwa nno
na ni jambo la kawaida kukuta wino mwekundu unaozidi maandishi ya mtafiti katika
kila ukurasa wa kazi aliyoisahihisha. Kwa mara ya kwanza kukutana na hali hiyo,
nilikata tamaa na kudhani kwamba sitaweza kufuzu masomo yangu. Kwa bahati
nzuri, msimamizi wangu alinitia moyo kuwa nisiakate tamaa kwani huko ndiko
kujifunza na shule ndivyo ilivyo. Kutokana na ushauri huo niliongeza jitihada katika
masomo na leo hii nimefikia hatua hii.
Shukurani zangu za tatu nazitoa kwa familia yangu iliyopo katika mji wa Sebha
nchini Libya kwa kunisaidia kifedha na ushauri katika kipindi chote cha masomo
yangu. Mimi ninalipiwa gharama za masomo na Serikali ya Libya kwa asilimia mia
moja. Kutokana na machafuko na vita vinavyoendelea katika nchi yangu imekuwa ni
vigumu kwa serikali kutupatia fedha kwa wakati na wakati mwingine kutopatiwa
kabisa. Kwa hali hiyo, familia yangu imekuwa ikinitumia fedha mara kwa mara na
vii
kunifanya nisiishi kwa shida sana hapa Tanzania. Ninasema asante sana kwa familia
yangu.
Shukurani zangu za nne ninazitoa kwa mke wangu mpenzi ambaye kwa sasa nipo
naye hapa Tanzania. Mke wangu amekuwa akinitia moyo kwamba siku moja
nitafanikiwa na kukamilisha kazi yangu. Leo hii ninafurahi kuona hamasa na moyo
aliyokuwa akinitia vimenisaidia kukamilisha kazi yangu. Ninakushukuru sana mke
wangu kwa mawazo, uvumilivu na muongozo wako na Mwenyezi Mungu ndiye
atakayekulipa. Pia, ninapenda kumshukuru mtoto wetu Aisha Ali Edris Ali kwa
kunielewa kila mara nilipomfukuza asinisumbue wakati ninaandika kazi yangu.
Salamu zangu za tano ninazitoa kwa Walimu wote wa Chuo Kikuu Huria Cha
Tanzania kwa kunifundisha na kunipatia miongozo mbalimbali ya kukamilisha kazi
yangu. Miongoni mwao ni Profesa Emmanuel Mbogo, Daktari Anna Kishe, Daktari
Peter Pembe Lipembe, Daktari Hanna Simpassa, Daktari Zelda Elisifa na Hadija
Jilala. Ninasema asanteni sana walimu wangu kwa kunifundisha lugha ya Kiswahili
ambayo kwa sasa ninaiweza kiasi ikilinganishwa na nilivyokuja kutoka Libya kwa
mara ya kwanza.
viii
IKISIRI
Mada ya utafiti huu ni “Kutathmini Nafasi ya Mwanamke katika Mashairi ya
Kiswahili: Uchunguzi wa Mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala.”
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kulinganisha nafasi ya mwanamke katika
mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala ili kubaini falsafa yao juu ya
mwanamke katika jamii. Madhumuni mahususi ya utafiti huu yalikuwa ni
kulinganisha na kulinganua usawiri wa mwanamke katika mashairi ya Shaaban
Robert na Mathias Mnyampala, kulinganisha na kulinganua matumizi ya lugha ya
kisanaa inayotumiwa na Shaaban Robert na Mathias Mnyampala katika kusawiri
nafasi ya mwanamke na kubainisha falsafa ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala juu ya nafasi waliyompa mwanamke katika mashairi yao. Nadharia ya
Kifeministi ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data za utafiti huu. Mbinu za
usaili, hojaji na usomaji makini ndizo zilizotumika katika kukusanya data za utafiti.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa mwanamke anasawiriwa kama chombo cha
starehe kwa mwanaume, mwanamke ni kiumbe mpole na mnyenyekevu kwa
mumewe, ni mama na mlezi katika jamii, mwanamke na suala la uaminifu na
mwanamke na suala la umalaya na uasherati. Matumizi ya lugha ya tamathali za
takriri, tashibiha, taswira na ishara ndizo zilizotumika kusawiri nafasi ya mwanamke
katika mashairi yaliyotafitiwa. Falsafa yao juu ya mwanamke inasema, mwanamke
ni kiumbe mwenye daraja ya juu katika malezi na ustawi wa jamii nzima na si
familiya yake tu.
ix
YALIYOMO
Uthibitishi .................................................................................................................... ii
Haki Miliki .................................................................................................................. iii
Tamko…. .................................................................................................................... iv
Tabaruku ...................................................................................................................... v
Shukurani .................................................................................................................... vi
Ikisiri………. ............................................................................................................ viii
Yaliyomo ..................................................................................................................... ix
SURA YA KWANZA: UTANGULIZI .................................................. 1
1.0 Usuli wa Tatizo la Utafiti .............................................................................. 1
1.1 Tatizo la Utafiti ............................................................................................. 4
1.2 Malengo ya Utafiti ....................................................................................... 5
1.2.1 Lengo Kuu la Utafiti ..................................................................................... 5
1.2.2 Malengo Mahususi ........................................................................................ 5
1.2.3 Maswali ya Utafiti ......................................................................................... 6
1.3 Umuhimu wa Utafiti ..................................................................................... 6
1.4 Mipaka ya Utafiti .......................................................................................... 7
1.5 Matatizo ya Utafiti na Utatuzi Wake ............................................................ 8
1.6 Hitimishi ....................................................................................................... 8
SURA YA PILI: UTALII WA KAZI TANGULIZI NA MKABALA WA
KINADHARIA .............................................................................. 9
2.0 Utangulizi ...................................................................................................... 9
2.1 Ushairi wa Shaaban Robert ........................................................................... 9
x
2.2 Ushairi wa Mathias Mnyampala ................................................................. 15
2.3 Mkabala wa Kinadharia .............................................................................. 17
2.3.1 Nadharia ya Ufeministi ............................................................................... 17
2.4 Hitimishi ..................................................................................................... 19
SURA YA TATU: NJIA ZA UTAFITI ............................................... 21
3.0 Eneo la Utafiti ............................................................................................. 21
3.1 Kundi Lengwa ............................................................................................. 21
3.2 Sampuli ya Utafiti ....................................................................................... 22
3.3 Mbinu za Kukusanyia Data ........................................................................ 23
3.3.1 Mbinu ya Usaili ........................................................................................... 23
3.3.2 Hojaji .......................................................................................................... 23
3.3.3 Mbinu ya Usomaji Makini .......................................................................... 24
3.4 Mbinu ya Uchambuzi wa Data ................................................................... 24
3.5 Kuaminika kwa Data za Utafiti .................................................................. 26
3.6 Usahihi wa Data za Utafiti .......................................................................... 26
3.7 Hitimisho ..................................................................................................... 26
SURA YA NNE: UWASILISHAJI, UCHAMBUZI NA MJADALA
WA DATA ZA UTAFITI ................................................................ 28
4.0 Utangulizi .................................................................................................... 28
4.1 Usawiri wa Mwanamke katika Mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala ................................................................................................. 28
4.1.1 Mwanamke kama Chombo cha Starehe ...................................................... 29
4.1.2 Mwanamke ni Mpole, Mnyenyekevu kwa Mwanaume .............................. 32
xi
4.1.3 Mama na Malezi katika Jamii ..................................................................... 38
4.1.4 Mwanamke na Suala la Uaminifu ............................................................... 41
4.1.5 Suala la Uasherati na Umalaya katika jamii ............................................... 45
4.2 Matumizi ya lugha ya Kisanaa katika Mashairi ya Washairi Teule ........... 47
4.2.1 Matumizi ya Takriri katika Mashairi ya Washairi teule ............................. 48
4.2.2 Matumizi ya Tashibiha katika Mashairi ya Washairi Teule ....................... 51
4.2.3 Matumizi ya Taswira katika Mashairi ya Washairi Teule .......................... 54
4.2.4 Ishara katika Mashairi ya Washairi Teule .................................................. 57
4.3 Falsafa ya Washairi Teule Juu ya Mwanamke............................................ 60
4.3.1 Falsafa ya Shaaban Robert juu ya Mwanamke ........................................... 60
4.3.2 Falsafa ya Mathias Mnyampala juu ya Mwanamke ................................... 64
4.3.3 Hitimisho ..................................................................................................... 65
SURA TA TANO: MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO ...... 68
5.0 Utangulizi .................................................................................................... 68
5.1 Muhtasari wa Sura za Tasinifu ................................................................... 68
5.2 Hitimisho ..................................................................................................... 70
5.2.1 Usawiri wa Nafasi ya Mwanamke katika Mashairi ya Washairi Teule ...... 70
5.2.2 Matumizi ya lugha ya Kisanaa katika Mashairi ya Washairi Teule ........... 71
5.2.3 Falsafa ya Washairi Wateule juu ya Mwanamke ........................................ 72
5.3 Mapendekezo .............................................................................................. 73
MAREJELEO ............................................................................. 74
VIAMBATANISHO ...................................................................... 80
1
SURA YA KWANZA
UTANGULIZI
1.0 Usuli wa Tatizo la Utafiti
Shaaban Robert ni mwandishi mwenye jina kubwa katika uandishi wa kazi za fasihi
ya Kiswahili ambaye mpaka leo bado hajapata mtu wa badali katika ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati (Njogu na Chimeraha, 1999). Hii ina maana kwamba,
hakuna mtunzi wa kazi za fasihi ambaye ameweza kumfikia Shaaban Robert katika
utunzi wake (Chuachua, 2011). Walibora (2013) anawataja akina Wamitila na
Kezilahabi kuwa ni miongoni mwa watunzi wa kazi mbalimbali za fasihi lakini bado
hawajaweza kumfikia Shaaban Robert. Anaendelea kueleza kwamba, si tu
hawajamfikia kwa idadi ya kazi alizoandika lakini pia hawajamfikia kwa ujuzi wa
kisanaa hasa katika utumizi wa lugha na hasa kipengele cha uteuzi wa maneno au
msamiati anaoutumia katika kazi zake za mashairi, riwaya pamoja na insha.
Kutokana na umahiri wake –Shaaban Robert, katika utunzi wa kazi za fasihi, watafiti
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wamevutiwa katika kuhakiki na kutafiti
kuhusu kazi zake. Kwa hakika Shaaban Robert ni nguli wa utunzi katika fasihi ya
Kiswahili aliyeandika kazi zaidi ya 25 zikiwemo riwaya, mashairi na Insha
(Kezilahabi, 1983). Naye Twaib (2009) anaeleza kwamba, si kwamba hakuna mtunzi
wa fasihi ya Kiswahili aliyeweza kuandika kama Shaaban Robert kwa maana ya
idadi ya kazi pekee bali hakuna aliyemfikia kwa utaalamu wa kutumia lugha katika
kuandika kazi zake. Shaaban Robert alikuwa mtu mahiri katika utumizi wa lugha,
kiasi kwamba kila asomaye kazi zake huvutiwa sana na lugha nzuri ya Kiswahili
iliyotumika katika riwaya, ushairi na insha (Momanyi, 2001).
2
Chuachua (2011) anaeleza kwamba, Shaaban Robert hakuwa mtaalamu wa kutumia
lugha ya Kiswahili kwa ufasaha wake peke yake bali pia aliweza kubuni mandhari
isiyo halisi na kuitumia kuwasilishia mambo mbalimbali yanayotokea katika
mandhari halisi. Mfano mzuri wa kuunga mkono hoja hii unapatikana katika riwaya
za Kusadikika na Kufikirika. Anaendelea kueleza kwamba, kutokana na matumizi
haya ya mandhari isiyo halisi Shaaban Robert ameweza kuwasilisha na kuzungumzia
masuala mbalimbali ambayo yanaigusa jamii nzima na si ile ya Kitanzania peke
yake. Kezilahabi (1976a) anaeleza kwamba, unaposoma riwaya za Kusadikika na
Kufikirika utaona kwamba, mambo yanayoelezwa katika riwaya hiyo yanatokea
katika maeneo mbalimbali ya nchi za Afrika na popote pale duniani ambapo kuna
unyonyaji na utawala usio wa haki na sheria. Hii inatokana na mbinu za kisanaa
alizotumia katika utunzi wa riwaya hizo kuwa ni za hali ya juu mno kiasi cha kuweza
kuakisi mambo ambayo yanafanyika na kutendeka katika nchi mbalimbali duniani.
Mawazo ambayo yanapatikana katika riwaya zake zilizotajwa na Kezilahabi (1976a)
yanapatikana pia katika kazi zake za mashairi za Ashiki Kitabu Hiki na Pambo la
Lugha.
Shaaban Robert alikuwa si mtunzi tu wa kazi za fasihi bali pia alikuwa mwalimu
kwa wanafasihi wengi ambao walimuiga katika kutunga mashairi na kazi nyingine
fasihi. Kwa mfano, Mathias Mnyampala ni miongoni mwa watunzi wa ushairi wa
Kiswahili ambaye kwa maneno yake mwenyewe anakiri kwamba, alijifunza kutoka
kwa Shaaban Robert kutunga mashairi aliyopata kuyatunga katika Waadhi wa
Ushairi, Ngonjera za UKUTA na mengineyo (Abdullazizi, 1969). Mnyampala ni
bingwa katika utunzi wa mashairi yenye kufuata urari wa vina na mizani huku
3
akitumia lugha tamu kwa ulimi wa kuitamka na tumbuizi kwa masikio yenye
kuisikia (Kihore, 1978).
Abdullazizi (1969) anaendelea kueleza kwamba, Mathias Mnyampala alipata
kusifika sana katika tasnia ya utunzi wa mashairi ya Kiswahili baada ya kuanzisha
utanzu wa Ngojera na kuchapishwa katika Ngonjera za UKUTA namba moja na
mbili. Aina hii ya mashairi ni ya majibizano baina ya watu wawili na kuendelea,
jambo ambalo huipa sifa za sanaa za maonesho. Hata, hivyo katika maelezo yao
Mulokozi na Sengo (1995) wanaeleza kwamba, Mnyampala hakuwa mwanzilishi wa
utunzi wa ngonjera kwa kuwa zilikuwepo tangu katika kipindi cha usimulizi pale
mwanadamu alipoanza tu kutumia lugha na kuwasiliana. Jambo jema alilolifanya
Mnyampala ni kuuingiza utanzu wa Ngonjera katika maandishi ambayo tunayaona
katika Ngonjera za UKUTA namba moja na mbili.
Maelezo yanayotolewa katika usuli huu yanaonesha kwamba, Mathias Mnyampala
anatunga mashairi ambayo yanafanana na yale ya Shaaban Robert hasa katika
kipengele cha fani ambapo tumeona naye pia akitumia utunzi wa mashairi ya kufuata
kanuni za urari wa vina na mizani. Pengine inawezekana kukawa na ukaribu wa
dhamira na maudhui katika utunzi wa kazi za wawili hawa. Hili ndilo jambo ambalo
tulikusudia kulifanya katika kazi yetu hii kwa kulinganisha na kulinganua nafasi ya
mwanamke inavyojitokeza na kusawiriwa katika kazi za washairi Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala.
Kwa upande wa mashairi ya Shaaban Robert ni Momanyi (2001) ndio aliyechambua
nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert katika ngazi ya makala.
4
Makala yake yamekuwa ni dira na mwelekeo wetu katika kutaka kulinganisha na
kulinganua nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na yale ya
Mathias Mnyampala. Kuhusu mashairi ya Mathias Mnyampala hatujakutana na
mtafiti au mhakiki ambaye amechunguza nafasi ya mwanamke katika mashairi hayo
jambo ambalo limetuvutia sana kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo
kulizungumzia suala hili. Si watu wa mwanzo katika kulizungumzia suala hili tu bali
pia watu wa mwanzo kwa kulinganisha na kulinganua mashairi ya nguli hawa wawili
wa ushairi wa Kiswahili. Hivyo basi, utafiti huu umefanywa ili kulinganisha na
kulinganua nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala.
1.1 Tatizo la Utafiti
Utafiti na uhakiki kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii umefanywa kwa kiasi
kikubwa katika kazi za Shaaban Robert za riwaya kuliko katika mashairi yake
(Momanyi, 2001). Kwa upande wa mashairi ya Mathias Mnyampala hatujakutana na
mtafiti hata mmoja ambaye amechambua au kuhakiki masuala ya kijinsia katika
mashairi hayo. Baada ya kulifahamu hili, Momanyi (2001) aliamua kuandika makala
juu ya nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert. Katika makala yake
alionesha kwamba, Shaaban Robert anamsawiri mwanamke katika hali chanya na
hali hasi. Kwa bahati mbaya sana alishindwa kueleza kwa undani ni kwa vipi
mwanamke anasawiriwa katika hali hizo mbili na badala yake akaishia kugusiagusia
tu.
Si hivyo tu, bali pia hakuna mtafiti yeyote ambaye amefanya utafiti wake kwa nia ya
kulinganisha usawiri wa nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na
5
mashairi ya Mathias Mnyampala ili kupata uelewa mpana zaidi kuhusu nafasi ya
mwanamke katika mashairi ya Kiswahili. Tunayasema haya kwa sababu, watunzi
hawa wawili wanasifika na kuheshimika sana katika utunzi wa mashairi, kwa hivyo
kutathimini usawiri wao wa nafasi ya mwanamke umetupatia uelewa mpana zaidi wa
masuala ya kijinsia katika fasihi ya Kiswahili. Hivyo, katika tasinifu hii
tumechambua na kuhakiki kwa kina nafasi ya mwanamke katika mashairi ya
Shaaban Robert na kulinganisha na kulinganua na mashairi ya Mathias Mnyampala.
1.2 Malengo ya Utafiti
Utafifi huu utakamilika baada ya kukamilika kwa lengo kuu moja na madhumuni
mahususi matatu. Lengo kuu na mdhumuni mahususi ni haya yafuatayo:
1.2.1 Lengo Kuu la Utafiti
Lengo kuu la utafiti huu ni kulinganisha nafasi ya mwanamke katika mashairi ya
Shaaban Robert na Mathias Mnyampala ili kufahamu falsafa na mtazamo wa wasanii
hawa juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii.
1.2.2 Malengo Mahususi
Utafiti huu una jumla ya malengo mahususi matatu ambayo ni:
1. Kulinganisha na kulinganua usawiri wa nafasi ya mwanamke katika mashairi
ya Shaaban Robert na yale ya Mathias Mnyampala.
2. Kulinganisha na kulinganua matumizi ya lugha ya kisanaa inayotumiwa na
Shaaban Robert na Mathias Mnyampala katika kusawiri nafasi ya mwanamke.
3. Kubainisha falsafa ya Shaaban Robert na ile ya Mathias Mnyampala juu ya
nafasi waliyompa mwanamke katika mashairi yao.
6
1.2.3 Maswali ya Utafiti
Utafiti huu unakusudia kujibu maswali yafuatayo:
1. Usawiri wa nafasi ya mwanamke unalingana na kutofautiana vipi katika
mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala?
2. Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wanafanana na kutofautiana vipi
katika matumizi ya lugha ya kisanaa wanaposawiri nafasi ya mwanamke?
3. Ni ipi Falsafa ya Shaaban Robert na ile ya Mathias Mnyampala juu ya nafasi
waliyompa mwanamke katika mashairi yao?
1.3 Umuhimu wa Utafiti
Utafiti huu utakuwa rejeleo muhimu kwa wanataalimu wote wanaojihusisha na
masuala ya fasihi ya Kiswahili hususani Ushairi wa Kiswahili. Wanafunzi wa
masuala ya fasihi watautumia utafiti huu katika kujifunza namna ushairi ulivyo na
uwezo wa kusawiri nafasi ya mwanamke katika jamii.
Kwa watafiti wa masuala ya fasihi watauona utafiti huu kama sehemu muhimu ya
wao kupata maeneo zaidi ya kufanyia utafiti katika kazi za Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala. Shaaban Robert ameandika kazi nyingi mno ambazo zinahitaji
kufanyiwa uhakiki na uchambuzi zaidi wa kitaaluma. Kupitia utafiti huu, watafiti
wanaweza kuyaona maeneo mbalimbali ya kuyashughulikia kwa kuyafanyia utafiti.
Wahadhiri wa vyuo vikuu watautumia utafiti huu kama rejeleo muhimu katika
kuandaa vitabu, makala, na insha kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wao. Hii
itawafanya wasipate taabu ya kusoma kitabu chochote cha Shaaban Robert na kutoka
patupu na badala yake, maelezo yaliyotolewa katika uchambuzi wetu ni darasa tosha
7
kwao. Watalaamu wa masuala ya jinsia pamoja na wanaharakati wa masuala hayo
watauona utafiti huu kuwa ni sehemu ya kutoa elimu kwa umma wa wasomaji
kuhusu masuala la kijinsia katika jamii.
Utafiti huu utakuwa na umuhimu wa kubainisha falsafa ya Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala kuhusu nafasi ya Mwanamke katika jamii ya Watanzania. Yapo
baadhi ya maandishi ambayo yameeleza kwa ufupi kuhusu mtazamo wa Shaaban
Robert kwa wanawake (Senkoro, 1988). Hata hivyo, maandishi hayo yamegusia tu
juu ya mtazamo wa mwandishi Shaaban Robert kuhusu wanawake bila ya
kuyafanyia uchambuzi wa kina. Utafiti huu umechunguza kwa kina kuhusu falsafa
ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala kwa wanawake na nafasi yao katika
jamii.
1.4 Mipaka ya Utafiti
Utafiti huu ulijikita katika kuchunguza nafasi ya mwanamke katika mashairi
yaliyotungwa na Shaaban Robert na Mathias Mnyampala tu. Katika utafiti huu
hatukuzungumzia riwaya pamoja na insha alizotunga Shaaban Robert bali
tumeshughulikia diwani zake za Pambo la Lugha na Ashiki Kitabu Hiki peke yake.
Kwa upande wa Mnyampala tumetumia kazi zake za Waadhi wa Ushairi na
Ngonjera za UKUTA namba Moja. Pia, tathimini ya masuala ya kijinsia- nafasi ya
mwanamke katika kazi hizo imefanywa kifasihi tu na si vinginevyo. Ni vema
ikaeleweka kwamba, nafasi ya mwanamke katika jamii inaweza kuelezwa kwa
namna nyingi kama vile kisiasa, Kitaaluma za Maendeleo, Kisosholojia na kadhalika.
Sisi tumetathimini nafasi ya mwanamke katika kazi teule kwa mtazamo wa kifasihi.
8
1.5 Matatizo ya Utafiti na Utatuzi Wake
Utafiti huu unategemea kukumbana na matatizo kadhaa; kwanza ni suala la pesa,
mazingara na ugeni wa mtafiti katika nchi ya Tanzania. Kwa sababu mtafiti anatokea
Libya hivyo mazingira ya Tanzania yatakuwa magumu kwake na pia kuelewa mila
na desturi za Watanzania kwa haraka na jinsi ya kukabiliana na hali hiyo ili kupata
data zinazofaa kujibu maswali ya utafiti. Hata hivyo, changamoto hizi zilitatuliwa
kwa mtafiti kutafuta mtafiti msaidizi ambaye alimuongoza katika mazingira haya
mageni kwake. Mtafiti msaidizi alimsaidia katika zoezi la kukusanya data pamoja na
kumfundisha baadhi ya mila na desturi za jamii ya Waswahili.
1.6 Hitimishi
Sura hii imewasilisha vipengele vinavyohusu utangulizi wa utafiti. Vipengele hivyo
ni usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, lengo kuu la utafiti, madhumuni mahususi
ya utafiti na maswali ya utafiti. Vipengele vingine ni umuhimu wa utafiti, mipaka ya
utafiti, matatizo na utatuzi wa matatizo ya utafiti. Sura inayofuata ni ya pili ambayo
inawasilisha utalii wa kazi tangulizi na mkabala wa kinadharia.
9
SURA YA PILI
UTALII WA KAZI TANGULIZI NA MKABALA WA KINADHARIA
2.0 Utangulizi
Katika sura hii tumetalii kazi tangulizi ambazo zimetafiti na kuhakiki nafasi ya
mwanamke katika hususani zile za Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Kwa
hakika, kazi nyingi za uhakiki zimefanywa kuhusu maandishi ya Shaaban Robert.
Miongoni mwa wachambuzi na wahakiki hao ni Kezilahabi (1976a), Kezilahabi
(1983), Njogu na Chimerah (1999), Momanyi (2001), Twaib (2009) na Chuwachuwa
(2011). Lakini katika tafiti zao hawakulenga kuchunguza nafasi ya mwanamke katika
mashairi ya Shaaban Robert. Watafiti hao walikuwa na malengo tofauti na ya utafiti
wetu lakini wamedokeza mambo ya msingi ambayo yatatusaidia katika utafiti wetu.
Maelezo zaidi yanatolewa katika sehemu inayofuata.
2.1 Ushairi wa Shaaban Robert
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 mwezi wa kwanza mwaka 1909. Shaaban Robert
alianza shule mwaka 1922 na kumaliza 1926 katika shule ya Kichwele ambayo kwa
sasa inafahamika kama Uhuru Mchanganyiko. Alipenda sana kusoma na
kujiendeleza kielimu lakini jitihada zake hazikuzaa matunda kwa haraka kwa sababu
ziliporwa na wakoloni kwa lengo la kumtumia kama chombo cha kutawalia. Hata
hivyo mwaka 1932 aliendelea na masomo kwa njia ya posta ambapo mwaka 1934
alitunukiwa Diploma ya Fasihi. Mwaka 1936-37 alitunukiwa cheti cha English Level.
Ni dhahiri kuwa Shaaban Robert alikuwa ni mtu mwenye juhudi kubwa katika
kujiendeleza kielimu na kama si wakoloni angalifika katika ngazi za juu zaidi.
10
Ilipofika mwaka 1926 alianza kazi katika idara ya Forodha Tanga. Hapo alidumu
kwa miaka takribani 18. Mwaka 1944-1946 alihamishiwa Idara ya Wanyamapori
huko Mpwapwa. Mwaka 1946 alirudishwa Tanga na kuwa Afisa Ardhi wa jimbo la
Tanga. Aidha barua zake zinaonesha pia aliwahi kufanya kazi katika mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam na Kisiju. Shaaban Robert alifariki tarehe
20.6.1964 na kuzikwa huko Vibambani tarehe 21.6.1962.
Senkoro (1968) anaeleza juu ya Mwamko wa kisiasa katika mashairi ya Shaaban
Robert na kwamba, nguli huyu wa fasihi ya Kiswahili alikuwa ni mtaalamu wa
kutumia lugha na mandhari ya kuhamasisha umma kudai haki zao bila ya mdaiwa
kutambua hilo kwa haraka. Katika Mashairi na Insha kwa mfano, tunaona namna
Shaaban Robert alivyo bingwa wa kuwasilisha dhamira za kisiasa katika mashairi
yake kwa kutumia lugha ya kisiasa.
Mawazo haya ya Senkoro (1968) tunakubaliana nayo kwa kiasi kikubwa kwa kuwa
si yeye wa kwanza kumsifu Shaaban Robert kuwa ni mtunzi mashuhuri katika
utumizi wa lugha ya Kiswahili katika kazi zake. Mawazo haya yanaungwa mkono na
Njogu na Chimerah (1999), Wamitila (2008) na Ndulute (1987). Hata hivyo,
halikuwa lengo la Senkoro (1968) kuhakiki nafasi ya mwanamke katika kazi za
kishairi za Shaaban Robert lakini ametupatia mwanga wa kufahamu kwamba,
Shaaban Robert ni bingwa wa matumizi ya lugha ya kisanaa katika utunzi wake wa
mashairi. Nasi tumeyasoma mashairi yake kwa utulivu ili kuona namna
anavyomsawiri mwanamke kupitia lugha hiyo ya kisanaa na kulinganisha na Mathias
Mnyampala.
11
Maganga (1971) anaeleza kwamba, Shaaban Robert ni mtu ambaye alikuwa na
mawazo ya kimapinduzi ambayo yalilenga kumkomboa kila mtanzania hususani
mwanamke kutokana na mateso mbalimbali yanayomkumba katika jamii. Shaaban
Robert anaonesha kwamba, mwanamke ndiye anayebeba ujauzito wa mtoto kwa
miezi tisa na baadaye kumlea mtoto huyo mpaka akaweza kujitegemea yeye
mwenyewe. Katika mazingira mengine mwanamke huachiwa majukumu ya kulea
watoto peke yake huku mwanaume akiishia katika ulevi na anasa nyingine za
kidunia. Shaaban Robert aliipinga hali hii na kuitaka jamii kumhurumia mama na
kumpatia msaada wowote atakaouhitaji ili aishi maisha mazuri.
Mawazo ya Maganga (1971) hapo juu yanaonesha kwamba, Shaaban Robert
amempatia mwanamke nafasi ya ulezi na huruma katika jamii huku mwanamme
akionekana kutokuwa na sifa hizo. Mawazo haya tumeyachukua na kuyafanyia
utafiti wa kina ili kuona ni kwa vipi mwanamke anatekeleza majukumu haya katika
kazi za Shaaban Robert huku tukilinganisha na yale ya Mathias Mnyampala.
Ndulute (1994) aliandika juu ya ushairi wa Shaaban Robert na kujadili mambo
mengi kuhusu mashairi hayo. Kwa mfano, alieleza juu ya fani na maudhui kwa
ujumla wake kama inavyosawiriwa na Shaaban Robert. Katika maelezo yake
amegusia kwamba, Shaaban Robert anazungumzia masuala ya jinsia katika jamii
akionesha kwamba, mwanamke ni kiumbe ambaye anastahili kupatiwa heshima
kubwa katika jamii kutokana na mambo mbalimbali anayoifanyia jamii katika
maisha yake ya kila siku. Ingawa, Ndulute (ameshatajwa) hakuzamia katika kueleza
ni kwa vipi sifa hizo anazopewa mwanamke zinajitokeza katika kazi hizo za Shaaban
Robert lakini ametufungua macho kwamba, nafasi ya mwanamke inajadiliwa na
12
kujitokeza katika mashairi ya Shaaban Robert. Tumefanya utafiti wa ndani zaidi ili
kuonesha nafasi aliyopewa mwanamke katika mashairi hayo pamoja na
kuyalinganisha na kulinganua na yale ya Mathias Mnyampala.
Sengo (1975) aliandika juu ya mada isemayo, Shaaban Robert: Uhakiki wa
Maandishi yake. Katika uhakiki huu, Shaaban Robert anaelezwa kuwa ni mtu
ambaye alijali sana ubinadamu katika jamii. Alipenda kuona kila mtu anapata
heshima yake, haki zake na kutendeana mema kati ya wanadamu katika jamii.
Mawazo haya yalikuja katika kipindi ambacho Tanganyika ilikuwa imetawaliwa na
Wakoloni ambao hawakujali haki za Wanatanganyika. Kwa mantiki hiyo Shaaban
Robert aliwataka Wakoloni hao kuwapatia wananchi haki zao pamoja na
kuwaheshimu. Maelezo haya ya Sengo (1975) yana umuhimu mkubwa katika
kuujenga utafiti wetu kwa sababu yanamwelezea Shaaban Robert kama mtetezi wa
haki katika jamii. Kutokana na hili tunaona kwamba, Shaaban Robert alitetea haki za
watu wote katika jamii wakiwamo wanawake na wanaume.
Kwa msingi huo basi, katika utafiti wetu tumechunguza nafasi aliyopewa mwanamke
katika kudai na kupatiwa haki zake za msingi katika jamii iliyokuwa ikitawaliwa na
Wakoloni. Ingawa uhakiki wa Sengo (ameshatajwa) haukulenga kuchunguza nafasi
aliyopewa mwanamke katika maandishi ya Shaaban Robert lakini umetupatia
ufahamu wa kutosha, kwamba nafasi ya mwanamke inatokeza na kujadiliwa katika
ushairi wa Shaaban Robert. Katika utafiti wetu tumechunguza kwa kina ni kwa vipi
nafasi ya mwanamke inajitokeza katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala.
13
Kezilahabi (1976a) aliandika kazi yake ambayo aliipa jina la Ushairi wa Shaaban
Robert. Katika kazi hii Kezilahabi ameanza kwa kumsifu Shaaban Robert kuwa ni
mtunzi mashuhuri na adhwimu katika tasinia ya fasihi ya Kiswahili asiyekuwa na
mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Jambo kubwa lililomvutia
Kezilahabi mpaka kuamua kumsifu Shaaban Robert ni ule ubingwa wake wa
matumizi ya lugha ya kisanaa ambao pia umeelezwa na Senkoro (1968). Anasema
kwamba, Shaaban Robert alikuwa ni bingwa wa uteuzi wa misamiati ambao watunzi
wa baada yake hawawezi kabisa kujinasibisha naye hata kidogo.
Hata hivyo, Kezilahabi (1976a) anaeleza kwamba, Shaaban Robert alijikita katika
kueleza baadhi ya mambo ambayo katika ulimwengu wa kawaida hayawezekani
kutokea. Miongoni mwa mwambo hayo ni lile na kutolea mifano ya watu wema
wasio na makosa hata kidogo na watu waovu tu wasio na wema hata kidogo. Hili ni
jambo ambalo halina uhalisia katika jamii. Suala hili tunakubaliana nalo na tunaona
kwamba, linatoa mchango muhimu wa kukamilisha utafiti wetu. Hata hivyo,
Kezilahabi hakuelewa kwamba, utunzi wa Shaaban Robert ulikuwa hivyo kwa nia ya
kuhimiza mema na kukataza maovu katika jamii. Haina maana kwamba, Shaaban
Robert alikuwa hatambui kwamba, hakuna mtu mwema tu asiye na chembe ya uovu
na hakuna pia mtu muovu tu asiye na chembe ya wema ila alifanya hivyo kwa
makusudi maalumu. Mawazo haya tumeyachukua na kuyafanyia kazi katika utafiti
wetu ili kuona ni kwa namna gani yanamlenga mwanamke na kulinganisha na
kulinganua na mashairi ya Mathias Mnyampala.
Kezilahabi (1976b) aliandika tasinifu yake ya Uzamili juu ya Shaaban “Robert
Mwandishi wa Riwaya.” Ingawa kazi hii ilihusu riwaya lakini pia alitumia kazi moja
14
ya kishairi iitwayo Mapenzi Bora sambamba na riwaya za Shaaban Robert. Pamoja
na mambo mengi ambayo ameyaonesha katika tasinifu yake, amekiri kwamba, mama
ni kiumbe ambaye amesawiriwa na Shaaban Robert kama kiumbe mvumilivu na
mwenye unyenyekevu mkubwa katika maisha. Kutokana na hali hii, mwanamke
amekuwa kiigizo chema cha ukarimu, upole na hekima katika jamii na kuufanya
ulimwengu kuwa mahali salama pa kuishi watu wote. Lau ingelitokezea mwanamke
kukosa sifa hizo basi dunia ingekuwa mahali pabaya pa kuishi. Mawazo haya
tunayakubali na tumeyafanyia kazi katika utafiti wetu ili kueleza kwa kina namna
mwanamke anavyosawiriwa katika mashairi ya Shaaban Robert na yale ya Mathias
Mnyampala.
Momanyi (2001) aliyandika makala juu ya nafasi ya mwanamke katika ushairi wa
Shaaban Robert. Katika makala yake hii alionesha kuwa Shaaban Robert anamsawiri
mwanamke katika hali mbili. Hali ya kwanza ni ile inayomtazama mwanamke kama
kiumbe ambaye ni mlezi katika jamii, mkarimu, mpole, mnyenyekevu, mwenye
huruma na kadhalika. Hali ya pili ni ile ambayo inamtazama mwanamke kama
kiumbe duni katika jamii. Mawazo haya ni muafaka kwa sababu yanaeleza mambo
kama yanavyotokea katika jamii. Wapo wanawake ambao wanafanya mambo
yanayokubalika katika jamii na wapo wengine ambao wanafanya yale
yasiyokubalika katika jamii. Huu ndio uhalisia katika maisha ya jamii na msanii
makini ni lazima ayasawiri hivyo. Mawazo ya Momanyi ni msingi muhimu katika
kusukuma mbele utafiti wetu na tumeyachukua na kuyafanyia kazi katika utafiti huu.
Hata hivyo, makala yake ilikuwa finyu mno kiasi cha kushindwa kuieleza
kinaganaga nafasi ya mwanamke katika ushairi wa Shaaban Robert. Utafiti huu
15
tulioufanya umelenga kuziba pengo hilo kwa kuchunguza nafasi ya mwanamke
katika mashairi ya Shaaban Robert ili kuona ni jinsi gani msanii huyo anaitumia
sanaa yake kuwasilisha falsafa na mtazamo wake kuhusu nafasi ya mwanamke katika
jamii huku tukimlinganisha na kumlinganua na Mathias Mnyampala.
2.2 Ushairi wa Mathias Mnyampala
Mathias Mnyampala alizaliwa mwaka wa 1917 na kufariki dunia mwaka wa 1969.
Alizaliwa katika kitongoji cha Muntundya katika kijiji cha Ihumwa katika wilaya ya
Chamwino katika mkoa wa Dodoma. Alifanya kazi kama karani wa kodi katika
serikali ya kikoloni na na baada ya uhuru aliendelea na kazi ya utumishi wa umma
katika mahakama kama hakimu. Aliandika vitabu zaidi ya 25. Alichaguliwa kuwa
mwenyekiti wa UKUTA katika mwaka wa 1961(Abdulazizi, 1969). Kazi zake za
ushairi hasa utunzi wa Ngonjera ulimfanya kupata sifa nyingi sana katika tasinia ya
fasihi ya Kiswahili. Wapo watafiti kadhaa ambao wametafiti na kuhakiki kazi zake
ingawa si kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa Shaaban Robert. Kati ya waliohakiki
na kutafiti kazi zake ni:
Abdullazizi (1969) ambaye aliandika juu ya ukumbusho wa Marehemu Sheikh
Mathias E. Mnyampala. Katika makala yake haya, anamsifu Mnyampala kuwa ni
mtunzi mashuhuri ambaye alianzisha utanzu wa ngonjera katika ushairi wa Kiswahili
na kueleza dhamira mbalimbali. Miongoni mwa dhamira hizo ni zile zinazohusu
umoja na mshikamano katika jamii, umuhimu wa kuishi Kijamaa na Kujitegemea,
malezi na maadili mema katika jamii, uongozi bora na imara, haki na usawa katika
jamii na kadhalika. Mawazo ya Abdulazizi (1969) ni muhimu katika kuupeleka
mbele utafiti huu kwa sababu unagusia mambo ambayo ni muhimu kwetu
16
kuyachunguza kwa kina. Anapotaja masuala ya umoja na mshikamano katika jamii
bila shaka anazungumzia umoja baina ya mwanamke na mwanamme. Tumefanya
utafiti wa kina katika mashairi ya Mnyampala ili kuona nafasi anayompa mwanamke
katika kazi zake na kulinganisha na kulinganua na zile za Shaaban Robert.
Kihore (1978) aliandika makala yake juu ya Waadhi wa Ushairi diwani ya mashairi
ya Mathias Mnyampala. Katika uchambuzi wake amebainisha vipengele mbalimbali
vya kifani na kimaudhui. Kwa upande wa fani, anaonesha kwamba, Mathias
Mnyampala ni bingwa wa kuandika mashairi ambayo yanafuata urari wa vina na
mizani (Mulokozi na Kahigi, 1979). Kwa upande wa maudhui, anaeleza kwamba,
Mathias Mnyampala anaeleza juu ya dhaimira za ujenzi wa jamii mpya iliyo na
uongozi bora, usawa, haki, heshima kwa watu wake, upendo, amani na kuhurumiana
baina ya wanadamu. Ingawa Kihore (1978) hakuwa na lengo la kuzungumzia nafasi
ya mwanamke katika mashairi ya Mathias Mnyampala lakini yapo mambo kadhaa
ambayo ameyagusia na yanatuelekeza kufahamu kwamba, katika mashairi ya
Mnyampala kuna usawiri wa nafasi ya mwanamke katika jamii. Tumechunguza kwa
kina na kuonesha ni kwa vipi nafasi ya mwanamke inajitokeza katika mashairi ya
Mathias Mnyampala na kulinganisha na kulinganua na mashairi ya Shaaban Robert.
Ndulute (1985) anaeleza kwamba, Mathias Mnyampala ni miongoni mwa washairi
wa Kiswahili ambaye ameacha utajiri mkubwa sana katika tasinia ya ushairi wa
Kiswahili. Kwanza alianzisha utanzu wa Ngonjera ambao unaonesha kwamba,
ushairi ni tukio halisi ambalo linaweza kutendwa kwa kuigizwa kama ilivyo katika
utanzu wa tamthilia na maigizo. Pili alikuwa ni miongoni mwa washairi ambao
amedumisha kanuni za utunzi wa ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia umbo lake la
17
asili. Mawazo haya tunakubaliana nayo na kwamba, yanatoa mchango muhimu
katika kusukuma mbele utafiti huu.
Hata hivyo, si kweli kwamba, Mnyampala ndiye aliyeaanzisha utanzu wa ngonjera
kwa kuwa utanzu huu ulikuwepo tangu siku nyingi za kipindi cha usimulizi ila
ingefaa kusema kwamba, yeye ameutia katika maandishi. Nia kuu ya utafiti huu ni
kuchunguza nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala kwa hivyo mawazo ya Ndulute (ametajwa) hapo juu yametupatia
muongozo kamili wa kufanikisha nia yetu hii.
2.3 Mkabala wa Kinadharia
Katika sehemu hii tunaeleza nadharia ambayo imetumika katika kuwezesha
kukamilika kwa madhumuni mahusui ya utafiti wetu. Nadharia hiyo ni ile ya
Ufeministi ambayo inafafanuliwa kwa kina hapa chini.
2.3.1 Nadharia ya Ufeministi
Kuna nadharia nyingi ambazo hutumika kuchambua na kuhakiki kazi za kifasihi.
Nadharia hizo hutumiwa ili kutoa muongozo kamili juu ya namna kazi za mwandishi
fulani zitakavyochambuliwa na kuhakikiwa. Kwa mfano, katika utafiti wetu
tulikusudia kutafiti nafasi ya mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala kwa hivyo ni lazima tutumie nadharia ambayo inaelezea na
kufafanua masuala ya jinsia yalivyo, yanavyotokea na yanavyotakiwa kuwa katika
jamii. Hivyo basi, katika utafiti huu tumetumia nadharia ya Uchanganuzi Nafsia
katika Mtazamo wa Kike (Feminist Psychoanalytic Theory). Hii ni nadharia
iliyoibuka kutokana na kazi zilizoasisiwa na Jacques Lacan kama alivyonukuliwwa
18
na Momanyi (2001). Nadharia hii inahakiki matini katika misingi ya uchanganuzi
nafsia. Huzingatia kuweko kwa nafsi bandia au nafsi isiyo halisi iliyojengwa
kutokana na mielekeo ya kiuana, utaratibu fiche wa kisaikolojia pamoja na taasubi za
kiume.
Katika utaratibu fiche, maumbo halisi ya kiisimu katika akili ya mwanamke
hughubikwa na badala yake maumbo ya kidhahania huimarishwa. Maumbo haya
yasiyo na uhusianao wowote na uhalisia wake kama binadamu ndiyo yanayobainika
hususan kupitia lugha na tabia yake. Utaratibu huu ambao ni wa kiishara ndio
unaoashiria tofauti za kiuana zinazopatikana katika utamaduni wa jamii.
Kwa mujibu wa mtazamo huu, nafasi ya mwanamke imefungamana na lugha
inayomzungumzia na lugha inayoashiria uana wake. Nafasi hii hufinyangwa na jamii
kupitia asasi mbalimbali ili aweze kukubalika katika utaratibu huo wa kishara.
Uchanganuzi nafsia katika mtazamo wa kike ni nadharia bia ya uumbaji wa nafsi
katika misingi ya uana.
Sababu ya kuteua nadharia hii, ni kwamba wapo watafiti ambao pia wametumia
nadharia hii katika kuchambua mahusiano ya mwanamke na mwanamume katika
kazi za fasihi mfano Momanyi (2001). Hatimaye nadharia hii ilimweza kumfikisha
kwenye mafanikio katika kuibua suala la ujinsia katika fasihi na kutimiza malengo
yake ya utafiti. Aidha uhakiki wa kazi za fasihi kwa kutumia nadharia hii una wajibu
wa kuzingatia kuwepo kwa taasubi za kiume zilizoimarishwa ndani ya utaratibu wa
kiishara katika mfumo wa kuumeni. Taasubi hizo ndizo zinazomdunisha mwanamke
na kumweka katika kitengo maalumu kijamii (Momanyi, 2001).
19
Maudhui ya nadharia hii yanaonesha kwamba, mwanamke ni kiumbe ambaye
amedunishwa sana katika jamii kutokana na kushamiri kwa mfumo dume katika
jamii. Mfumo dume katika jamii unamfanya mwanamke kuwa ni kiumbe
aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumtumikia na kumstarehesha
mwanaume kwa njia na namna mbalimbali (Momanyi, 2007). Kwa mfano,
mwanamke anaonekana kuwa ni kiumbe wa kukaa nyumbani akifanya kazi za
kupika chakula, kufua nguo, kuosha vyombo, kusafisha nyumba, kulea watoto, kulea
ndugu wa mume na kadhalika. Wakati mwanamke anatazamwa kwa namna hii,
mwanaume ni kiumbe aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kufanya kazi
za kuingiza kipato. Hali hii kwa hakika imemfanya mwanamke kuonekana kama
kiumbe dhaifu mbele ya mwanamme kwa sababu mwanamke anafanya kazi ambazo
haziingizi kipato na anategemea kipato cha mwanamme katika kuendeshea maisha
yake. Hii ina maana kwamba, pasipokuwepo mwanaume basi mwanamke hawezi
kuishi maisha mazuri.
Hivyo basi, tumeyatumia maudhui ya nadharia hii katika kuchunguza nafasi ya
mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Nadharia hii
imetusaidia kuona ni kwa vipi Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wanaieleza
nafasi ya mwanamke katika mashairi yao huku tukirejelea maudhui ya nadharia hii
tuliyoiteua kuitumia.
2.4 Hitimishi
Utalii wa kazi tangulizi uliofanywa katika sura hii unaonesha kuwa, hakuna mtafiti
aliyefanya utafiti wa kulinganisha na kulinganua nafasi ya mwanamke katika
mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Hili lilibainika baada ya sura
20
hii kutalii kazi tangulizi zilizotafiti ushairi wa Shaaban Robert na ushairi wa Mathias
Mnyampala. Nadharia ya Ufeministi ndiyo iliyotumika katika kuchambua data za
utafiti huu.
21
SURA YA TATU
NJIA ZA UTAFITI
3.0 Eneo la Utafiti
Babbie (1992) anaeleza kwamba, eneo la utafiti ni mahali ambapo utafiti unafanyikia
au unakusudiwa kufanyikia. Katika eneo la utafiti ndipo data za utafiti hupatikana
kwa mtafiti kufanya usaili, mahojiano, kushuhudia au kushiriki shughuli au tukio
fulani pamoja na watafitiwa. Eneo la utafiti ni jiji la Dar es salaam na jiji la Tanga.
Jiji la Dar es Salaam limeteuliwa kwa sababu ni mahali ambapo kunapatikana
machapisho mbalimbali yanamuhusu Shaaban Robert na Mathias Mnyampala kuliko
sehemu nyingine yoyote ile katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kwamba,
maktaba kubwa ambazo ndizo zenye machapisho yanayomuhusu Shaaban Robert
yanapatikana. Nalo jiji la Tanga limeteuliwa kwa sababu ndipo Nyumbani kwa
Shaaban Robert ambapo wanapatikana ndugu jamaa na marafiki ambao tumewasaili.
Sehemu maalumu itakapofanyikia utafiti huu ni Vibambani nje kidogo ya jiji la
Tanga. Pia tutafanya utafiti katika Manispaa ya Dodoma ambako ndiko nyumbani
kwa Mathias Mnyampala na familia yake inapatikana huko. Maeneo haya matatu
yametupatia data tunazozihitaji ili tuweze kufanikisha malengo ya utafiti wetu.
3.1 Kundi Lengwa
Kulingana na Cresswell (2009) kundi lengwa ni wanachama wote, mtu mmoja,
kikundi au elementi ambazo mtafiti amekusudia kuzihusisha katika utafiti wake.
Kwa hiyo katika utafiti huu walengwa ni diwani mbili za Shaaban Robert ambazo ni
Pambo la Lugha na Ashiki Kitabu Hiki na Ngonjera za UKUTA na Waadhi wa
Ushairi. Katika kazi hizo mbili za kila mmoja ndimo tulikopata data za kueleza
22
namna Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wanavyoisawiri nafasi ya
mwanamke katika jamii. Kundi la pili litakuwa ni watoto, ndugu, jamaa na marafiki
wa Shaaban Robert ambao wanapatika katika jiji la Tanga na wale wa Mathias
Mnyampala wa Dodoma. Kundi la tatu ni wale ambao wametafiti kazi za wasanii
hawa wawili katika utunzi wao wa mashairi.
Katika kundi hili la pili tutapata data zinazoeleza namna Shaaban Robert alivyokuwa
akiishi na wanajamii wenzake katika familia yake na nje ya familia hususani
mtazamo na matendo yake dhidi ya wanawake. Kundi la tatu litawahusu watafiti na
wahakiki ambao wameshughulikia kazi za Shaaban Robert kwa namna moja au
nyingine. Watafitiwa hawa walitueleza wao wanaionaje nafasi ya mwanamke katika
mashairi ya Shaaban Robert na yale ya Mathias Mnyampala walipokuwa
wakiyasoma mashairi hayo katika harakati za kukamilisha malengo ya utafiti wao.
3.2 Sampuli ya Utafiti
Uteuzi wa sampuli ya utafiti kama unavyoelezwa na Young (1984) ni mchakato wa
kuchagua kikundi cha vitu au watu ili kitumike katika utafiti kama kiwakilisho cha
kundi lote linalotafitiwa kwani sio rahisi kutafiti kundi zima la watafitiwa. Sampuli
ya utafiti huu imeganyika katika makundi matatu. Kundi la kwanza linajumuisha
diwani mbili za mashairi ya Shaaban Robert ambao ni Pambo la Lugha na Ashiki
Kitabu Hiki na Ngonjera za UKUTA pamoja na Waadhi wa Ushairi. Kundi la pili ni
la watafitiwa ambao ni watoto, ndugu, jamaa na marafiki wa Shaaban Robert ambao
jumla yao ilikuwa ni 10 na kundi la tatu ni la watafitiwa ambao wameshughulikia
kazi za Shaaban Robert na Mathias Mnyampala ambao jumla yao ni 10.
23
3.3 Mbinu za Kukusanyia Data
Katika kukusanya data za utafiti huu tumetumia mbinu tatu ambazo ni; mbinu ya
usaili, hojaji na maktaba.
3.3.1 Mbinu ya Usaili
Usaili ni mbinu ya kukusanya data kwa mahojiano ya ana kwa ana kati ya mtafiti na
mtafitiwa. Mtafiti huandaa maswali na kuyaandika katika dodoso kwa ajili ya
kuwauliza watafitiwa wake ili kupata data zinaweza kusaidia kujibu maswali yake ya
utafiti (Kothari, 2009). Tumeitumia mbinu hii kufanya usaili na watafitiwa ambao
walishatafiti maandishi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala kwa namna moja
au nyingine. Watafitiwa hawa wametueleza ni kwa vipi Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala wanazungumzia nafasi ya mwanamke katika jamii. Mbinu hii ya usaili
ni madhubuti katika kumpatia mtafiti data za kutosha kumwezesha kujibu maswali
ya utafiti wake kwa muda mfupi (Borg na Gall, 2003). Vilevile, mbinu hii humsaidia
mtafiti kupata data ambazo hapo awali alikuwa hajategemea kuzipata. Si hivyo tu
bali pia, mbinu hii inamwezesha mtafiti kuuliza maswali ya ziada kutegemeana na
msailiwa anavyojibu maswali yake. Hata hivyo, mapungufu ya mbinu hii ni
kwamba, inatumia muda mrefu sana na mtafiti hawezi kupata data kutoka kwa
watafitiwa wengi kwa muda mfupi. Mapungufu ya mbinu hii yalitatuliwa na
matumizi ya mbinu ya Hojaji.
3.3.2 Hojaji
Hojaji ni mbinu ya kukusanya data maskanini kwa mtafiti kuandaa maswali katika
karatasi na kuacha wazi nafasi za kujazwa na watafitiwa pale watakapopatiwa hojaji
hizo (Cohen na Wenzake, 2000). Mbinu hii humwezesha mtafiti kukusanya data
24
nyingi kwa muda mfupi kutoka kwa watafitiwa wengi tofauti na ilivyokuwa katika
mbinu ya usaili. Pia, mbinu ya hojaji humwezesha mtafiti kutumia muda wake vizuri
kwani wakati wahojiwa wanapokuwa wanajaza hojaji yeye huendelea na shughuli
nyingine katika harakati za kukamilisha utafiti wake. Mapungufu ya mbinu hii ni
kwamba, haifai kutumika kuwahoji watafitiwa ambao hawajui kusoma na kuandika.
Upungufu huu unalituliwa na mbinu ya usaili ambayo tumeieleza hapo juu. Mbinu
hii ilitumika kukusanya data kutoka kwa baadhi ya wataalamu wa fasihi ambao
wametafiti kazi za ushairi za watunzi hawa wawili.
3.3.3 Mbinu ya Usomaji Makini
Hii ni mbinu ya utafiti inayomtaka mtafiti kusoma kazi alizoziteua kwa makini ili
aweze kupata data anazokusudia zijibu maswali yake ya utafiti (Cresswell, 2009;
Robson, 2007; Best na Khan, 1993). Kwa mantiki hii, mtafiti alisoma kazi nne za
ushairi alizoziteua na kila alipokutana na aya, sentensi, au neno ambalo linahusiana
na malengo ya utafiti alilinukuu katika daftari maalumu. Vilevile, mbinu hii ilitumika
katika kukusanya data za upili kutoka katika machapisho mbalimbali yanayopatikana
katika maktaba za Chuo Kikuu Huria Cha Tanzani, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili na Makavazi ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.
3.4 Mbinu ya Uchambuzi wa Data
Uchambuzi wa data hufanywa ili kuweza kukamilisha malengo ya utafiti na
kuyawasilisha matokeo ya utafiti huo katika tasinifu (Inyani, 2002). Katika
kuchambua data za utafiti huu tulitumia mbinu ya mkabala wa kidhamira. Mkabala
huu unatoa maelekezo kwamba, katika kuchambua data za utafiti ni lazima hatua kuu
nne zifuatwe (John, 2007). Hatua ya kwanza ni kukusanya data za utafiti kwa mujibu
25
wa kanuni mbalimbali zinazoongoza ukusanyaji wa data katika utafiti. Hatua ya pili
ni kuzipanga data zilizokusanywa katika makundi kwa kadiri zinavyofanana na
kuwiana. Hatua ya tatu ni kuhusianisha data za utafiti na madhumuni ya utafiti ili
kuweza kuandaa mada kuu na ndogondogo ambazo husaidia kulifanya zoezi la
uchambuzi wa data kuwa rahisi. Hatua ya mwisho ni kuchambua data za utafiti kwa
namna ambayo inajibu maswali ya utafiti husika.
Uchambuzi wa data za utafiti huu ulifanywa kwa kuzingatia hatua zote nne. Katika
hatua ya kwanza tulizingatia kanuni zote za ukusanyaji wa data. Hii ndiyo hatua ya
kwanza katika ukusanyaji wa data za utafiti. Huwezi kuchambua data kama
hujakusanya, ndio maana hii ikawa ni hatua ya kwanza. Kanuni za ukusanyaji wa
data ni zile zote zilizoelezwa katika sura hii ya tatu. Hatua ya pili ilikuwa ni kupanga
data kulingana na vile zinavyohusiana na kufanana. Data zilizohusu nafasi ya
mwanamke katika mashairi teule ziliwekwa katika kundi moja kutoka kwa kila
mwandishi. Data zilizohusu matumizi ya lugha ya kisanaa katika kazi hizo za ushairi
nazo ziliwekwa katika kundi moja. Na kundi la mwisho ni lile lililohusu data za
falsafa za Shaaban Robert na Mathias Mnyampala juu ya nafasi ya mwanamke.
Hivyo basi katika kuchambua data za utafiti huu hatua zote nne tulizozieleza
zitazingatiwa.
Katika hatua ya tatu tuliazipanga data za waandishi wote wawili kwa kuzichanganya
zile zinazoeleza jambo moja na kisha kuunda mada kuu na mada ndogondogo
zilizotuwezesha kufanya uchambuzi. Mada zilizotengenezwa katika sura ya nne
zilizingatia madhumuni mahususi ya utafiti. Hatua ya mwisho ilikuwa ni kufanya
uchambuzi na kujadili data za utafiti na kuunda sura ya nne ya tasinifu hii.
26
3.5 Kuaminika kwa Data za Utafiti
Mtafiti ametumia mbinu zaidi ya moja katika kukusanya data za utafiti wake.
Mapungufu ya mbinu moja ya kukusanyia data yalitatuliwa kwa haraka na mbinu
nyingine na hivyo kuzifanya data zake kuaminika kwa wasomaji wake (Babbie,
1992). Mbinu ambazo tulizitumia katika kukusanya data ni mbinu za usaili, hojaji na
usomaji makini. Vilevile, mkabala wa kidhamira ndio ambao umetumika katika
kuchambua data za utafiti huu ambao bila shaka ni mkabala maarufu katika
uchambuzi wa kazi za kifasihi. Hivyo, data za utafiti huu zinaaminiwa na wasomaji
na watafiti wengine kwa sababu umefanywa kisayansi na kitaaluma.
3.6 Usahihi wa Data za Utafiti
Usahihi wa data za utafiti unatokana na kufuatwa kwa taratibu zote za utafiti husika
kama ilivyoainishwa katika pendekezo la utafiti (Cohen na Wenzake, 2000). Mtafiti
alihakikisha kwamba, mbinu za utafiti zilizoelezwa katika pendekezo la utafiti
zinafuatwa na kuzingatiwa kwa makini tangu mwanzo wa utafiti huu mpaka mwisho.
Mbinu hizi zilijadiliwa na kuimarishwa katika semina za uzamili na wataalamu
wabobezi katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili kwa nia ya kuzifanya kuwa sahihi na
imara zaidi.
3.7 Hitimisho
Mbinu za utafiti ndizo husaidia kupatikana kwa data zinazopelekea kukamilisha
madhumuni mahususi ya utafiti na hatimaye lengo kuu. Sura hii imewasilisha
vipengele vya eneo la utafiti, kikundi lengwa, sampuli ya utafiti na usampulishaji.
Vipengele vingine ni mbinu za kukusanya data za usaili, hojaji na usomaji makini,
27
mbinu ya mkabala wa kinadharia ya uchambuzi wa data, kuaminika kwa mbinu za
utafiti na usahihi wa data za utafiti.
28
SURA YA NNE
UWASILISHAJI, UCHAMBUZI NA MJADALA WA DATA ZA UTAFITI
4.0 Utangulizi
Hii ni sura mama katika utafiti wetu kutokana na umuhimu wake. Sura hii ndiyo
inayowasilisha mambo muhimu ambayo yanawezesha kutimizwa kwa malengo ya
utafiti. Young (1984) anaeleza kuwa, utafiti hauwezi kukamilika mpaka pale
matokeo ya utafiti huo yatakapowasilishwa kwa namna inayokubalika kitaaluma.
Hivyo, uwasilishaji, uchambuzi na mjadala wa data za utafiti huu umefanywa kwa
kurejelea madhumuni mahususi ambayo jumla yake ni matatu. Madhumuni mahususi
ya kwanza yalilenga katika kulinganisha na kulinganua usawiri wa nafasi ya
mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Madhumuni
mahususi ya pili yalihusu kulinganisha na kulinganua matumizi ya lugha
yanayotumiwa kumsawiri mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala. Madhumuni mahususi ya tatu na mwisho yalihusu kulinganisha na
kulinganua falsafa ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala katika kumsawiri
mwanamke. Baada ya utangulizi huu sasa tutazame madhumuni mahususi ya kwanza
yalivyotimizwa katika utafiti huu.
4.1 Usawiri wa Mwanamke katika Mashairi ya Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala
Usawiri wa mwanamke katika kazi za fasihi umefanywa na wahakiki pamoja na
watunzi mbalimbali wa kazi za fasihi za ushairi, riwaya, tamthilia, nyimbo, ngano na
michezo ya kuchekesha (Momanyi, 2001). Usawiri wa mwanamke katika kazi hizo
hujitokeza kwa namna anuai ambazo ni faafu au chanya na zisizofaafu au hasi.
29
Mathalani, mwanamke husawiriwa kama chombo cha kumstarehesha mwanaume,
kiumbe asiyekuwa mwaminifu, msaliti, Malaya na kiumbe tegemezi kwa
mwanaume. Pia mwanamke husawiriwa kama kiumbe mchapakazi, mwadilifu,
mama na mlezi wa familia, mzalishaji mali, na kiongozi wa familia (Ramadhani,
2013).
4.1.1 Mwanamke kama Chombo cha Starehe
Mwanamke kusawiriwa kama chombo cha starehe kwa mwanaume ni dhamira kuu
katika kazi nyingi za fasihi hasa kutokana na mfumo dume uliopo katika maisha
(Moore, 1998). Mfumo dume ni ile hali ya wanaume kuonekana kuwa ndio watu wa
tabaka la juu katika jamii na wanapaswa kupatiwa matunzo na heshima ya hali ya juu
kutoka kwa wanawake. Khatibu (1985) anatoa mfano wa Utenzi wa Mwanakupona
kama kielezeo sahihi cha maisha ya mwanamke mbele ya mumewe tangu
anapoolewa mpaka kufarikiana. Anasema, mwanamke anatakiwa ampokee mumewe
anapotoka kazini, amkaribishe ndani na kumketisha kitako, amkandekande na
kumchua ili kupunguza maumivu, amwandalie maji ya kukoga na kumkogesha na
kisha ampake mafuta na kumchana nywele miongoni mwa mengi ya hayo. Mathias
Mnyampala anamsawiri mwanamke kama chombo cha starehe kwa mwanaume
katika shairi la “Tamaa.” Anasema:
Na awe mzee sana, meno kinywani hanayo
Hawezi kitu tafuna, sababu ni kibogoyo
Lakini nyama kiona, humpaparika moyo
Tamaa ni wayo wayo, haina moyo kuchoka
Akiona msichana, moyo una wayo wayo
Pale wanapokutana, maneno huwa ya payo
Vipi wewe nguvu huna, ukatamanisha moyo
Tamaa ni wayo wayo, haina moyo kuchoka (Uk. 18).
30
Katika beti hizo mbili za shairi, kunaoneshwa kuwa mwanamke ni chombo cha
starehe kwa mwanaume hasa starehe za Kingono. Mtu mzima ambaye ameshazeeka
na kutokuwa na nguvu bado anaonekana kumtaka mwanamke na kustarehe naye
kingono. Kwa hakika, mwanaume huyo hawezi kufanya tendo hilo kwa ufanisi
unaotegemewa kwa sababu ya kukosa nguvu za kufanya hivyo. Swali tunalojiuliza ni
kuwa, kwa nini mwanaume huyo amtake mwanamke ambaye ni msichana mdogo
ambaye damu yake bado inachemka? Jibu la swali hili si jingine bali ni kuwa
mwanaume huyu anamuona mwanamke kama chombo cha starehe tena starehe kwa
mwanaume. Ni starehe kwa mwanaume kwa sababu, Mzee kama huyo hawezi
kumstarehesha mwanamke kutokana na kukosa nguvu za kufanya hivyo. Hivyo,
katika hali kama hii starehe inakuwa si ya watu wawili bali mtu mmoja tu. Mkazi
mmoja wa “Area C” katika Manispaa ya Dodoma alitueleza kuwa, katika jamii ya
Wagogo mwanaume ni mtu asiyetarajiwa kuzeeka katika masuala ya mapenzi na
ngono kama ilivyo kwa mwanamke. Mwanaume atastaafu kazi lakini si ngono. Ndio
maana karibu kila mzee wa Kigogo anakuwa na mahusiano ya kingono na binti asiye
wa makamo yake.
Mwanamke kama chombo cha starehe kwa mwanaume inabainika pia katika
mashairi ya Shaaban Robert. Anamchora mwanamke kama chombo cha starehe kwa
mwanaume kutokana na maumbile yake. Mwili wa mwanamke umeumbwa kwa
namna ambayo inamwezesha mwanaume kustarehe vizuri bila wasiwasi wowote.
Katika shairi la “Urafiki” lililopo ndani ya Pambo la Lugha anasema:
Umbo la Kupendeza, kama la malaika,
Sura ya kufurahisha, kama ile ya pepo,
Umbo la takaso, kama mbingu na mwezi,
Hulingani na mkadi, labda lulu bahari (Uk. 32).
31
Ubeti huu unamaanisha kuwa mwanamke ni chombo cha starehe kwa mwanaume
kutokana na kuwa na umbo zuri la kumburudisha na kumstarehesha mwanaume.
Mathalani, pale mshairi anaposema kuwa mwanamke ana umbo la kupendeza kama
la malaika, tunapata hisia kuwa umbo hilo ni la kumpendezesha na kumfurahisha
mwanaume. Hata msitari wa pili nao unaeleza jambo hilo hilo. Mwanamke
anasawiriwa kama chombo ambacho mwanaume akikitazama tu basi anapata starehe
ya ajabu. Hata katika jamii ya leo kila mwanaume hupenda kuoa mwanamke ambaye
ana umbo na sura ya kuvutia watu pale wamtazamapo. Mwanamke huyo anapopita
barabarani na kila mtu hasa wanaume kuanza kumshangaa basi mume au rafiki wa
mwanamke huyo hupata raha ya ajabu kabisa. Usaili tuliofanya na mkazi mmoja wa
eneo la Kange katika jiji la Tanga kuhusiana na mwanamke kuwa chombo cha
starehe kwa wanaume alikiri kuwa ni kitu cha kweli na kinatokea katika jamii.
Aalieleza kuwa katika Jiji la Tanga hivi sasa wapo wanawake ambao wanafanya kazi
ya kuuza miili yao na wakionekana katika barabara kadhaa usiku wakiwa nusu uchi.
Nusu uchi hiyo huwafanya wanaume kuwatamani na kwenda kustarehe nao.
Hali hii ndiyo inayotufanya tuamini kuwa mwanamke anatazamwa kama chombo
cha starehe kwa mwanaume. Imefika mahali katika jamii kuona baadhi ya wanaume
wakiwazuia wanawake zao kufanya kazi ngumu na kuwataka kukaa nyumbani
wakisaidiwa kazi na wafanyakazi wa ndani. Lengo hasa la kufanya hivyo, ni
kumvundika mwanamke ili aive vizuri na kuvutia kila siku. Katika usaili tulioufanya
na Mzee Sengo alieleza kuwa, mwanamke anapokuwa ameiva na kupendeza vizuri
humfanya mwanaume kuvutiwa kufanya ngono na mwanamke huyo. Msailiwa
mmoja katika barabara ya Kumi na Nne jijini Tanga alifafanua kuwa mwanamke
32
kuvundikwa aive ndio sahihi yake. Hata kule kutakiwa mwanamke kujigubika nguo
mwili mzima ni kuvifanya viungo vyake vipate jua na kupauka. Kila mara
vinapofunikwa ndivyo maungo ya mwanamke huiva na kupendeza. Hii inaonesha
kuwa ikiwa mwanamke hafuniki maungo yake hupauka na kutomvutia mwanaume
kingono. Kwa mantiki yote hiyo, inaonesha kuwa mwanamke ni chombo cha starehe
kwa mwanaume. Ramadhani (2013) anasema kuwa, nyimbo za Taarab ya Mipasho
za Mzee Yusuf Mzee kwa mfano, zinamchora mwanamke kama chombo cha
kumstarehesha mwanaume katika maisha yake yote.
Mjadala uliofanyika hapo juu unaonesha kuwa, Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala wanafanana katika kumsawiri mwanamke kama chombo cha
kumstarehesha mwanaume. Tafauti yao ni kuwa Mathias Mnyampala ameonesha
bayana kuwa mwanaume ni mtu anayemchukulia mwanamke kama chombo cha
starehe hasa za ngono. Hili limeonekana pale mzee mwanaume asiyekuwa na nguvu
kuonekana akiwa bado anatamani kuwa na mahusiano na msichana mdogo. Shaaban
Robert kwa upande wake amemsawiri mwanamke kama chombo cha starehe kwa
mwanaume kutokana na umbo na sura aliyonayo mwanamke. Hata hivyo, kwa
pamoja watunzi wote hawa wawili wanamsawiri mwanamke kama chombo cha
starehe kwa mwanaume.
4.1.2 Mwanamke ni Mpole, Mnyenyekevu kwa Mwanaume
Mwanamke ni kiumbe ambaye anatarajiwa kuwa ni mtu mpole na mnyenyekevu kwa
mwanaume katika maisha ya kila siku. Upole na unyenyekevu huo utaonekana katika
lugha anayotumia pale anapoongea na mwanaume. Mwanamke hategemewi
33
kubishana au kutoa lugha ya matusi kwa mumewe au mwanaume mwingine yoyote
katika jamii. Shaaban Robert anasema:
Mke akiwa mbishi, wa kushindana kusema
Na majivuno na mashi, na ulimi wake pima
Hata kama wala pishi, wali na kilo ya nyama
Utajiona aishi, duniani huna kima (uk. 22).
Mwanamke anapokuwa ni mbishi na tena mwenye majivuno huyafanya maisha ya
mwanaume kuwa magumu sana. Momanyi (2001) anaeleza kuwa ni jambo la ajabu
kuona mwanamke akitakiwa kutokuwa mbishi na mwenye majivuno na mwanaume
asionywe juu ya mambo hayo. Anaona kuwa sifa hizo si nzuri kwa wanajamii wote
na si kwa mwanamke pekee. Hata hivyo, ni mwanamke pekee anayetakwa kutokuwa
na tabia hizo ili awe mnyenyekevu kwa mwanaume. Mtunzi anaonesha kuwa kama
mwanamke atakuwa na tabia ya ubishi, majivuno na mwingi wa kusema sana basi
mumewe atakosa raha ya kuishi duniani. Ikatokea mwanaume huyo kuwa ni mtu
mwenye uwezo mkubwa wa kuweza kula kila anachotaka basi hawezi kunawiri
kutokana na majivuno, ubishi na maneno ya mke wake. Katika hojaji moja
kuliandikwa kwamba mwanaume yoyote anayetaka kuishi katika ndoa yake kwa
amani ni vema akahakikisha kuwa anapata mke ambaye si mbishani na mwenye
kusema sana.
Maelezo ya Shaaban Robert katika ubeti uliopo hapo juu yanaonesha kuwa
mwanamke ni kiumbe ambaye anaweza kuyafanya maisha ya mwanaume kuwa
mazuri au mabaya. Hili tunalipata pale anaposema kuwa, kama mwanamke akiwa ni
mtu wa madhila kwa mume basi mume huyo ataona kuwa hakuna haja ya kuishi tena
duniani. Kwa msingi huu, mwanamke anapaswa kuwa mnyenyekevu, mpole na mtii
34
kwa mumewe kwa kila jambo atakaloambiwa. Inapotokea mwanamke akawa
anapaza sauti yake juu ya ile ya mwanaume, anaweza kumfanya mwanaume huyo
kutokuwa na raha ya kuishi duniani na kumsababishia kupata maradhi kama yale ya
“Presha,” kupanda au kushuka kwa mapigo ya moyo kuliko ilivyo kawaida. Kwa
mfano, katika jamii za watu wa Libya mwanamke ni kiumbe ambaye anapaswa
kumheshimu sana mume wake na mara nyingi hatakiwi kusema neno au kupinga
jambo atakaloambiwa na mumewe mbele ya hadhara hata kama jambo hilo
hakubaliani nalo. Hii inatokana na mafunzo ya dini ya Kiislamu ambayo yanaelekeza
mwanamke kuwa hivyo.
Katika kitabu cha Ashiki Kitabu Hiki cha Shaaban Robert, pia kunaelezwa kuwa
mwanamke ni kiumbe asiyetarajiwa kutoa lugha ya matusi. Anasema:
Bi. Harusa na Bi. Chilli, wamejivunjia njia
Wameingia mahali, huchukiza kuwaona
Ya Rabi! Wape akili, hili wasitende tena
Matukano si amali, hasa kwa wasichana (uk. 35).
Shaaban Robert anaonesha kuwa mwanamke kuzungumza lugha ya matusi ni kitu
kibaya mno kupata kufanywa na mwanamke. Wataalamu wa masuala ya jinsia
wanayaona maelezo kama haya yanatolewa na Shaaban Robert kuwa ni gandamizi
na kumfanya mwanamke kujitoa kwa mwanaume (submissive to men) kwa kila
jambo (Macknnon, 1991). Suala la kutotumia lugha ya matusi ni jambo ambalo
linapaswa kutofanywa na watu wote katika jamii na si mwanamke peke yake. Hali
hii inatokana na mfumo dume ambao si kwamba unamfanya mwanamke kuwa ni
kiumbe mwema bali ni njia ya kumfanya asiwe na uwezo wa kuhoji au kuuliza
jambo lolote kwa mumewe kwa kuwa kwa kufanya hivyo ataonekana anamdharau
35
mumewe. Mkazi mmoja wa eneo la Chumbageni alitueleza kuwa, tunaona inatokea
katika jamii mtoto wa kike analazimishwa kuacha shule na kuolewa. Watoto wengi
wa kike hushindwa kupinga na kulazimika kuolewa utotoni na kuacha shule. Hii
inatokana na kunyamazishwa tangu wakiwa watoto wadogo kwa maelekezo kuwa
mwanamke hatakiwi kujibizana na wazazi wake na hasa baba.
Mathias Mnyampala kwa upande wake, naye pia anamsawiri mwanamke kama
kiumbe anayetakiwa kuwa mpole na mnyenyekevu kwa mwanaume. Mwanamke
hatarajiwi kujibizana na mumewe kwa jambo lolote lile na anapokatazwa jambo
lolote basi hutakiwa kuliacha mara moja. Kwa mfano katika ngonjera ya “Mke
kuomba Ruhusa kwa Mume,” anasema:
MKE
Nina jawabu adhimu, bwana nataka kwambia
Kuniradhi muadhamu, lazima kunisikia
Wala usinituhumu, kuwa bazazi wa njia
Nenda kwetu kutembea, niruhusu mume wangu
MUME
Jawabu yako naamu, Aziza sikuridhia
Walkalili fahamu, kwa ghadhabu kuniingia
Leo ni kutaramu, mengine wahitajia
Hwendi leo nakwambia, nikakaa peke yangu
MKE
Niruhusu tafadhali, jua nimeazimia
Nisirudie madhali, khasa nimekusudia
Bwana utanikatili, usiponikubalia
Nenda kwetu kutembea, niruhusu mume wangu
MUME
Ni bileshi kulalama, wala sitakusikia
Laaziza akirama, hayo uliyonambia
Na tena natuhuma, kuna dume langojea
Hwendi leo nakwambia, nikakaa peke yangu
36
MKE
Takwenda unifanyeni, lipi umekusudia?
Wewe ni mume gani, kama uliye nabiya?
Jama baba kanilani, kanipa chimvi balia
Nenda kwetu kutembea, niruhusu mume wangu (uk. 40-41).
Hapa tunaoneshwa majibizano baina ya mume na mke kuhusu mke kupatiwa ruhusa
ya kwenda nyumbani kwao kumtazama dada yake. Kwanza, tunaoneshwa kuwa
mwanamke hawezi kutoka nyumbani kwake kwenda mahali popote bila kutaka na
kupatiwa ruhusa na mumewe. Mkazi mmoja wa Majengo katika Manispaa ya
Dodoma anaeleza kuwa katika kabila lao la Wagogo ni wajibu wa mke kuomba
ruhusa kwa mumewe pale anapotaka kwenda nje na nyumba yake na kutokufanya
hivyo huhesabiwa kama ni utomvu wa nidhamu. Katika jambo lisilotegemewa mke
anaonekana kubishana na mumewe kwa kulazimisha ruhusa ambayo mumewe
amekataa kuitoa. Kwa kufanya hivyo, mwanamke huyu anamfanya mwanaume kuwa
na mashaka kuwa huenda akiitoa ruhusa hiyo mkewe atakwenda kufanya maovu
hasa yale ya zinaa.
Maelezo ya Shaaban Robert na yale ya Mathias Mnyampala yaliyotolewa hapo juu
yanaonesha kufanana pale ambapo wote wanaonesha kuwa mwanamke hapaswi hata
mara moja kubishana na mumewe juu ya jambo lolote kuhusu maisha yao ya ndoa.
Badala yake mwanamke anapaswa kuitikia na kukubaliana na kila kitu anachoelezwa
na mumewe. Tafauti ya msingi inayojitokeza kwa watunzi hawa wawili ni kuwa,
Shaaban Robert ameonesha kutoa maonyo zaidi kwa mke kutothubutu kujibizana na
mumewe hata siku moja. Analiona jambo hilo kuwa ni muongozo wa dini na
unapaswa kuheshimiwa na atakayekiuka anapingana na mafunzo ya dini. Hii ndiyo
hali iliyokuwepo wakati wa utunzi wa Shaaban Robert.
37
Kwa upande wake Mathias Mnyampala, anamuonesha mwanamke akibishana na
mumewe bila taabu yoyote. Hii inaonesha kuwa katika kipindi cha Mathias
Mnyampala tayari wanawake walishapiga hatua zaidi na kuanza kujibizana na
waume zao. Kwa wataalamu wa masuala ya jinsia kama Ngaiza (2002) na Moore
(1998) wanaiona hali hii kuwa ni hatua ya juu kabisa ya maendeleo kupata kufikiwa
na wanawake katika harakati zao za kujikomboa. Mwanamke kupaza sauti yake na
kupingana na baadhi ya mawazo ya wanaume ni ukombozi kutoka katika mfumo
dume. Hatua hii itawafanya wanawake kuwa huru na kuamua kufanya mambo yao
bila kuingiliwa na mtu yoyote. Si jambo la kubeza kwani hivi sasa wanawake
wamekuwa na nafasi kubwa hata ya ushiriki katika katika nafasi za uongozi na
kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao. Nafasi hii hawakuipata katika
kipindi cha Shaaban Robert.
Hata hivyo, matatizo ya kuvunjika kwa ndoa yamekuwa mengi kwa sasa
ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka hamsini iliyopita (Ramadhan, 2013). Hii
inaashiria kuwa kitendo cha wanawake kupata uhuru na nafasi kubwa ya kuweza
kujibizana na waume zao kunaongeza migogoro mingi baina yao ikilinganishwa na
kipindi ambacho wanawake hawakuwa na nafasi hiyo ya kujibizana na waume zao.
Mtoto wa Shaaban Robert anayejulikana kwa jina la Iqbali Shaaban Robert alitueleza
kuwa katika kipindi chote alichoshuhudia maisha ya baba na mama yake hakuwahi
kumuona mama yake akijibizana na baba yake. Anasema: “mama alikuwa mtu
mpole sana asiyependa kumuudhi baba kwa namna yoyote ile.” Hata hivyo, Moore
(1998) anaiona hatua hii ya wanawake kupata nafasi ya kujibizana na waume zao ni
hatua moja muhimu katika maendeleo ya masuala ya jinsia katika nchi za Afrika.
38
4.1.3 Mama na Malezi katika Jamii
Malezi ni hali ya wazazi au walezi kuwaongoza watoto wao katika misingi na
maadili ya jamii yao. Momanyi (2001) anasema kuwa, jukumu la malezi ni la wazazi
wawili (baba na mama) wa mtoto na si mmoja peke yake. Kutokana na mfumo dume
uliopo katika jamii mama ndiye aliyeachiwa jukumu la kulea watoto na baba
akishughulika na shughuli za uzalishaji mali na maendeleo kwa jumla. Hata hivyo,
katika hali ya kushangaza mtoto anapokuwa na tabia nzuri za kusifika katika jamii,
baba ndiye hupongezwa na kupatiwa sifa kwa malezi bora ya mtoto. Inapotokea
mtoto huyo akawa na tabia isiyo nzuri ya kuridhisha, lawama za malezi mabovu
humwangukia mama. Hii yote ni dalili ya mfumo dume ulioota mizizi katika jamii.
Mathias Mnyampala anatuonesha kuwa jukumu la malezi kwa watoto si la mama
pekee bali ni la wazazi wawili na jamii nzima kwa jumla. Tazama Shairi lake la
“Maonyo kwa Mtoto,” anasema:
Ungamonya huu mwiko, mwiko kuushika moto
Situme mkono wako, kushika kama kokoto
Katu hutashika lako, hadi apate majuto
Onyo lako kwa mtoto, kusikiwa ni katiti
Kusikiwa ni katiti, aendapo batobato
Na hasa ule wakati, wa uchanga na mtweto
Mwendo anenda matiti, hajui mema mapito
Onyo lako kwa mtoto, kusikiwa ni katiti
Mwambie sishike wembe, wembe una mkeketo
Kwa ulimi asilambe, tajikata zoloto
Ataona kama embe, hadi akatwe mkato
Onyo lako kwa mtoto, kusikiwa ni katiti (uk. 21).
Shairi hili linaanza kwa matumizi ya pili umoja kwa kumrejelea mtu fulani kuwa
ndiye mwenye jukumu la kumuonya mtoto. Mtu huyu anaweza kuwa baba au mama
kwa kuwa haikusemwa bayana ni nani hasa mwenye jukumu hilo. Kwa nukta hiyo,
tunaweza kusema kuwa Mathias Mnyampala anaona kuwa wazazi wote wanalo
39
jukumu la kulea watoto wao. Mtoto anapopata malezi ya baba na mama huimarika
zaidi kimadili na kimwenendo kuliko akilelewa na mzazi mmoja tu (Lyatuu, 2011).
Kutokana na ukweli huo baadhi ya wazazi hulazimika kuishi pamoja hata kama ndoa
yao ina misuguano mikubwa kwa nia ya kuwalea watoto wao wakiwa pamoja.
Hawako tayari kuvunja ndoa zao kwa sababu wanafahamu wakifanya hivyo
watasababisha watoto waishi bila ya malezi ya wawili hao.
Hata hivyo, tunaporejelea na kutazama shairi la “Maonyo kwa Mtoto,” liliandikwa
lini tunapata kubaini kuwa ni katika kipindi ambacho mwanamke ndiye
aliyebebeshwa jukumu kubwa la kulea watoto na familia nzima. Hivyo, matumizi ya
nafsi ya pili umoja katika msitari wa kwanza wa shairi, “Ungamwonya huu mwiko,
mwiko kuushika moto,” yanaashiria moja kwa moja kuwa aliyelengwa hapa ni
mwanamke. Mwanamke ndiye aliyedhaniwa kuwa na jukumu la kulea watoto kwa
sababu alikaa nao nyumbani siku nzima zaidi ya baba aliyeranda huku na huko
kutafuta riziki.
Kimsingi, malezo yetu tuliyoyatoa hapo awali yanaonesha kuwa katika shairi la
“Maonyo kwa Mtoto,” mama na baba wote wanajukumu kubwa la kuwapatia watoto
wao malezi bora. Kwa kutazama katika kipindi ambacho shairi hilo liliandikwa
tukabaini kuwa anayelengwa katika malezi ya mtoto hapa ni mama zaidi kuliko baba.
Upo usemi wa Kiswahili usemao, “Ukimwelimisha mama, umeelimisha jamii
nzima.” Usemi huu unatokana na hali halisi kuwa mama ndiye anayelea watoto
nyumbani na kwa hiyo kutumia muda mwingi katika maisha yake akiwa na watoto.
Kama kila mama akipata elimu juu ya malezi ya mtoto, itakuwa kazi rahisi kwake
40
kuwapatia watoto wake malezi bora. Hali ikiwa hivyo kwa akina mama wote ndivyo
jamii nzima itakavyoelimika kutokana na mafunzo na maonyo ya mama.
Shaaban Robert kwa upande wake naye amezungumzia dhamira hii kwa kuonesha
kuwa mwanamke wa zamani alikuwa na jukumu la kulea watoto na tena si mtoto
mmoja bali watoto wengi. Katika Insha na Mashairi (1971) Anasema:
Kinyume cha Mwanamke wa zamani. Aliyekuwa
mtumwa na mtumishi wa kazi ngumu kama kibarua,
Mwanamke wa zamani alionekana mchana na usiku
nyumbani na jikoni, kuzaa na kulea umati wa watoto,
Na mwenye lazima ya kufanya kazi ya kuangalia faraja
za bwana: Mume wake.
Maelezo haya ni ushahidi tosha kuwa mwanamke alitazamwa kuwa ndiye mtu
mwenye jukumu la kulea watoto na hakupatiwa msaada wowote katika hilo kutoka
kwa mumewe na wanajamii kwa jumla. Kazi hii kwa hakika ni ngumu na haikuwa
kazi pekee kwa mwanamke huyu. Wakati akilea watoto alipaswa pia kupika chakula,
kufua nguo, kusafisha vyombo, kutafuta kuni na kwa ujumla kuhakikisha kila kitu
katika familia kinakwenda sawasawa. Jambo kubwa na muhimu ambalo anatakiwa
kufanya ni kuhakikisha kuwa mumewe anaishi maisha mazuri kabisa. Maelezo ya
Shaaban Robert yanaonesha kuwa mwanamke anaelemewa sana na mzigo mkubwa
wa kulea watoto. Kwa hili anaonesha kuwa na huruma kubwa kwa mwanamke.
Kwa maneno ya Shaaban Robert jukumu hili kubwa la malezi lilikuwa kwa
mwanamke wa zamani. Maelezo yake tunakubaliana nayo kwa kuwa ni kweli kabisa
mwanamke wa zamani alikuwa na jukumu kubwa la kulea watoto. Pamoja na ukweli
huu, bado hata mwanamke wa siku hizi analo jukumu kubwa la malezi kwa watoto.
Kwa mfano, mwanamke wa kijijini amezongwa na majukumu mengi katika familiya
41
yake na kubwa likiwa ni kulea watoto. Lyatuu (2011) anaeleza kuwa katika jamii ya
watu wa vijijini, wengi wa wanaume wamesahau kabisa jukumu la kulea watoto na
kuwaachia wanawake peke yao. Kila kitu mtoto atakachomuuliza baba yake,
hujibiwa kuwa amuulize au amweleze mama yake na siyo yeye (baba).
4.1.4 Mwanamke na Suala la Uaminifu
Uaminifu ni kitu muhimu sana katika mahusiano ya mume na mke katika maisha yao
ya kila siku. Uaminifu baina ya wawili hao ndio unaodumisha na kuendeleza
mahusiano yao na kuyafanya kuwa mapya kila uchao (Ramadhani, 2013). Katika hali
ya kawaida, uaminifu unapaswa kuwa watu wote katika jamii na si mtu mmoja peke
yake. Hata hivyo, katika maisha ya siku hizi mwanamke anaonekana kulaumiwa kwa
kukosa uaminifu na kusababisha matatizo makubwa katika jamii (Khalifa, 2013).
Mwanamke anaonekana kuwa ni kiumbe laghai na mwenye kudanganyika kirahisi
kwa ghilba na vitu vidogo kama vile fedha, mavazi, chakula na vitu vya aina hiyo na
kumsaliti mwenzi wake. Shaaban Robert anaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe
asiyemwaminifu na asiye aminika. Shairi “Kuoa,” lililopo katika Pambo la Lugha
linasema:
Kuoa mke wa haya, kukutazama hawezi
Kama kweli yatakiwa, ni mke wa fumanizi
Amwitaye humwendea, huwa hana kizuizi
Na jambo hili li wazi, ya fahamu yasemwayo (uk. 18).
Hii inaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe asiye aminika hata kama akiwa na haya
ya kutoweza kumtazama mtu usoni. Anaweza kuwa na haya kumtazama mumewe
usoni lakini asiwe na haya ya kujizuia na uzinzi. Haya alizokuwa nazo mwanamke
huyu ni za kinafiki tu na hazina ukweli wowote. Kwa nini haya alizonazo
42
mwanamke katika kumtazama mumewe zinapaswa kuwa hivyo hivyo katika mambo
mengine ndiyo kuaminika kwa mwanamke huyo? Lakini anapokuwa na haya ya
kumtazama mumewe usoni tu hana haya ya kuepuka zinaa na udanganyifu wa
wanaume, mwanamke anakuwa ni kiumbe asiyeaminika.
Vile vile, hii inaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe ambaye hana uwezo wa kukataa
maelezo yoyote anayoambiwa na mwanaume hata kama anayoambiwa yanaathiri
maisha na ndoa yake. Mwanamke anafananishwa na mtoto mdogo. Anasema,
“Amwitae huenda, huwa hana kizuizi.” Hii inamchora mwanamke kama kiumbe
asiye na uwezo wa kutafakari jambo lolote analoambiwa na mtu yeyote bila ya
kufikiria athari za hayo anayoambiwa. Mkazi mmoja wa barabara ya nane katika jiji
la Tanga alieleza kuwa, mwanamke wa siku hizi ni mjanja asiyedanganyika kwa
urahisi kama ilivyokuwa zamani. Habari ya kumdanganya mwanamke kwa Chips
Kuku sasa imekwisha na wengi wa wanawake wanajitambua na wanajiheshimu.
Haya ni mawazo ya watu wenye mtazamo wa mfumo dume ambao humuona
mwanaume kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kutafakari mambo kabla ya
kufanya maamuzi. Kinyume chake, mwanamke hufanya maamuzi bila ya kufikiri na
hujutia maamuzi yake baadae (Lyatuu, 2011). Huu ni ugandamizaji na udhalilishaji
wa jinsia ya kike kwa kuwa si kweli kwamba wanawake wote hufanya maamuzi bila
ya kufikiria. Wapo hata wanaume ambao wakati mwingine hujikuta wamefanya
maamuzi bila ya kutafakari na kujutia baadae. Kufanya maamuzi yoyote yale bila ya
kufikiria ni udhaifu wa kibinadamu na si wa mwanamke peke yake. Hivyo, si
sawasawa kumlaumu mwanamke kwa makosa ambayo yanaweza kufanywa na
mwanaume pia.
43
Mwanamke kiumbe ni asiye mwaminifu na asiyeaminika ni dhamira
inayowasilishwa katika mashairi ya Mnyampala ya Waadhi wa Ushairi na Ngonjera
za Ukuta. Katika shairi la “Mke Kuomba ruhusa kwa Mumewe,” anasema:
MKE
Nina jawabu adhimu, bwana nataka kwambia
Kuniradhi muadhamu, lazima kunisikia
Wala usinituhumu, kuwa bazazi wa njia
Nenda kwetu kutembea, niruhusu mume wangu
MUME
Jawabu yako naamu, Aziza sikuridhia
Walkalili fahamu, kwa ghadhabu kuniingia
Leo ni kutaramu, mengine wahitajia
Hwendi leo nakwambia, nikakaa peke yangu (uk. 40).
Inaonekana mwanamke kunyimwa ruhusa ya kwenda kumtazama dada yake kwa
kuhofiwa kwenda katika mambo ya ubazazi. Mwanamke mwenyewe tayari
amekwishaweka shaka ya kukubaliwa ruhusa anayotaka ndiyo maana akatanguliza
samahani kuwa yeye haendi katika mambo ya ubazazi bali anakwenda kumuona
dada yake. Hii inaonesha kuwa, wanawake wamekwisha athiriwa na mfumo dume
kiasi cha kujiona ni wakosaji kila mara. Pia, wanawake wamekwishaifahamu vizuri
akili ya wanaume kuwa daima huwadhania kuwa ni watu waovu wasioaminika hata
kidogo.
Shao (2004) anaona kuwa, wanawake ni watu ambao wameathiriwa sana na mfumo
dume kiasi cha wao wenyewe kuendeleza unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia
dhidi yao wenyewe. Hii tunaiona pale mwanamke anapoomba ruhusa ya kutoka
nyumbani kwa kujitetea kuwa haendi kushiriki katika mambo maovu. Kwa nini
mwanamke huyo asiombe ruhusa bila ya kujitetea kuwa haendei mambo maovu?
Ikiwa ataomba ruhusa bila kujitetea kuwa haendi kushiriki uovu, atapatiwa ruhusa
44
hiyo? Majibu ya maswali haya yanatupeleka katika ukweli kuwa mfumo dume
umemfanya mwanamke kuonekana kama kiumbe asiyeaminika hata kidogo kwa
mumewe na hata jamii kwa jumla. Tazama majibu ya mume kwa mkewe katika ubeti
ufuatao:
MUME
Ni bileshi kulalama, wala sitakusikia
Laaziza akirama, hayo uliyonambia
Na tena natuhuma, kuna dume langojea
Hwendi leo nakwambia, nikakaa peke yangu (uk. 41).
Mume ameamua kudhihirisha bayana kwa nini hataki kumpatia mkewe ruhusa ya
kwenda kwao kutembea kwa msingi kuwa mkewe huyo ana miadi ya kukutana na
mwanaume mwingine. Katika msitari wa tatu wa ubeti hapo juu maneno
yaliyokozwa wino yanaashiria kuwa mwanamke huyo anakwenda kufanya zinaa na
mwanaume asiye mumewe. Hali kama hii inajitokeza katika jamii nyingi duniani na
si ya Waswahili peke yake. Kwa mfano, Katika nchi za Kiarabu, mwanamke
hatakiwi kwenda mahali popote pale peke yake bila kuongozana na mumewe au
ndugu yake wa kiume. Sababu kuu ya kufanya hivyo ni kumlinda mwanamke huyo
asije akaingia katika maasi na wanaume wa barabarani. Pili, mwanamke ni kiumbe
dhaifu ambaye hawezi kufanya maamuzi ya haraka akiwa peke yake na hivyo ni
lazima awe na muongozo wa mwanaume. Tazama dondoo lifuatalo ambalo ni
maelezo binafsi ya mtafiti:
Wanafunzi wa kike kutoka katika nchi yangu ya Libya
ambao wapo hapa Tanzania na kwingineko duniani
wamefuatana na wanaume ambao ni ndugu zao wa
karibu. Ndugu hao wanaweza kuwa ni kaka, baba,
mjomba, babu, mtoto wa kiume wa kaka au dada.
Ndugu huyo huandamana na mwanafunzi wa kike
katika shughuli zote za masomo mpaka wanapomaliza.
Ndugu wanaofuatana na wanafunzi hao wa kike
45
hulipiwa gharama zote za maisha na serikali ya Libya
katika kipindi chote hicho. Waarabu ni watu wenye
wivu sana na wanawake na huamini kwamba, iwapo
mwanamke ataachwa peke yake anaweza kuchukuliwa
na wanaume wengine huko katika masomo yao. Pia,
serikali ya Libya imepiga marufuku raia wake kuoa au
kuolewa na mtu asiyekuwa Mlibya au Mwarabu kutoka
katika mataifa ya Kiarabu yaliyoteuliwa.
Hii inaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe anayehitaji uongozi na ulinzi kutoka kwa
mwanaume katika kila jambo analolifanya. Mwanamke peke yake hawezi kufanya
mambo yakawa mazuri akiwa peke yake kwa kuwa hana uwezo huo. Mawazo haya
si lolote wala chochote kwa wataalamu wa masuala ya jinsia kwani katika jamii
wapo wanawake ambao hujiongoza wenyewe na hata kuongoza familia zao kwa
manufaa makubwa. Koda (2000) anayaona mawazo kama haya kuwa ni njia ya
kuimarisha makucha ya mfumo dume katika jamii.
4.1.5 Suala la Uasherati na Umalaya katika jamii
Uasherati na umalaya ni maneno yanatumika kumaanisha utendwaji wa tendo la
ndoa pamoja na mambo yanayoambatana nayo pasipo halali ya kufanywa kwayo.
Inapotokea mwanaume na mwanamke ambao si wanandoa kufanya ngono na
yanayohusiana nayo huelezwa kuwa watu hawa ni Malaya au Asherati. Njogu na
Wafula (2007) katika maelezo yao juu ya nadharia ya Ufeministi wanaeleza kuwa
umalaya ni dhana anayopambwa nayo sana mwanamke katika jamii kuliko
mwanaume hali ya kuwa wote wawili wanashiriki katika kadhia hiyo ya umalaya.
Kutokana na mfumo dume ulioenea katika jamii wanawake wametupiwa kila jambo
baya kuwa ni la kwao. Mathias Mnyampala anabainisha kuwa mwanaume na
mwanamke ambao wanashiriki katika ngono isiyokuwa halali wote ni Malaya na
asherati. Tazama beti zifuatazo kutoka shairi la “Malaya” katika Waadhi wa Ushairi:
46
Japo mtu wa silaha, machoni ukimuona
Amefunga na nikaha, yeye na mwana Amina
Ni mtu mwenye karaha, si mtu mwenye maana
Asherati hana haya, angawa mtu mkubwa
Na haoni mwanamke, po pote wakikutana
Lazima amtake, maneno yenyewe zina
Huzitoa pesa zake, mapenzi yapate fana
Asherati hana haya, angawa mtu mkubwa
Japo ni mke wa mtu, rafiki wanopendana
Kutongoza huthubutu, si kitu wakikosana
Huja uharibu utu, wanapofumaniana
Asherati hana haya, angawa mtu mkubwa (uk. 73).
Katika beti hizi tatu mtunzi anaonesha kuwa mwanaume ambaye tayari ana mkewe
na mwanamke ambaye tayari ana mumewe nyumbani wanashiriki katika kitendo cha
ngono kinyume na taratibu na kanuni za jamii. Kwa kauli hiyo, inaonekana kuwa
Malaya anaweza kuwa mwanaume na mwanamke pia. Si vema kumlaumu
mwanamke pekee kuwa ndiye Malaya na mwanaume akaachwa tu na wakati
mwingine kupewa sifa nzuri kuwa yeye ni bingwa wa kufanya zinaa na wake za
watu.
Katika ubeti wa tatu hapo juu mwanamke anasawiriwa kuwa ni kiumbe mpenda
fedha na kutokana na hilo hughilibiwa na wanaume na kufanya nao zinaa hata kama
tayari yeye ni mke wa mtu. Suala la wanawake kupenda fedha zisizopatikana kihalali
ni jambo baya ambalo huwasababishia wanawake wengi kuingia katika mkondo wa
maovu yenye madhara si kwao tu bali kwa wenzi wao, familia zao na jamii zao. Hata
hivyo, anayetoa fedha hapa ni mwanaume kumpatia mwanamke ambaye ni mke wa
mtu ili kumshawishi washiriki ngono. Mhojiwa mmoja wa eneo la Vibambani huko
Tanga aliandika katika hojaji aliyopatiwa akihoji, kwa nini mwanamke ndiye
47
alaumiwe ati anapenda fedha kama kila mwanaume angelitunza fedha zake ni
mwanamke yupi angelimlazimisha kumpatia. Kwa bahati nzuri katika jamii ya
Watanzania na hata katika mataifa ya Kiarabu kama Libya, mwanaume ndiye
mtongozaji huku mwanamke akiwa msikilizaji tu. Hakuna sababu yoyote ya
mwanaume kutoa fedha kama anajiamini kuwa na ujuzi wa kutongoza. Kumbe
mwanaume kutoa fedha kwa mwanamke kama kigezo cha kumpata mwanamke huyo
ni udhaifu wa mwanaume kushindwa kutongoza kwa maneno.
4.2 Matumizi ya lugha ya Kisanaa katika Mashairi ya Washairi Teule
Matumizi ya lugha ni mojawapo kati ya mbinu nyingi za kisanaa zinazotumiwa na
watunzi wa mashairi katika kusawiri dhamira katika kazi zao. Senkoro (1988)
anaeleza kuwa matumizi ya lugha katika kazi ya ushairi ndiyo yanayowafanya watu
kupenda au kutopenda kazi za mwandishi yeyote wa ushairi wa Kiswahili. Matumizi
hayo ya lugha yapo ya aina kwa aina na huchaguliwa na mtunzi kulingana na ustadi
alionao katika utunzi wa mashairi (Senkoro, 1988). Mtunzi bora wa mashairi ya
Kiswahili husifika kwa ustadi wake katika uteuzi wa maneno ambayo yanalandana
vizuri kwa vina na mizani (Masamba, 1983). Bila shaka huu ni mtazamo wa utunzi
wa mashairi kwa mujibu wa wanamapokeo. Haijuzu, kwani Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala ambao tunatafiti mashairi yao wote ni washairi wa Kimapokeo
kwa maana ya kutunga mashairi yao kwa kuzingatia urari wa vina na mizani.
Pia, matumizi ya lugha ya kitamathali ndiyo hutawala kwa kiasi kikubwa katika
lugha ya mashairi. Tamathali za semi zina sifa ya kufumba mambo na kueleza
mambo mengi kwa muhtasari. Ushairi nao ni utanzu wa fasihi ambao hueleza
mambo mengi lakini kwa kutumia lugha ya mkato, mnato na fumbizi kwa wasomaji
48
wake. Hivyo, mtu anapozungumza juu ya matumizi ya lugha ya kitamathali katika
mashairi hana tafauti na mtu anayezungumzia umuhimu wa maji ya bahari, mto au
bwawa kwa samaki.
Washairi Shaaban Robert na Mathias Mnyampala ni miongoni mwa washairi nguli
wa mashairi ya Kiswahili ambao wanaheshimika sana kitaifa na kimataifa. Washairi
hawa wanatumia lugha ya kitamathali katika mashairi yao kwa nia ya kufumba
dhamira zenye maadili kuntu kwa jamii yao. Tamathali zinazotumiwa na watunzi
hawa wawili ni takriri, tashibiha, taswira, sitiari, jazanda, kejeli, utani, majazi na
nyinginezo.
4.2.1 Matumizi ya Takriri katika Mashairi ya Washairi teule
Njogu na Chimerah (2014) wanafasili takriri kuwa ni tamathali ya usemi ambayo
hutumiwa na watunzi wa mashairi kwa kurudirudia baadhi ya silabi, maneno na
sentensi katika tungo zao ili kutoa msisitizo wa jambo ambalo wanadhani ni muhimu
kwa wasomaji kulinasa mara moja. Matumizi ya takriri huifanya hadhira ya kazi ya
ushairi kuwa makini na zingativu katika usomaji wao kutokana na nguvu ya takriri
katika moyo wa msomaji. Senkoro (1988) anaiona takriri kama chombo
kinachotumika katika kumkumbusha msomaji kile kilichosemwa katika ubeti
uliotangulia na kuhusianisha na anachosoma katika ubeti ungalipo. Hii ni sawasawa
na kusema kuwa matumizi ya takriri katika ushairi husaidia kuunganisha mawazo na
kuleta mtiririko sahali kwa msomaji wa mashairi. Mathias Mnyampala katika shairi
la “Mama,” lililopo katika Waadhi wa Ushairi, ametumia takriri za aina tatu zote
kwa pamoja zikizungumzia nafasi ya mwanamke. Tazama mfano ufuatao:
49
Kama walipa fadhila, ya kushukuria wema
Na akubariki Mola, akujalie rehema
Jambo lenye na Jamala, mshukuru sana mama
Fadhila umpe mama, na Mola takubariki
Na Mungu takubariki, rehema utaichuma
Taichuma kwa Maliki, Muumba wetu Karima
Mama yu pekee baki, radhi ya mama ghanima
Fadhila umpe mama, na Mola takubariki
Fadhila mama umpe, na nyingi mno heshima
Yakupasa umlipe, pamoja nyingi huruma
Mwiko sana simtupe, ijapo ana kilema
Fadhila umpe mama, na Mola takubariki
Kama wataka mwamuzi, wa kuondoa zahama
Ya kuondoa ulozi, wenye ndweo na hasuma
Ni mama ndiye hirizi, wa kuondoa tuhuma
Fadhila umpe mama, na Mola takubariki
Beti hizo nne zinathibitisha matumizi ya takriri za aina tatu ambazo ni takriri silabi,
takriri neno na takriri sentensi. Takriri silabi ni vina kati ambavyo vimekuwa
vikibadilika kutoka ubeti mmoja na mwingine. Vina mwisho ni “ma” na vinafanana
katika beti zote za shairi hapo juu. Takriri neno inajitokeza kupitia neno “mama”
ambalo limerudiwa katika kila ubeti na zaidi ya mara moja katika baadhi ya beti.
Neno hilo limerudiwa mara 8 katika shairi zima. Marudiorudio haya yanaifanya
hadhira kuuona uzito wa mama katika jamii na hivyo kumpatia heshima anayostahili.
Mama ndiye anayelea watoto kwa muda mrefu kuliko baba kwani mama huanza kazi
hiyo ya ulezi tangu angali mjamzito na kuendelea na kazi hiyo ya ulezi kwa muda
mrefu baada ya kuzaliwa mtoto huyo. Ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa
analipa fadhila kwa mama yake kutokana na mengi aliyofanyiwa na mama yake.
Takriri sentensi ndiyo inayokazia wazo hili, “fadhila umpe mama, na Mola
takubariki.”
50
Shaaban Robert pia anayo matumizi ya takriri kama hizo katika mashairi yake. Kwa
mfano katika Shairi la “Fedha,” lililopo katika Ashiki Kitabu Hiki, anasema:
Fedha imevunja nguu,
Milima ikatambaa,
Fedha ni kitu Kikuu,
Aliyenayo shujaa,
Hutiiwa na wajuu,
Wa chini wakaridhia.
Mtu aliye na fedha,
Japo duni ni kubeli,
Asemalo lina ladha,
Neno lake Ikibali,
Hazukiwi na bugudha,
Uongowe huwa kweli (uk. 8-9).
Neno “fedha,” katika beti hizi mbili limerudiwa mara tatu zaidi kuliko maneno
mengine yaliyopo katika beti hizo. Kurudiwarudiwa kwa neno hilo kunatoa msisitizo
kwamba fedha huweza kutumika kufanya jambo lolote zuri na baya katika jamii.
Kwa mfano, fedha huweza kutenganisha au kuvunja ndoa ya mtu. Kwa mfano,
hutokea katika jamii mke kumuacha mumewe na kwenda kuolewa na mwanaume
mwingine kwa sababu ana fedha na yule mume wa kwanza ni masikini. Vile vile,
vitendo vya umalaya na uasherati vinavyofanyika katika jamii na lawama kubwa
ikielekezwa kwa mwanamke ni ishara tosha ya kwamba fedha ndiyo zinazosababisha
mambo haya kutokea katika jamii.
Washairi wote wawili wana matumizi ya takriri katika mashairi yao. Takriri
zilizotumika zina nia ya kusisitiza juu ya mambo ya msingi ambayo mtunzi anataka
hadhira yake iyapate. Mathias Mnyampala anaonekana kuwa na matumizi ya takriri
neno mara nyingi zaidi kuliko Shaaban Robert. Kwa mfano, Mathias Mnyampala
amerudia takriri neno “mama” mara nane katika shairi la “Mama,” wakati Shaaban
51
Robert amerudia neno “fedha,” katika shairi la “Fedha” mara tatu tu. Hii ni kwa
mujibu wa mifano iliyopo hapo juu. Pia, Mathias Mnyampala amekuwa na matumizi
ya takriri sentensi katika shairi la “Mama” tulilolitolea mfano hapo juu hali ya kuwa
Shaaban Robert hakuonesha matumizi hayo katika shairi la “Fedha” tulilolitolea
mfano hapo juu. Hata hivyo, wote kwa pamoja wameonesha kuwa matumizi ya
takriri za aina kwa aina ni muhimu katika kuwasilisha dhamira kwa hadhira ya
mashairi.
4.2.2 Matumizi ya Tashibiha katika Mashairi ya Washairi Teule
Tashibiha ni tamathali za usemi ambazo hutumika kulinganisha vitu vyenye sifa na
tabia tofauti kuwa ni kitu kimoja chenye kufanana bila ya kutofautiana (Njogu na
Chimerah, 1999). Tashibiha hutumia maneno ya mlinganisho kama; sawasawa na,
mithili ya, kama, anafanana na, na mfano wa. Matumizi ya maneno haya ya
ulinganisho hutupatia tashibiha ambazo huiwezesha hadhira kupata dhamira zilizomo
katika shairi hilo. Shaaban Robert katika shairi “kuoa,” lililopo katika Ashiki Kitabu
Hiki anasema:
Kuoa mke si kufu,
Atakuliza machozi,
Kwa mambo yake dhaifu,
Ukonde ubaki ngozi,
Huwezi kumsarifu,
Cheo chako hakiwazi,
Kwake kama upuuzi,
Yafahamu yasemwayo (uk. 6).
Hapa tunaoneshwa matumizi ya tashibiha “Ukonde ubaki ngozi,” yakifafanua vizuri
dhamira ya ya mateso ya mwanaume kutoka kwa mkewe. Shaaban Robert anafunza
kuwa kuoa si jambo la kupapiapapia na kukimbilia kwani madhara yatokanayo na
52
matatizo ya ndoa ni makubwa. Kabla ya kuoa mtu anatakiwa kufanya utafiti wa kina
juu ya mchumba wake kwa nia ya kujiridhisha kuwa atakuwa mwenza sahihi kwake.
Pasipo kufanya utafiti kabla ya kuoa na kuamua kuoa mwanamke yeyote tu kunaleta
matatizo ya mwanaume kukonda na kubakia kama ngozi. Hii ina maana kwamba
kutokana na kero za mke asiyekuwa mwema kwa mumewe, humfanya mumewe
huyo kuwa na hali mbaya kiafya kutokana na mawazo. Hii inawataka watu wote
kuwa makini katika kutafuta mwenzi wa kumuoa au kuolewa.
Mjadala katika aya ya hapo juu unaonesha kuwa mwanamke ndiye mtu anayeweza
kusababisha matatizo kwa mume na katika ndoa kwa jumla. Huu ndio mtazamo wa
watu wengi katika jamii kiasi hata cha kuwakataza watoto wao wa kiume wasioe
binti kutoka nyumba fulani kwa madai kuwa watoto wa nyumba hiyo ni watovu wa
adabu. Hili kwa hakika ni eneo mojawapo kati ya maeneo makubwa ya ugandamizaji
wa jinsia ya kike (Khalifa, 2012). Si kweli kuwa wanawake ndiyo watu wabaya
wasababishao matatizo katika familia na kuwakondesha waume zao. Ni baadhi tu ya
wanawake ndiyo huwa na tabia mbaya katika ndoa kama ilivyo pia kwa baadhi ya
wanaume. Katika ngonjera ya “Maana yake nini Nyama ya Ulimi,” Mathias
Mnyampala anasema:
JAWABU
Ni maneno ya ufumbe, yatakiwa kufumbua
Ya usemi wa vijembe, ukweliwe hupindua
Ni maneno ya ubembe, mjinga kumzindua
Maneno ya kuzindua, ndiyo nyama ya ulimi
Kiutumia vizuri, mambo takuwa fahua
Ulimi taleta heri, kwa mapenzi ya murua
Ulimi kileta shari, ndiyo shari tavumbua
Maneno ya kuzindua ndiyo nyama ya ulimi
53
Ulimi waponza Kichwa, kwa maneno kufyatua
Halijazama likachwa, huja kuzua belua
Aso jeuri huachwa, hupendwa kama halua
Maneno ya kuzindua, ndiyo nyama ya ulimi
Mtu kumridhi mke, mpe neno la murua
Japo awe na makeke, wazimu utapungua
Neno jema utamke, mwelewa hupata afua
Maneno ya kuzindua, ndiyo nyama ya ulimi (uk. 85).
Sehemu ya ngonjera hii ya Mathias Mnyampala ina matumizi ya tashibiha
hupendwa kama halua. Hii ina maana kuwa mwanamke ambaye si msemaji sana
wa maneno hupendwa na mumewe pasina kifani. Mke wa mtu hapaswi kuwa mtu wa
vijembe kwa mumewe na kwa watu baki katika jamii. Mwanamke anapaswa kuwa
mtu mpole na heshima asiye na sauti ya juu kwa mumewe. Hii itamfanya mke huyo
apendwe na mumewe kwa upendo usio kifani kama vile watu wanavyopenda halua.
Halua ni aina ya kitafunwa kitamu mno kinachotengenezwa kwa nafaka, viungo,
sukari na mafuta.
Katika ubeti wa nne kunaoneshwa kuwa, mwanaume naye anapaswa kuwa mtuvu wa
ulimi kwa mkewe. Mwanaume hapaswi kuwa na lugha ya masimango na kero kwa
mkewe kwani atasababisha kuchukiwa na mkewe. Kumbe si mwanamke peke yake
ambaye anatakiwa kuwa na maneno laini na ukarimu kwa mumewe hata mwanaume
pia anapaswa kuwa hivyo hivyo kwa mkewe. Wana nadharia ya Ufeministi kama
Moore (1998) wanaiona hali kama hii kuwa ni hatua ya juu ya maendeleo kufikiwa
katika harakati za ukombozi wa wanawake kutoka katika makucha ya mfumo dume.
Mfumo dume uliwafanya wanawake kuwa chini na kujinyenyekeza kwa waume zao
huku wanaume wakionekana kuwa katika tabaka la juu la kuwanyanyasa wanawake.
54
4.2.3 Matumizi ya Taswira katika Mashairi ya Washairi Teule
Taswira ni picha anayoipata msomaji wa ushairi baada ya kusoma shairi ambalo
limepambwa kwa lugha ya mafumbo. Senkoro (1988) anaeleza kuwa taswira ni
maneno ambayo yalivyopangwa katika shairi huweza kuchora picha kamili ya kitu,
hali, wazo, dhana au mawazo mengine. Tunajifunza kuwa taswira hujitokeza akilini
kwa msomaji wa shairi kwa sababu ni katika mashairi ndiyo kuna matumizi
makubwa ya taswira kuliko ilivyo katika kazi nyingine za fasihi. Shaaban Robert
katika shairi la “Sijui,” ndani ya diwani ya Ashiki Kitabu Hiki anaeleza:
Mwanamume kinyozi,
Dada mimi simwezi,
Heri nipande ngazi,
Nende japo kwa goa.
Sinifanyie kelele,
Maneno mapesa mbele,
Nikanunue mchele,
Huko nitakofika (uk. 12).
Taswira ya haraka haraka inayopatikana katika shairi hili ni kuwa mwanamke
anaonekana kuwa ni kiumbe anayependa fedha zaidi kuliko kitu kingine katika
maisha. Kutokana na kupenda kwake fedha amekuwa ni mtu asiyekuwa na mapenzi
ya dhati kwa mumewe. Mwanamke wa aina hii yupo tayari kumwacha au kumsaliti
mumewe kwa kufanya ngono na wanaume wengine wenye fedha.
Katika shairi la “Sinyamaziki” katika kitabu cha Mwafrika Aimba cha Shaaban
Robert tunapewa taswira nyingine inayohusu nafasi ya mwanamke kwa mumewe.
Tazama mfamo:
Sana nilimnyenyekea,
Bali sikupata wema,
Mali imenipotea,
55
Ndipo nikarudu nyuma,
Na sasa najijutia,
Nikikumbuka gharama,
Sinyamaziki kusema-
Hukumbuka mali yangu.
Huba ilinikithiri,
Moyo na mwili mzima,
Miliki nikahasiri,
Kuuza chini ya kima,
Fedha nimpe mzuri,
Anisabilie wema,
Sinyamaziki kusema-
Hukumbuka mali yangu.
Nilitoa kwa mapenzi,
Nipate njema hatima.
Hakuuweza ulezi,
Akanitupa yatima.
Sasa sina usingizi,
Machoni umenibana.
Sinyamaziki kusema-
Hukumbuka mali yangu (uk. 13-14).
Beti hizi za shairi zinaonesha taswira kuwa, mwanaume alifanya kila aliloweza
kumridhisha mkewe lakini mkewe huyo alimuacha mumewe na kuondoka zake.
Mume amepatwa na simanzi kubwa na hata kuanza kujutia mali zake alizotumia
katika kumridhisha mkewe na sasa ameyoyomea kwingine. Hii inathibitisha msemo
wa Waswahili, “fedha siyo kila kitu katika maisha.” Mtu anaweza kuwa na fedha na
mali nyingi lakini akakosa raha na amani katika maisha yake na fedha zake
zisimsaidie kitu.
Mathias Mnyampala anatupatia taswira ya umuhimu wa mzazi au wazazi kuwajali
watoto wao kwa kuwapatia mahitaji yao yote ya msingi katika maisha. Katika shairi
la “Kuku,” lilipo katika Waadhi wa Ushairi anasema:
56
Akose kinywa na kucha, haachi kutabaruku
Watotowe hataacha, Vifaranga vyake kuku
Akichokozwa huchacha, kishikwa na dukuduku
Mfano huo wa kuku, hufatwa na kila chumbe (uk. 3).
Ubeti huu unatupatia taswira kamili ya mzazi hasa mama alivyo na huruma kwa
wanawe. Daima, kuku huwa hawaachi watoto wake mbali na alipo yeye kwa kuhofia
kudhuriwa na maadui kama mwewe na wanyama wengine hatari kwa maisha ya
vifaranga ambao ni kuku wa baadae. Hii inafanana sana na mama ambapo siku zote
huwa karibu na watoto wake popote anapokwenda. Katika nchi zenye vita akina
mama hupata taabu kubwa ya kukimbia mashambulizi kwa sababu hulazimika
kukimbia wakiwa na watoto mgongoni na wengine wadogo mikononi. Hii
huwafanya kukosa kasi ya kukimbia mashambulizi na kuuwawa pamoja na watoto
wao.
Msitari wa mwisho katika ubeti wa shairi hapo juu unaonesha kuwa mfano wa kuku
kujali na kuthamini watoto wake hufuatwa na kila kiumbe. Katika uhalisia, mfano
huu hufuatwa na wanawake kuliko wanaume. Baadhi ya wanaume hutelekeza familia
zao na kuwacha wanawake wakiteseka kuwapatia watoto mahitaji ya maisha
(Ngaiza, 2004; Koda, 2000). Hii inatokana na dhana ya kwamba mwanamke ndiye
mwenye jukumu la kulea watoto na baba ana jukumu la kutafuta mahitaji ya
kujikimu kimaisha. Inapotokea baba ameshindwa kupata mahiyaji hayo huikimbia
familia yake na kumwachia mama mzigo huo mkubwa. Madhumuni ya Mathias
Mnyampala kutoa msitari huo ni kutoa mawaidha kwa wanajamii wote kuiga mfano
wa kuku katika malezi ya watoto na si kumwachia mama peke yake. Mara nyingi
taswira hukaribiana sana na ishara na kwa hiyo ni vema tutazame tamathali ya ishara
inavyojitokeza katika mashairi ya washairi teule.
57
4.2.4 Ishara katika Mashairi ya Washairi Teule
Tamathali ya usemi aina ya Ishara ni dhana au mawazo mbalimbali anayotumia
msanii katika kazi yake ya fasihi kuwakilisha vitu, dhana au mawazo mengine
(Senkoro, 1988). Mathalani, katika shairi la Abdilatif Abdalla la “Mnazi: Vuta
N’kuvute” katika diwani ya Sauti ya Dhiki, mshairi katika kuzisawiri hali za uchumi
na kisiasa zilivyo Afrika ametumia taswira ya mnazi na walanzi, ambayo ni sihara ya
mvutano uliopo baina ya akina ALII na BADI (Senkoro, ameshatajwa). Maelezo
haya yanatupatia ufahamu kuwa, washairi hutumia vitu halisia katika jamii kujenga
ishara ambazo ndani mwake mna dhamira za kijamii, kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni. Shaaban Robert katika shairi lake la “Nyumba za Ngoma” anasema:
Wanawake magunge,
Wamezidi pangapunge,
Heri tusiwahonge,
Wataka kutuibia (uk. 13).
Ubeti huu unatoa ishara kuwa wanawake wanaendekeza sana vitendo vya umalaya
na ukahaba katika jamii kwa ajili ya kujipatia kipato. Hii inaonesha kuwa umalaya na
uasherati vimekuwa ni vitu vya kawaida katika jamii. Mshairi anaonesha pia
wanaume ndio wanaochangia katika kuendeleza vitendo vya umalaya na ukahaba
katika jamii kutokana na kuwahonga wanawake fedha ili wakubaliane kufanya tendo
hilo. Kama wanaume wangekuwa na msimamo wa kutowahonga wanawake ili
kununua ngono, umalaya na ukahaba usingelikuwapo kwa kasi kubwa katika jamii.
Haya ni mawaidha anayoyatoa Shaaban Robert kwa wanaume kama njia ya
kupunguza vitendo vya umalaya na ukahaba katika jamii.
58
Katika Shairi lake jingine la “Nani atakutendea?” ametoa ishara ya ushauri na
mawaidha kwa wanawake nao kutokubali kurubuniwa na wanaume kushiriki katika
ngono zisizo na utaratibu unaotambulikana. Anasema:
Na wanaume magunge
Wamezidi pangapunge
Kina dada tujitenge
Hasara itatujia (uk. 14).
Hii inatoa ishara kuwa si vema kutoa lawama kwa wanawake peke yao kuwa ni
Malaya na asherati na kuwasahau wanaume. Wanaume ni wadau muhimu katika
kuendeleza au kupunguza vitendo vya umalaya katika jamii. Hii ni kwa sababu
umalaya na ukahaba hauwezi kufanywa na mwanamke peke yake bila ya kuwapo
mwanaume. Kwa ubeti huu, Shaaban Robert anatoa mawaidha kwa wanawake
kukataa kudanganywa na wanaume kwa fedha na kukubali kushiriki ngono zitakazo
hatarisha maisha yao.
Mathias Mnyampala kwa upande wake naye pia ametumia tamathali ya usemi ya
ishara kuwasilisha dhamira zinazohusu masuala ya jinsia baina ya wanaume na
wanawake. Katika shairi la “Ubaya” Lilipo katika Waadhi wa Ushairi, anasema:
Nyoka hujiviringisha, akaingia shimoni
Njiani hujiepusha, kukimbia hatarini
Lakini mwovu komesha, akikuuma huponi
Mwovu huwa hajioni, husingizia wengine
Husingizia wengine, kujitoa nuksani
Ubaya wake akane, akajiweka pembeni
Usiku akugugune, akutoe duniani
Mwovu huwa hajioni, husingizia wengine
Ubaya hauna kwao, tangu pembeni pembezoni
Po pote una kikao, tangu hapa na mwishoni
Kwa kila wautakao, hauwatoki maishani
Mwovu huwa hajioni, husingizia wengine (uk. 11-12).
59
Katika beti hizo tatu, mshairi anatoa ishara ya ubaya katika jamii kwa kumtumia
nyoka ambaye huuma watu na kujificha katika shimo akihofia kuuwawa na watu. Hii
ni ishara ya mtu yeyote mwovu katika jamii kwani anapofanya uovu hujificha ili
watu wasimuone. Mtu huyu anaweza kuwa mwanaume au mwanamke. Kwa mfano,
mke wa mtu anaweza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine nje
ya ndoa yake na akawa anakutana kwa siri kubwa na mwanaume huyo. Hufikia
mahali mume na hawara wa mke wakakalishwa meza moja na kula chakula bila ya
kutambuana. Huu ndiyo ubaya wa mwanamke unaofananishwa na ule wa nyoka
kuuma watu na kukimbilia shimoni. Mfano kama huu unaweza pia kumwangukia
mwanaume ambaye tayari ana ndoa au ana mpenzi wake wa kudumu lakini anatoka
nje ya mahusiano hayo. Simu ya nyoka ni kali na huweza kusababisha kifo kwa
aliyeumwa na nyoka. Hii ni sawasawa na mwanaume au mwanamke kutoka nje ya
ndoa na kuukwaa UKIMWI. UKIMWI ni zaidi ya kuumwa na nyoka kwani una
hatari kubwa katika maisha ya mwanadamu.
Matumizi ya lugha ya kisanaa katika kazi za fasihi ni uwanja mpana ambao hauwezi
kutafitiwa katika utafiti huu na kumalizika. Si tu katika utafiti huu, hata katika utafiti
wowote ule unaohusu fasihi ya Kiswahili ni vigumu kwa mtafiti kutafiti vipengele
vyote vya lugha ya kisanaa na kuvimaliza vyote. Vipengele vya matumizi ya takriri,
tashibiha, taswira na ishara vilivyowasilishwa katika utafiti huu vimeweza
kutuwezesha kukamilisha dhumuni mahususi la pili la utafiti huu. Kwa kutumia
vipengele hivi, Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wameweka bayana nafasi ya
mwanamke katika jamii sambamba na ile ya mwanaume. Kwa jumla, washairi hawa
wawili wanaonekana kutumia lugha ya kuwaidhi zaidi juu ya wanawake na wanaume
60
kuacha kutenda mabaya na kuwa watu wema. Mwanamke anasawiriwa kuwa na
nafasi ya juu kabisa katika ulezi wa watoto tafauti na ilivyo kwa baba. Wataalamu
wa masuala ya jinsia wanaiona hali hii kama ukandamizaji wa jinsia ya kike
unaofanywa na wanaume kupitia mfumo dume uliopo katika jamii. Sambamba na
hilo, washairi hawa wawili wameonesha pia mwanaume analo jukumu kubwa la
malezi kwa mtoto na asimwachie mkewe kazi hiyo yeye mwenyewe.
4.3 Falsafa ya Washairi Teule Juu ya Mwanamke
Falsafa kuhusu maisha hutafautiana kutoka mtunzi mmoja na mwingine na baadhi
hufanana. Wahakiki waliohakiki kazi za Kezilahabi kama Frolova (2003) anasema
kuwa kazi hizo zinatoa mkondo wa kifalsafa unaoyaona maisha kuwa hayana maana.
Waliohakiki kazi za Shaaban Robert kama Senkoro (1988) anaziona kazi hizo kuwa
zinayaona maisha kuwa na maana kubwa kwa mwanadamu. Hii ndiyo tafauti ya
falsafa iliyopo baina ya waandishi kuhusu maisha. Ili kutimiza madhumuni mahususi
ya tatu ya utafiti huu tutaanza kwa kutafiti falsafa ya maisha katika mashairi ya
Shaaban Robert na baadae mashairi ya Mathias Mnyampala.
4.3.1 Falsafa ya Shaaban Robert juu ya Mwanamke
Shaaban Robert anamuona mwanamke kuwa na nafasi kubwa katika kuyafanya
maisha ya duniani kuwa mazuri au mabaya. Mwanaume aliyejaaliwa kupata mke
mzuri huishi maisha kama ya peponi. Yule aliyejaaliwa kupata mke mwovu na
msumbufu huishi maisha mabaya ya shida na taabu kama aliye motoni. Falsafa hii
inatokana na mafundisho ya dini ya Kiislamu kwamba mwanamke ni kiumbe wa
kumtumikia mume kwa kumstarehesha kwa starehe mbalimbali za Kibailojia, kijamii
61
na kiutamaduni. Katika shairi la “Dunia Njema” katika kitabu cha Ashiki Kitabu Hiki
anasema:
Dunia nzuri na mambo yake,
Yana fahari ya peke yake,
Juu sayari ni taa zake,
Chini Johari ardhi yake.
Zulia lake nyasi kijani,
Na maji yake mvua mbinguni,
Kushuka kwake milele shani,
Sifa ni zake Mola Manani (uk. 28).
Hii inamaanisha kuwa dunia ni mahali pazuri pa kuishi na kupata starehe za aina kwa
aina kutokana na mambo ya dunia. Msitari wa kwanza wa ubeti huu unajenga ishara
kuwa kinachoifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi ni mambo yake. Mambo
haya ni pamoja na kuwa na mke mwema na mwadilifu. Tumeihusianisha ishara hii
na shairi la “Kuoa” katika diwani hiyohiyo ambalo linaeleza kuwa:
Kuoa mke si kufu,
Atakuliza machozi,
Kwa mambo yake dhaifu,
Ukonde ubaki ngozi,
Huwezi kumsarifu,
Cheo chako hakiwazi,
Kwake kama upuuzi,
Yafahamu yasemwayo (uk. 6).
Hii inamaanisha kuwa kuoa mwanamke ambaye ni muovu na asiye na adabu ni dhiki
kubwa katika maisha ya mwanaume. Kumbe starehe kubwa katika maisha ya
mwanaume ni kuwa na mke mwema. Ili kuepukana na dhiki hii Shaaban Robert
anawataka wanaume kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu kuomba kupatiwa mke
mwema. Mwanamke watakaye muomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu awe
amepambika kwa sifa nzuri. Miongoni mwa sifa hizo ni zile zilizopo katika shairi la
“Urafiki” katika kitabu cha Pambo la Lugha. Anasema;
62
Umbo la kupendeza, kama la malaika
Sura ya kufurahisha, kama ile ya pepo
Umbo la takaso, kama mbingu na mwezi
Hulingani na mkadi, labda luli bahari (uk. 32).
Huyu ndiye mwanamke ambaye Shaaban Robert anamuona kuwa ataweza kumpatia
mwanaume starehe ya duniani. Momanyi (2001) anaziona sifa alizopambwa
mwanamke katika ubeti huu ni za kumfanya kuwa ni kifaa cha kutumiwa na
mwanaume kama chombo cha starehe. Momanyi (ameshatajwa) amesahau kuwa
Falsafa ya Shaaban Robert kumhusu mwanamke ni kuwa, ni kazi na wajibu wa
mwanamke kumpatia mumewe starehe zote anazohitaji katika maisha. Hata hivyo,
tunapingana na mawazo ya shaaban Robert hapo juu kuwa sifa alizompamba nazo
mwanamke katika ubeti hapo juu hazitoshi kumfanya mwanamke kuwa kiumbe
anayeweza kumpatia mwanaume starehe zote anazohitaji katika maisha. Sifa
muhimu aliyoisahau katika ubeti huu ni tabia njema ya mwanamke. Mwanamke
muovu atamfanya mumewe kuwa mtu wa shida na taabu katika maisha yake yote.
Katika kuendeleza falsafa yake kuhusu nafasi ya mwanamke katika maisha ya mume
na jamii kwa jumla, Shaaban Robert anaonya kuwa starehe hizo huwa zina mwisho
wake. Katika Shairi la “Maswali na Majibu” katika Ashiki Kitabu Hiki anasema:
Dunia imetubana,
Imetuvika masombo,
Tulikwenda kwa mapana,
Tukapiga watu fimbo.
Ngoma ikivuma sana,
Ni kupasuka kiwambo,
Roho zimejaa mambo,
Radha ziko wapi tena? (uk. 105).
Hii inaonesha kuwa starehe anazopata mwanadamu hapa duniani ikiwamo ile ya
kuwa na mke mwema na kushiriki naye katika starehe za kingono, hufika mahali
63
zikaisha. Kwa sababu starehe hizo huwa zinakwisha mwanadamu anaaswa
kutoziabudu na kuziendekeza starehe hizo. Kutokana na kuendekeza starehe hizo
baadhi ya watu hutoka nje ya ndoa zao na kujisababishia madhara makubwa ya
kupata maradhi. Pamoja na Shaaban Robert kuonesha falsafa yake juu ya mwanamke
kuwa na nafasi kubwa katika kumpatia mwanaume starehe za dunia ametoa pia
hadhari muhimu kwa wanaume kutoendekeza starehe hizo na kufikia kufanya maasi.
Hadhari hii ni sahihi na inapendeza ikifuatwa na wanajamii katika maisha yao ya kila
siku. Baadhi ya wanaume wanapoona wake zao wamezeeka hutafuta watoto wadogo
wa kike na kuwa na mahusiano nao.
Kwa upande wa pili falsafa ya Shaaban Robert kumhusu mwanamke inaona kuwa
mwanamke anapaswa kupata stahili sawa na zile anazopata mwanaume katika
maslahi ya kazi. Haiwezekani mwanamke na mwanaume wakafanya kazi iliyo
sawasawa halafu mwanamke akapata ujira kidogo na mwanaume ujira mkubwa. Kwa
mfano, wakati mwanaume anakwenda kazini asubuhi mwanamke hubaki nyumbani
kulea watoto wao na kufanya kazi za ndani kama kufua nguo, kuosha vyombo,
kusafisha nyumba, kuandaa chakula na kuwahudumia watu wote waliopo katika
nyumba yao. Kazi hizi huwa hazina malipo kwa mwanamke na hata akiwa na shida
yoyote ile inayohitaji kutatuliwa kwa fedha inakuwa vigumu kuitatua. Mwanaume
ambaye amemwachia mke mzigo mzito wa shughuli nyumbani hulipwa mshahara na
hathubutu hata mara moja kumkumbuka mke ambaye ndio anayeandaa mazingira
mazuri ya mume kufanya kazi. Katika shairi la “Nani Atakutendea” anaeleza:
Kazi bila manufaa,
Nani atakutendea,
Sinifanyie hadaa,
Kungwi hakunihusia.
64
Sinifanyie hamaki,
Shetani wangu hataki,
Sharti unipe haki,
Ndipo ataputulia (uk. 13).
Shairi hili linaonya kuwatumikisha wanawake kwa kazi nyingi bila ya kuwapatia
malipo stahiki au hata kutambua mchango wao. Usawa wa malipo baina ya
mwanaume na mwanamke katika kazi ni kitu muhimu kitakacholeta ustawi wa
maisha ya wanaadamu wote katika maisha yao ya duniani.
4.3.2 Falsafa ya Mathias Mnyampala juu ya Mwanamke
Mathias Mnyampala ana fanana na Shaaban Robert juu ya falsafa ya maisha
kumhusu mwanamke. Anamuona mwanamke kuwa ni kiumbe muhimu katika
kumsaidia mwanaume kutimiza majukumu yake. Haya yanabainika katika shairi
“Taji la Nyumba” kwa mfano:
Taji kitu cha heshima, avae vema mvaaji,
Atulizane mtima, kama mtungi na maji,
Si vae mwenye kilema, hawi huyo mtunzaji,
Mke mwema ndiye taji, la utukufu wa mumewe.
Taji lipambiwe zari, zaujati na zauji,
Mume ni bwana shauri, kwa jamii mtunzaji,
Taji hili la fahari, nyumbani linafariji,
Mume mwema ndiye taji, la utuvu wa mkewe.
Asiye heshima mke, atakuwa mfujaji,
Hata pia mume wake, akiwa mkorogaji,
Na taji lisichafuke, kwa mambo ya ulewaji,
Mume na mke ni taji, la utukufu wa nyumba (uk. 11).
Hii inamaanisha kuwa mwanamke ana nafasi kubwa katika kuyaimarisha maisha ya
mumewe. Mwanamke akiwa mtu mwema kwa mumewe, mume huyo atapata raha
isiyokifani katika maisha yake. Katika ubeti wa kwanza msitari wa kwanza
65
tunaelezwa sifa za taji na kazi zake. Taji huvikwa mtu aliyepata mafanikio maalumu
kama ishara ya kumpongeza kwa mafanikio yake. Mwanamke kufananishwa na taji
ni sawa na kusema kwamba muonekano wa mume ulivyo hufanywa na mke. Kama
mume ni nadhifu na mwenye furaha, ni zao la mke katika jitihada za kumnawirisha
mume wake. Na kama mume ni mkondefu, asiye na furaha na mchafu pia ni zao la
mke wake. Hili linapatikana katika msitari wa mwisho wa ubeti wa kwanza, “mke
mwema ndiye taji la utukufu wa mume.”
Mathias Mnyampala hakuwa na upendeleo katika falsafa yake juu ya nafasi ya
mwanamke katika jamii na kwa mumewe. Katika ubeti wa pili anaonesha kuwa, ili
mwanamke aweze kumfanya mumewe kuwa na utukufu katika jamii ni lazima apate
ushirikiano kutoka kwa mumewe. Mume ndiye ambaye atamfanya mkewe afanye
kazi za kumnawirisha na kumfanya mumewe kuwa na utukufu katika jamii.
Mwanamke anahitaji utulivu wa nafsi ili kuweza kumhudumia mumewe. Utulivu huo
wa nafsi kwa mke utapatikana kama mwanaume atampenda mkewe na kutomsaliti
kwa kutembea na wanawake wengine nje ya ndoa yao. Katika ubeti wa mwisho wa
shairi la “Taji la Nyumba” kunatolewa msisitizo kuwa ustawi wa familia ni mume na
mke wote kuwa watu wema. Si mke au mume peke yake anayeweza kujenga ustawi
katika maisha bali wote wawili.
4.3.3 Hitimisho
Kwa jumla Shaaban Robert na Mathias wanaonekana kutawaliwa na mawazo ya
mfumo dume katika kumsawiri mwanamke. Falsafa zao zinamtazama mwanamke
kama kiumbe asiyeaminika na msaliti katika maisha ya ndoa. Mwanamke
anasawiriwa kuwa ni kiumbe anayependa fedha na huweza kufanya jambo lolote
66
baya kwa ajili ya kujipatia fedha. Haya yanaonekana pale wanapomsawiri
mwanamke kama kiumbe Malaya na kahaba anayeendekeza vitendo vya kiasherati.
Kwa kiasi kidogo mwanaume naye amesawiriwa kujihusisha na vitendo hivyo vya
umalaya na uasherati. Tulidhani ingekuwa vema mwanaume akasawiriwa kuwa
ndiye anayeoongoza katika vitendo hivyo vya umalaya na uasherati. Daima,
mwanaume ndiye huanza kumtongoza mwanamke kushiriki naye ngono. Mwanamke
hukubali na ndiyo azma hiyo hufanikiwa. Katika hali ya kawaida yule anayeanza
kumshawishi mtu mwingine kufanya jambo baya huwa ndiyo mbaya wa kwanza na
nafasi ya pili humwangukia yule aliyeshawishika. Katika hali ya kushangaza,
mwanamke ambaye yupo katika nafasi ya kushawishika, ndiye anaonekana kuwa
mbaya zaidi kuliko wanaume.
Pia, falsafa juu ya nafasi ya mwanamke inayosawiriwa na Mathias Mnyampala na
Shaaban Robert inaonekana kupata mizizi yake katika mafundisho ya dini zao.
Shaaban Robert ni Muislamu na Mathias Mnyampala ni Mkiristo. Dini hizi mbili
zimetoa mchango mkubwa katika kujenga falsafa yao juu ya mwanamke. Kwa
mfano, katika uchambuzi wa data imebainika kuwa mwanamke anapaswa
kumnyenyekea mwanaume kwa lugha na maneno mazuri yasiyokuwa ya karaha na
matusi. Momanyi (2001) anaunga mkono hoja hii na kusisitiza kwamba, lugha ya
matusi haipendezi kwa mtu yoyote na si kwa mwanamke pekee. Hata hivyo,
mwanamke kusisitizwa kutokuwa na lugha ya matusi ni kitu cha msingi sana kwa
sababu mwanamke ndiye hulea watoto. Hii ni sawa na kusema kuwa, mwanamke
hutumia muda wake mwingi kukaa na watoto kuliko mwanaume. Ikitokea
mwanamke akawa ni mtu wa kutukanatukana hovyo hovyo iko hatari kubwa kwa
67
watoto kujifunza lugha ya matusi kutoka kwa mama yao. Falsafa hii ya Shaaban
Robert na Mathias Mnyampala kumuhusu mwanamke ni muhimu sana katika
kuimarisha maadili ya jamii.
Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wanaonekana kuwa na falsafa ya kuwaidhi
jamii kama njia ya kuleta mabadiliko ya kimaadili kwa wanajamii wote. Mashairi
yao mengi yamekaa katika mtindo wa kukataza mambo mabaya na kuamrisha
kutendwa kwa mambo mema ndani ya jamii. Ingawa msisitizo wao unaonekana
kuilenga jamii nzima lakini kwa kiasi kikubwa mwanamke ndiye anayeonekana
kulengwa zaidi na mawaidha yao. Hii inatufanya tuelewe kuwa mabadiliko ya
mwanamke kitabia na kimaadili yana mchango mkubwa katika maendeleo ya kitabia
na kimaadili ya jamii nzima. Ni sawasawa kabisa na ule msemo wa Waswahili
usemao “ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima.” Msemo huu
tumepata kuusema hapo awali na tumeurudia hapa ili kukazia maarifa na uelewa
wetu juu ya falsafa walizo nazo Shaaban Robert na Matias Mnyampala juu ya nafasi
ya mwanamke ndani ya jamii.
68
SURA TA TANO
MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
5.0 Utangulizi
Muhtasari, hitimishi na mapendekezo ya utafiti wote yanatolewa katika sura hii.
Muhtasari wa sura zote tano za tasinifu hii utatolewa na kisha kufuatiwa na
muhtasari wa madhumuni mahususi ya utafiti. Baada ya hapo kutatolewa hitimishi
na mwisho itakuwa ni mapendekezo.
5.1 Muhtasari wa Sura za Tasinifu
Utafiti huu una jumla ya sura tano. Sura ya kwanza inahusu utangulizi wa utafiti
ukihusisha vipengele vya usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, lengo kuu la
utafiti, madhumuni mahususi na maswali ya utafiti. Vipengele vingine ni umuhimu
wa utafiti, mipaka ya utafiti na matatizo ya utafiti na utatuzi wake. Kutokana na
vipengele hivi tumeweza kuweka haja ya kufanyika kwa utafiti huu wazi na bayana.
Sura ya pili ya utafiti huu imewasilisha utalii wa kazi tangulizi na mkabala wa
kidhamira. Utalii wa kazi tangulizi umefanywa kwa kuanza na kazi zilizofanywa
katika kuhakiki mashairi ya Shaaban Robert na kisha kufuatiwa na kazi tangulizi
zilizotafiti mashairi ya Mathias Mnyampala. Katika sura hii pia tumewasilisha
nadharia ya Ufeministi ambayo ndiyo iliyotumika katika uhakiki wa nafasi ya
mwanamke katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala.
Sura ya tatu ya utafiti huu imewasilisha njia za utafiti. Njia hizo zimehusisha eneo la
utafiti, kundi lengwa, sampuli ya utafiti, mbinu za ukusanyaji wa data; usaili, hojaji
na usomaji makini. Vipengele vingine ni mbinu ya uchambuzi wa data ya mkabala
69
wa kidhamira, kuaminika kwa data za utafiti na usahihi wa data za utafiti
zilizokusanywa.
Sura ya nne ya tasinifu hii imewasilisha, kuchambua na kujadili data za utafiti. Data
hizo zilichambuliwa kwa kufuata mtiririko wa madhumuni mahususi ambapo
dhumuni mahususi la kwanza lilihusu kulinganisha na kulinganua nafasi ya
mwanamke katika mashairi ya Mathias Mnyampala na Shaaban Robert.
Yaliyowasilishwa kuhusiana na dhumuni hili ni mwanamke kama chombo cha
starehe, mwanamke ni mpole na mnyenyekevu, mama na mlezi katika jamii,
mwanamke na suala la uaminifu na suala la uasherati na umalaya katika jamii.
Madhumuni mahususi ya pili yalihusu kulinganisha na kulinganua matumizi ya
lugha ya kisanaa inayotumiwa kusawiri nafasi ya mwanamke katika mashairi ya
Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Yaliyobainika katika madhumuni haya ni
matumizi ya takriri, matumizi ya tashibiha, matumizi ya taswira na mwisho ni
matumizi ya ishara.
Madhumuni mahususi ya tatu ya utafiti huu yalihusu kulinganisha na kulinganua
falsafa ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala juu ya mwanamke.
Yaliyowasilishwa katika madhumuni mahususi haya ni falsafa ya Shaaban Robert
juu ya mwanamke na baadae kufuatiwa na falsafa ya Mathias Mnyampala.
Sura ya tano ya tasinifu hii ndio inayowasilisha muhtasari, hitimishi na mapendekezo
yanayohusu utafiti mzima. Katika mtiririko wa sura za tasinifu hii, sura ya tano ndiyo
ya mwisho.
70
5.2 Hitimisho
Hitimisho linalotolewa katika sehemu hii, limezingatia madhumuni ya utafiti ambayo
jumla yake yalikuwa matatu.
5.2.1 Usawiri wa Nafasi ya Mwanamke katika Mashairi ya Washairi Teule
Usawiri wa mwanamke kama chombo cha starehe kwa mwanaume ni dhamira
inayoendelea kujitokeza kama dhamira maarufu katika kazi za ushairi za Shaaban
Robert na Mathias Mnyampala. Shaaban Robert kwa mfano, ametumia lugha ya
ishara kuonesha kwamba mwanaume hata akizeeka bado anakuwa na tama ya
kufanya ngono za wasichana wadogo. Kimsingi mwanaume huyo hana nguvu za
kuweza kufanya tendo la ngono kwa ufanisi lakini kwa sababu anamuona
mwanamke kama chombo cha starehe basi anamtamani. Mathias Mnyampala kwa
upande wake anamuona mwanamke anayeshiriki katika vitendo vya umalaya na
uasherati kuwa anatumia kama chombo cha starehe kwa wanaume. Kama kawaida
yake Mathias Mnyampala anatoa waadhi kwa watu kujiepusha na vitendo hivyo
kupitia shairi la “Malaya” lililopo katika Waadhi wa Ushairi.
Washairi wote wawili wanaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe anayetakiwa mpole
na mnyenyekevu kwa mume. Unyenyekevu wake utaonekana katika lugha
anayoitumia anapoongea na mume wake. Hapaswi kutumia lugha ya matusi wala
kujibizana na mume wake. Ngonjera ya “Mke kumba ruhusa kwa Mume” ni mfano
mzuri unaonesha maonyo kwa mke kufanya mabishano na mumewe. Hata hivyo,
ngonjera hii inaonesha wanawake kuanza kuruka viunzi vya mfumo dume na kuanza
kubishana kwa baadhi ya mambo na waume wao.
71
Mwanamke anasawiriwa kuwa na nafasi kubwa katika malezi ya watoto kutokana na
kukaa nao kwa muda mrefu katika siku kuliko ilivyo kwa wanaume. Kwa nafasi hiyo
mwanamke hapaswi kutumia lugha ya matusi kwani ni rahisi kwa watoto kuiga
lugha hiyo kutoka kwa mama yao. Washairi wote wawili wanaonesha kuwa
mwanamke huelemewa na mzigo wa kulea watoto wengi na wakati huo huo
akishughulika kwa shughuli nyingine za nyumbani. Wito unaotolewa na washairi
hawa kwa wanaume ni kuwa wanaume nao washiriki katika kulea watoto na
wasiwaachie wanawake peke yao.
Suala la uasherati na umalaya limeonekana kusukumiwa kwa mwanamke peke yake
hali ya kuwa wote wawili hushiriki katika tendo hilo. Shaaban Robert anaonekana
kumsawiri mwanamke kuwa ni kinara wa umalaya na uasherati. Mathias Mnyampala
anaonekana kuwalaumu wanawake na wanaume kuwa wote ni wahanga wa umalaya
na uasherati. Mwanaume ndiye anaanza kumtongoza mwanamke na mwanamke
akikubali ndiyo tendo la ngono hufanyika. Kama mwanaume akinyamaza kimya bila
ya kutongoza wanawake umalaya na uasherati hautakuwepo katika jamii.
5.2.2 Matumizi ya lugha ya Kisanaa katika Mashairi ya Washairi Teule
Matumizi ya lugha ya kisanaa yanayojitokeza katika mashairi ya Shaaban Robert na
Mathias Mnyampala ni mengi nasi tumeteua manne tu. Matumizi hayo ni yale ya
takiriri, tashibiha, taswira na ishara. Mbinu hizi za kisanaa kwa ujumla wake
zimetumika kutoa msisitizo wa mambo ya msingi ambayo watunzi wapenda jamii
iyapate. Kwa mfano, tumeona katika shairi la “Mama” neno “mama” limerudiwa
mara nane ili kuonesha kuwa mama ni muhimu sana katika ustawi wa jamii na
maendeleo yake kwa jumla. Tashibiha zilizotumika katika kazi za Shaaban Robert na
72
Mathias Mnyampala zinamsawiri mwanamke kama kiumbe ambaye ana uwezo
mkubwa wa kuweza kumfanya mwanaume akaishi au asiishi kwa furaha duniani.
Mwanamke huweza kutibua saikolojia ya mwanaume na kumfanya kuwa na mawazo
yenye kutafuna mwili wake na kumkondesha. Ushauri unaotolewa na washairi hawa
ni kuwa ni lazima mwanaume ampende mkewe kwa dhati ili naye apendwe na
mkewe. Hii itawafanya kujaliana na kupendana na kutosababishiana matatizo ya
kisaikolojia.
5.2.3 Falsafa ya Washairi Wateule juu ya Mwanamke
Washairi wote wawili wanafalsafa juu ya mwanamke inayokaribiana na kufanana
sana kuliko inavyotafautiana. Wanamuona mwanamke kuwa ni kiumbe mwenye
nafasi ya juu katika kuleta ustawi wa familia na jamii. Mwanamke ndiye anayeandaa
kizazi na taifa la kesho. Ikitokea mwanamke akapata elimu ya kutosha huwa vema
katika kuwalea watoto kwa kuwamegea sehemu ya elimu yake na kuwafanya kuwa
vijana wenye maadili.
Kwa upande mwingine bado wanaonekana kumsawiri mwanamke kama kiumbe
dhaifu ambaye huingia katika maovu kwa vishawishi vya wanaume. Kutokana na
hili, mwanamke anaonekana kuwa yeye ndiyo chanzo cha matatizo mengi yakiwamo
maradhi katika jamii. Mtazamo huu unajitokeza zaidi katika mashairi ya Shaaban
Robert kuliko katika mashairi ya Mathias Mnyampala. Mnyampala anaonesha
kwamba, mwanaume na mwanamke wote kwa pamoja wana nafasi sawa katika
kuleta maasi na maovu katika jamii. Maovu kama ya zinaa hayafanywi na mtu
mmoja bali wote wawili. Mwanaume anaweza akalaumiwa zaidi kwa sababu mara
73
nyingi yeye amekuwa ndiyo muanzilishi wa maovu hayo kwa kumtongoza
mwanamke.
5.3 Mapendekezo
Shaaban Robert na Mathias Mnyampala wameandika vitabu vingi vya mashairi
vinavyoeleza nafasi ya mwanamke katika jamii. Katika utafiti huu tumeteua sehemu
tu ya vitabu hivyo visivyofikia nusu ya vitabu vyo. Itakuwa vema kama watafiti
wengine nao watachunguza nafasi ya mwanamke katika vitabu vingine vya ushairi
vya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala.
Watafiti wajao wanaweza wakatafiti kwa kina zaidi matumizi ya lugha ya kisanaa
inavyotumika katika mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala. Sisi
tulifanya matumizi ya lugha ya kitamathali kuwa ni moja kati ya mathumuni
mahususi ya utafiti wetu. Watafiti wajao wanaweza kulifanya hili kuwa lengo kuu
katika utafiti wao.
Ingawa Shaaban Robert na Mathias Mnyampala ni watunzi wa mashairi ya
kimapokeo lakini wanatafautiana katika vipengele kadhaa vya kifani katika utunzi
wao wa mashairi. Utafiti zaidi unaweza kufanywa ili kubainisha namna Shaaban
Robert wanavyofanana na kutofautiana katika matumizi ya vipengele vya kifani
katika mashairi yao. Mathalani, Mathias Mnyampala ana matumizi ya mtindo wa
ngonjera katika mashairi yake. Je, Shaaban Robert naye ana matumizi ya mtindo
kama huo? Utafiti zaidi ufanyike.
74
MAREJELEO
Abdullazizi, M.H. (1969), “Ukumbusho wa Marehemu Shehe Shaaban Robert
Mathias E. Mnyampala,” katika Kiswahili. Namba 39, Dar es Salaam: TUKI,
Kur. 2-4.
Babbie, E (1992) The Practice of Social Research. 6th
edition. Wadsworth Publishing
Company.
Best and Kahn, J. (1993). Research in Education. New York: Allyn Bacon Inc.
Borg, W.R and Gall, M.D, (2003).Educational Research: An Introduction. Longman
London.
Chuachua, R., (2011), Itikadi katika Riwaya za Shaaban Robert, Dar es Salaam:
TATAKI.
Cohen, na Wenzake, (2000) Research Methods in Education. 5th
edition. London:
Rutledge Falmer.
Frolova, N. (2003). “Euphrase Kezilahabi: The Renewal of Kiswahili Poetry”. In
Kiswahili, Vol. 66 Dar es salaam. IKR.
Inyani, S.K. (2002). Utafiti wa Kiswahili na Maswala ya Uana: Utafiti wa Kiswahili.
Nairobi. Downtown Printing Works ltd.
Creswell, J.W., (2009), Research Design: Qualitative, Quantitatie, and Mixed
Methods Approaches. Los Angeles: SAGE Publication.
John, L., (2007), Critical Reading: A Guide. In http://www. Brocku.
Ca/English/jlge/criticalreadig. Html. Accesssed, 30th
, October 2006.
75
Kezilahabi, E. (1976a), Ushairi wa Shaaban Robert. Nairobi. EALB.
Kezilahabi, E. (1976b), “Shaaban Robert Mwandishi wa Riwaya,” Tasinifu ya M.A
Kiswahili, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Kezilahabi, E. (1983), “Uchunguzi katika Ushairi wa Kiswahili,” katika Makala ya
Semina za Kimataifa za Kiswahili namba 3. Dar es Salaam: TUKI.
Khalifa, A.I.S. (2012), “Usawiri wa Masuala ya Kijinsia katika Lugha ya Mashairi.
Mifano Kutoka Mashairi ya Bongo Fleva Tanzania”, Dar es Salaam. Tasnifu
ya M.A. Kiswahili. Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
Khatibu, M.S. (1985), “Utenzi wa Mwanakupona,” katika, Mulika namba 17, Dar es
Salaam: TUKI, Kur. 46-52.
Kihore, Y. M. (1978), “Waadhi wa Ushairi,” katika Mulika, Namba. 12. Dar es
Salaam: TUKI. Kur, 54-59.
Koda, B. (2000) “The Gender Dimension of Land Rights in Tanzania: Case Study of
Msindo Village, Same District”, Unpublished Ph.D Thesis, UDSM.
Kothari, R.C. (2009) Research Methodology. Methods and Techniques New Delhi:
New Age International (P) Limited, Publishers.
Lyatuu, J. (2011), “Usawiri wa Wanawake katika Fasihi ya Kiswahili: Ulinganifu wa
Waandishi wa Kike na Kiume: Uchaguzi katika Riwaya Teule,” Tasnifu ya
M.A. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Macknnon, C.A. (1991), Toward A Feminist Theory of State. London: Havard
University Pess.
76
Maganga, M.A (1971), “Maisha ya Shaaban Robert na Mawazo yake,” katika
Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili. Nairobi: OUP, pp. 33-54.
Massamba, D. P. B. (1983), “Suala la Ushairi wa Kiswahili,” Katika Makala ya
Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili-Fasihi namba 3. Dar es
Salaam: TUKI.
Mnyampala, E. M. (1965), Waadhi wa Ushairi. Dar es Salaam: East African
Literature Bureau.
Mnyampala, E.M. (1970), Ngonjera za UKUTA: Kitabu cha Kwanza. Dar es Salaam:
OUP.
Momanyi, C. (2001), Nadharia ya Uchanganuzi Nafsia katika Mtazamo wa Kike na
Uhakiki wa Kifasihi: Kioo cha lugha. Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar
es salaam.
Momanyi, C. (2007), Patriarchal Symbolic Order: The Syllables of Power as
Accentuated in Waswahili Poetry. The Journal of Pan African Studies, Vol.1,
no. 8.
Moore, H. (1998), Feminism and Anthropology. Mimepolis: University Press of
Minnesota.
Mulokozi, M. and Kahigi, K.K. (1979), Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es
Salaam: TPH.
Ndulute, C.L (1985), Politics in Poetic Garb: The Literary Fortunes of Mathias
Mnyampala,” in Kiswahili, Vol. 52/1&2, Dar es Salaam: TUKI, PP 143-160.
77
Ndulute, C.L. (1987), “Shaaban Robert’s Poetic Land Scape: From Ethinicism to
Nationalism,” in Kiswahili, Vol. 54. Dar es Salaam: TUKI, pp 110-125.
Ndulute, C.L. (1994), The Poetry of Shaaban Robert. DUP: Dar es Salaam.
Ngaiza, M.K. (2002), “Gender Dynamics in Poverty Alleviation in Tanzania: Ngara
District Case Study.” Unpublished, Ph.D. Thesis, UDSM.
Ngaiza, M.K. (2004), “Harmonization and Mainstreaming Gender in Local
Government or Transforming Patriarchy: The Case of Two Wards in Bukoba
District Council, Tanzania,” In: Tanzania Journal of Development Studies,
Vol. 5, No. 3 page 25-38.
Njogu, K. na Rocha, C. (1999), Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi,
JKF.
Ramadhani, S. K. (2013), “Usawiri wa Mwanamke Katika Taarab ya Mipasho:
Mfano Kutoka Nyimbo za Mzee Yussuf Mzee”. Tasinifu ya M.A. Kiswahili,
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Robert, S. (1948), Pambo la Lugha. London: Nelson.
Robert, S. (1951), Kusadikika. London: Nelson.
Robert, S. (1967), Kufikirika. Nairobi: OUP.
Robert, S. (1968), Ashiki Kitabu Hiki. London: OUP.
Robert, S. (1968), Kilelezo cha Fasili. London: Nelson.
Robert, S. (1969), Mwafrika Aimba. London: Nelson.
78
Robert, S. (1971), Insha na Mashairi. London: Nelson.
Robson, C., (2007), How to do a Reserch Project: A Guide for Undergraduate
Students, Carton Victoria: Blackwell Publishing.
Sengo, T.S.Y., (1975), Shaaban Robert: Uhakiki wa Maandishi Yake, Nairobi:
Foundation Books.
Senkoro, F.E.M.K (1968), “Mwamko wa Kisiasa katika Ushairi wa Shaaban
Robert,” Katika Mulika, Namba 8, Kur. 26- 36.
Senkoro, F.E.M.K (1988), Ushairi: Natharia na Tahakiki. DUP: Dar es Salaam.
Shao, I.F. (2004), “Context for Gender Mainstreaming Internationally, Regionally
and Nationally,” Paper Presented at a Gender Sensitization Workshop for
UDSM Council Members, Zanzibar.
Taib, A.H., (2009), “Maisha ya Shaaban Robert na Falsafa yake katika Maandishi,”
katika Mulika, kur. 130-147. TUKI.
Taib, A.H., (2009), “Maisha ya Shaaban Robert na Falsafa yake katika Maandishi,”
katika Mulika, kur. 130-147. TUKI.
Wafula, R. M na Njogu, K (2007), Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: The
Jomo Kenyatta foundation.
Walibora, K.W. (2013), “Ujasiri wa Kujimulika katika Uandishi wa Kiswahili:
Uhakiki wa Mbali na Nyumbani,” Tawasifu ya Shafi Adam Shafi.
79
Wamitila, K.W., (2008), Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi,
Nairobi: Vide-Muwa.
Young, P.V., (1984), Scientific Social Surves and Research, Enalewood Chiffs:
Prentice Hall. Inc.
Yin, R.K., (1994), Case Study Research: Design ad Methods, (2nd
eds. Thousands
Oaks Calif: SAGE publishers.
80
VIAMBATANISHO
Kiambatisho A
Dodoso la Usaili wa Ndugu Jamaa na Marafiki wa Shaaban Robert na Mathias
Mnyampala
Ninaitwa Ally Edris mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Kiswahili Chuo
Kikuu Huria Cha Tanzania. Ninafanya utafiti juu ya Mashairi ya Shaaban Robert na
hivyo ninaomba ushirikiano wako katika kukamilisha utafiti wangu. Ninayo maswali
machache ambayo ninataka kukuuliza huku nikitanguliza shukurani zangu za dhati
kwako.
Maswali ya Kudodosa
Sehemu A: Maswali juu ya Shaaban Robert
1. Ninaomba unieleze namna unavyomfahamu Shaaban Robert.
2. Shaaban Robert alikuwa na mahusiano gani na mabinti na wanawake kwa
ujumla?
3. Shaaban Robert alipenda kuona mwanamke anapata au anapatiwa nini katika
maisha?
4. Umekwishawahi kusoma kazi yoyote ya mashairi ya Shaaban Robert?
5. Shaaban Robert anaeleza nini katika mashairi hayo?
6. Ni upi mtazamo na falsafa ya Shaaban Robert juu ya nafasi ya mwanamke katika
jamii?
7. Ni mambo gani yaliyomfanya Shaaban Robert kumsawiri mwanamke hivyo
alivyomsawiri katika mashairi yake.
81
Sehemu B: Maswali kwa Ndugu na Jamaa wa Mathias Mnyampala
8. Ninaomba unieleze namna unavyomfahamu Mathias Mnyampala.
9. Mathias Mnyampala alikuwa na mahusiano gani na mabinti na wanawake kwa
ujumla?
10. Mathias Mnyampala alipenda kuona mwanamke anapata au anapatiwa nini
katika maisha?
11. Umekwishawahi kusoma kazi yoyote ya mashairi ya Mathias Mnyampala?
12. Mathias Mnyampala anaeleza nini katika mashairi hayo?
13. Ni upi mtazamo na falsafa ya Mathias Mnyampala juu ya nafasi ya mwanamke
katika jamii?
14. Ni mambo gani yaliyomfanya Mathias Mnyampala kumsawiri mwanamke
hivyo alivyomsawiri katika mashairi yake.
Ninakushukuru Sana
82
Kiambatanisho B
Hojaji kwa Waliotafiti Mashairi ya Shaaban Robert na Mathias Mnyampala
Ninaitwa Ally Edris mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Kiswahili Chuo
Kikuu Huria Cha Tanzania. Ninafanya utafiti juu ya Mashairi ya Shaaban Robert na
hivyo ninaomba ushirikiano wako katika kukamilisha utafiti wangu. Ninayo maswali
machache ambayo ninataka kukuuliza huku nikitanguliza shukurani zangu za dhati
kwako.
Maswali ya Kuhoji
Sehemu A: Maswali juu ya Shaaban Robert
1. Taja kazi za Mashairi ya Shaaban Robert ambazo
umezisoma…………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
…………
2. Kazi ipi ya Ushairi ambayo imekuvutia sana na kwa nini?
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
………
3. Shaaban Robert amempa mwanamke nafasi gani katika mashairi
yake………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
………….
4. Unafikiri ni kwa nini amempa nafasi hiyo
aliyompa……………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………………
……………
5. Nini Falsafa ya Shaaban Robert juu ya mwanamke katika
jamii?.........................................................................................................................
...................................................................................................................................
...................................................................................................................................
83
...................................................................................................................................
...................................................................................................................................
....................
Sehemu B: Maswali juu ya Mathias Mnyampala
1. Taja kazi za Mashairi ya Mathias Mnyampala ambazo
umezisoma……………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
………………………
2. Kazi ipi ya Ushairi ambayo imekuvutia sana na kwa nini?
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
3. Mathias Mnyampala amempa mwanamke nafasi gani katika mashairi
yake……………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………….
4. Unafikiri ni kwa nini amempa nafasi hiyo
aliyompa………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………
……………………………
5. Nini Falsafa ya Mathias Mnyampala juu ya mwanamke katika
jamii?...................................................................................................................
.............................................................................................................................
.............................................................................................................................
..........................................................................................................
Ninakushukuru Sana