jamhuri ya muungano wa tanzania2016/06/21 · 1 a. utangulizi 1. mheshimiwa spika, napenda kutumia...
TRANSCRIPT
-
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
UFAFANUZI WA HOJA ZA WAHESHIMIWA
WABUNGE AKICHANGIA HOTUBA ZA WAZIRI WA
FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB)
AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI 2015 NA
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17 PAMOJA NA BAJETI
KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/17
JUNI 20, 2016
DODOMA
-
1
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe
binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri
majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango
wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8 Juni, 2016.
2. Mheshimiwa Spika, Kipekee, ninampongeza sana Mhe. Naibu
Spika kwa umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia
Kanuni za Bunge wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika
viwango vyake ni vya kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda,
mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri, (nadhani
alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!), nataka niliambie
Bunge lako tukufu kwamba kwa viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika
alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi za haki asilimia 100
kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT. Hongera sana.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na:
Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman
Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde,
Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge
wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni.
Ninawashukuru wote.
-
2
4. Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 158 wamechangia hoja
niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza na 25
kwa maandishi.
B: HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI
5. Mheshimiwa Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi
wakati wa mjadala juu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya
Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:
Kuthubutu kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja na kuanza ujenzi
wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, barabara,
umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za
abiria;
Kuongeza ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi
kufikia wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba
mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha matumizi ya vifaa vya
kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na Hazina kutoa
fedha hizo kama ilivyopangwa;
Kusimamia nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo
ya lazima ikiwa pamoja na safari za nje, posho, sherehe, kuondoa
watumishi hewa katika utumishi wa umma;
Kuhimiza azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya
watumishi kazini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa;
-
3
Kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;
Kuanzisha mahakama ya kushughulikia mafisadi;
Kuweka kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili
kupanua fursa za ajira na wigo wa kodi; na
Kujielekeza kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi
wakuu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kutatua kero za
wananchi, hasa masikini.
C: USHAURI ULIOTOLEWA NA WABUNGE WENGI
6. Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi pia walitoa ushauri katika
maeneo mbalimbali, ili yazingatiwe katika bajeti hii au bajeti zijazo.
Naomba kurejea ushauri muhimu uliotolewa na Wabunge kama
ifuatavyo:
Kuongeza tozo kwenye mafuta ili mapato hayo yatumike kupanua
huduma za maji na na kukamilisha vituo vya afya na zahanati
vijijini;
Kuboresha mfumo wa kodi ikiwa pamoja na kufuta kodi, ushuru
na tozo za kero kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara
wadogo, wakati na wakubwa/ wawekezaji, lakini pia kutoa ahueni
ya kodi kwenye taulo za akinamama na vifaa vya watu wenye
ulemavu, vifaa vya michezo, zana za uvuvi, na kulinda viwanda
vya ndani;
-
4
Kuchukua hatua za ziada kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na
uvuvi kwa kuongeza kilimo cha umwagiliaji, pembejeo, ugani,
utafiti, mnyororo wa thamani, masoko, ruzuku, mikopo na bajeti
ya kilimo;
Kuimarisha utalii kwa kuzingatia fursa za kipekee za Tanzania
katika sekta hii;
Kuchukua hatua madhubuti kulinda mazingira na kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi;
Shilingi milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji ziwekewe utaratibu
mzuri na endelevu;
Kuongeza kasi ya kulipa madeni ya ndani (watumishi, wastaafu,
wakulima, watoa huduma & makandarasi);
Kuimarisha elimu na kuhakikisha inaendana na mahitaji ya
wataalam wa Tanzania ya leo na kesho;
Kupanua wigo wa kodi hususan katika sekta zenye mapato
makubwa kama mawasiliano, madini, maliasili na ardhi, na sekta
nyingine zenye fursa kama uvuvi na biashara kwenda nchi jirani,
e-commerce, gawio kutoka katika mashirika ya umma, sambamba
na kuhakikisha kila mwananchi analipa kodi stahiki ili kuchangia
maendeleo ya Taifa na kupunguza utegemezi;
-
5
Kupambana na uvujaji wa mapato hususan katika biashara ya
mafuta, miamala ya kielektroniki, transfer pricing na misinvoicing,
misamaha ya kodi, wizi na udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi,
maduka ya jumla, n.k.
Kuimarisha ushirikishwaji wa wadau ikiwa ni pamoja na Bunge,
katika maandalizi ya mipango na bajeti ya Serikali;
Kuendeleza utulivu wa uchumi ikiwa pamoja na kudhibiti mfumuko
wa bei, kuongezeka kwa kasi deni la Taifa, kushuka kwa thamani
ya shilingi, matumizi ya dola sambamba na shilingi (dollarisation),
kupanua huduma za kibenki hadi vijijini na kupunguza riba;
Kuboresha sheria mbalimbali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji
na kufanya biashara nchini;
Kuchukua tahadhari katika kufanya mageuzi katika mfumo wa kodi
na tozo nchini ili kuepuka kudhoofisha halmashauri na utekelezaji
wa dhana ya (ugatuaji madaraka D by D);
Kutoa msukumo zaidi kwa ushiriki wa sekta binafsi katika
utekelezaji wa miradi ya kipaumbele, ikiwa pamoja na PPP;
Kuanzisha duka la kununua madini kutoka kwa wafanya biashara
wadogo kutoka nchi jirani na kutoza kodi ya asilimia moja
Kuandaa mikakati mahsusi kwa ajili ya kukabiliana na umasikini
-
6
katika mikoa masikini zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia upya
uwiano katika mgawanyo wa fedha na rasilimali nyingine za
umma; na
Kuongeza bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuiwezesha
kufanya kazi zake kwa ufanisi;
D: UFAFANUZI WA BAADHI YA HOJA
7. Mheshimiwa Spika, zipo hoja zilizotolewa na Kamati ya Bajeti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kurudiwa na Waheshimiwa Wabunge
wengi, ambazo baadhi yake napenda kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo:
Hoja Na. 1: Pendekezo la kuongeza Tozo ya shilingi 50 kwenye
mafuta kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa maji na kukamilisha
ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, hili ni pendekezo lenye lengo zuri na Serikali
inalipokea. Hata hivyo, ni vema kutambua kwamba kufuatia
kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, gharama ya
mafuta yote yaliyoagizwa kutoka nje imepungua (kwa takriban
20%) na kuchangia kushuka kwa mfumuko wa bei (sasa umefikia
5.2%). Mwenendo huu hakika umeleta ahueni kwa wananchi wetu
wengi. Hivyo, kwa sasa Serikali imeamua kutoongeza tozo kwenye
mafuta ili wananchi waendelee kunufaika na unafuu huo wa bei ya
mafuta. Ni dhahiri kuwa ongezeko la tozo katika mafuta ya petroli
na dizeli litasabisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini jambo
-
7
ambalo litaongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji wa chakula na bidhaa kama vifaa vya ujenzi na
huduma nyingine.
Aidha, wataalam wa uchumi wanashauri kuwa kipindi kama hiki
cha uwepo wa bei ndogo ya mafuta ni fursa nzuri kwa nchi
kuwekeza, hususan katika ujenzi wa miundombinu, viwanda
(energy-intensive sectors) na kuendeleza ujuzi na teknolojia.
Ndiyo sababu Serikali inaona kuwa ni busara Zaidi badala ya
kuongeza tozo kwenye mafuta, tujielekeze kuongeza bajeti ya
kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji, nishati
na elimu sambamba na kutumia fedha zilizopangwa kwa ufanisi
Zaidi.
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa kuboresha
huduma ya maji nchini, ambayo ni ahadi ya muhimu katika Ilani
ya CCM, bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji kwa mwaka wa
fedha 2016/17 fedha za ndani zimeongezwa kwa asilimia 85
kutoka shilingi bilioni 373.01 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni
690.16 mwaka ujao wa fedha 2016/17. Kufuatia jitihada kubwa
zinazoendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali
itahakikisha fedha hizi zinapatikana na kutolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maji vijijini kama ilivyokusudiwa. Aidha,
kwa upande wa haja ya kukamilisha ujenzi wa zahanati vijijini na
vituo vya afya katika kata, Wizara ya afya inajipanga kufanya
kwanza tathmini ya majengo hayo katika mwaka 2016/17 kwa ajili
ya utekelezaji 2017/18.
-
8
Hoja Na. 2: Pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi ya Mapato
kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kodi ya
mapato hutozwa kwenye vyanzo vyote vya mapato (global
income);
Kiinua mgongo ni chanzo kimojawapo cha mapato
kinachotambuliwa na Sheria na hutozwa kodi;
Kupitia Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Mapato, kiinua mgongo
kinacholipwa kwa wabunge wakati wanamaliza muhula wa miaka
mitano kimesamehewa kodi;
Msamaha huu hauzingatii kanuni ya usawa ya utozwaji kodi, kwani
watu wengine wote wanaopata malipo ya kiinua mgongo, iwe
katika sekta binafsi au utumishi wa umma, hutozwa kodi katika
mapato hayo. Kwa hiyo, hatua hii imechukuliwa ili kujenga misingi
ya usawa na haki katika ulipaji wa kodi; na
Lengo la kufanya marekebisho hayo sasa ni kwa ajili ya kuweka
utaratibu wa kisheria ambao utatumika kukokotoa stahili za
Mbunge endapo ukomo wa Mbunge yeyote utatokea katika kipindi
cha kuanzia Julai, 2016 na kuendelea. Aidha, mabadiliko haya
-
9
yanafanyika sasa ili kuzingatia msingi wa utozaji kodi ambao
inataka kodi iwe inatabirika (predictability principle).
Mheshimiwa Spika, Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba
siku nilipowasilisha pendekezo hili kwa Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
aliridhia mara moja na kusisitiza kwamba kulipa kodi ni wajibu wa
Watanzania wote ili tujenge nchi yetu. Na kwa kuwa kiongozi
lazima aongoze kwa mfano alielekeza kuwa yeye ni Mbunge wa
Tanzania nzima na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi stahiki
kwenye mafao yake ya kustaafu!
Hivyo, napenda kufafanua kwamba marekebisho niliyowasilisha
mbele ya Bunge lako Tukufu tarehe 8 Juni 2016 katika hotuba
yangu ya Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2016/17 maana yake ni kuwa
kiinua mgongo cha viongozi wote wa kisiasa waliotajwa
kusamehewa kodi chini ya Sheria ya Mafao ya Viongozi wa kisiasa
(The Political Service Retirement Benefits Act 1995) sasa kitakatwa
kodi! Hivyo, kiinua mgongo cha Mhe. Samia Suluhu Hassan
Makamu wa Rais, kitakatwa kodi! Mhe. Kassim M. Majaliwa, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa
Ruangwa naye atakatwa kodi! Vivyo hivyo, Mhe. Spika na Naibu
Spika watakatwa kodi! Aidha, Mawaziri (wakianza na Waziri wa
Fedha) na Naibu Mawaziri wote sisi ni wabunge, hivyo kiinua
mgongo chetu kitakatwa kodi! Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kadhalika kiinua mgongo chao kitakatwa kodi!! Mabadiliko haya ni
-
10
kwa mujibu wa kifungu 10(3) cha Sheria ya Kodi ya Mapato
ambacho kimeweka sharti la kutotambua misamaha mingine
yoyote ya kodi ya mapato ambayo haijatolewa kwa mujibu wa
sheria hii.
Hoja Na.3: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO) ametengewa fedha
kidogo sana kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Hivyo,
bajeti ya ofisi hiyo iongezwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Ukomo wa bajeti ya matumizi mengineyo (OC) uliotengwa kwa
mafungu mbalimbali umezingatia maamuzi na mkakati wa Serikali
wa kupunguza matumizi ya kawaida na kuelekeza fedha nyingi
katika bajeti ya miradi ya maendeleo;
Katika kufikia ukomo wa matumizi mengineyo kwa Serikali nzima
(Wizara, Idara, Taasisi za Kiserikali, Mikoa na Halmashauri)
uchambuzi wa kina ulifanyika kubaini mahitaji ya fedha ambayo
siyo ya lazima kwa wakati huu na hivyo hayawezi kuathiri utendaji
wa taasisi husika. Miongoni mwa mahitaji yaliyopunguzwa ni:
gharama za kumbi za mikutano, mafunzo na safari nje zisizo za
lazima, maadhimisho na sherehe, posho na kudhibiti matumizi ya
magari kwa mafungu yote. Aidha Serikali iliangalia miradi ambayo
inaweza kutekelezwa kwa awamu;
-
11
Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na majukumu ya msingi
ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, kama ilivyo kwa taasisi nyingine
nyeti, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, mihimili mingine ya
Dola na uwezo wa kukabiliana na dharura. Hivyo, endapo
kutajitokeza mahitaji ya lazima ambayo yatakwama kutekelezwa
na ofisi ya CAG kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itahakikisha
mahitaji hayo yanazingatiwa wakati wa mapitio ya utekelezaji wa
bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka.
Hoja Na.4: Ushuru wa bidhaa kutozwa kwenye ada ya miamala ya
uhawilishaji wa fedha utaathiri mtumiaji wa mwisho na si
makampuni ya simu
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa katika miamala ya fedha
(Excise Duty on Money Transfer) hautakatwa kwenye fedha
zinazotumwa au kupokelewa, bali katika ada inayotozwa na benki
au kampuni ya simu;
Kwa sasa Sheria inatamka kwamba ada hii itatozwa katika kutuma
fedha tu. Hata hivyo, baadhi ya kampuni za simu na benki
zimekuwa zikitumia mwanya wa Sheria hiyo kupunguza wigo wa
kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea tu;
Kwa mapendekezo haya, ushuru wa bidhaa utatozwa kwenye ada
ya miamala ya uhawilishaji fedha ama wakati wa kutuma au
kupokea fedha au vyote viwili kadri itakavyotozwa; na
-
12
Mantiki yake ni kuwa, ushuru huu utalipwa na benki au kampuni
ya simu na siyo mtumaji au mpokeaji. Hata hivyo, Mamlaka ya
Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), itawajibika kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na
uhalisia wa huduma itolewayo na kufanya ukaguzi (cyber forensic
audit) wa miamala ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo
ili yasihamishie mzigo kwa mtumiaji wa mwisho.
Hoja Na. 5 Tathmini ya hali ya umasikini kimkoa
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Viashiria vya kupima hali ya umaskini nchini hupatikana kwa
kutumia Utafiti wa Mapato na Matumizi katika kaya ambao
hufanyika kila baada ya miaka mitano hapa Nchini. Utafiti wa
mwisho ulifanyika mwaka 2011/12.
Mheshimiwa Spika,
i. Hali ya umaskini katika kaya hupimwa kwa kuangalia mahitaji ya msingi (basic needs) kwa kila mwanakaya ukijumuisha mahitaji ya chakula yenye kiwango cha kilo kalori 2,200 kwa mlo kwa siku na hii ni kutokana na Kipimo cha Shirika la Afya Duniani - WHO. Mbinu hii inaonesha kiwango cha chini kabisa cha kipato anachohitaji mtu kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbali mbali ya msingi.
ii. Kiwango cha umaskini wa chakula hupimwa kwa gharama ya
kiwango cha chini cha aina mbali mbali ya vyakula vyenye
-
13
kufikia kiwango cha kilo kalori 2,200 kinachohitajika kwa mlo wa mtu maskini kwa siku katika mwezi. Kwa utafiti huu gharama ya kununulia chakula cha mtu mmoja kwa siku bila kujali eneo alilotoka ni Shillingi 858. Kiwango cha umaskini wa chakula ni gharama ya matumizi yote ya kaya ambayo yapo chini ya gharama wanayohitaji ili kukidhi mahitaji ya chakula yaani (Food Poverty Line). Na kwa umaskini wa mahitaji ya msingi ambao huhusisha chakula ni Tshs. 1,216 (Basis Needs poverty line) kwa siku kwa kila mtu mmoja tu.
Mheshimiwa Spika, utafiti wa kukusanya taarifa za kupima hali
ya umasikini nchini hukusanya matumizi na mapato ya kaya.
Taarifa zinazokusanywa ni umri, hali ya ndoa, elimu na afya,
manunuzi na matumizi ya kaya, umiliki wa bidhaa za matumizi na
mali, makazi na vifaa vya ujenzi, upatikanaji wa huduma na vifaa,
shughuli za ajira na kiuchumi, utalii na shughuli za kilimo.
Uchambuzi wa kina wa hali ya umaskini katika ngazi ya mkoa na
wilaya yaani (Poverty Mapping) uliongozwa na wataalam wa
REPOA na ulibainisha kuwa: Region Watu Wanaoishi Chini Mstari
wa Umaskin 2000/01 (%)
Watu Wanaoishi Chini
Mstari wa Umaskini
2011/12 (%)
Mwanza 43 35
Kagera 29 39
Kigoma 38 49
Singida 49 38
Geita Included in Mwanza 44
-
14
Mheshimiwa Spika, sababu zinazoeleza kwanini kiwango cha
umasikini katika Mikoa kama Mwanza, Kigoma, Singida, Geita, na
Kagera ni kikubwa zaidi ukilinganisha na mikoa ya Lindi na Mtwara
ni nyingi.
Umasikini wa kipato ni mkubwa zaidi pale ambapo wananchi
wengi zaidi wanaishi vijijini (33.3%) ikilinganishwa na mijini
(21.7%). Mfano: Mwaka 2000/01 umaskini wa Kipato mkoa wa
Mwanza ulikuwa 48%. Baada ya kugawanywa na kutolewa Wilaya
ya Geita ambayo ilikuwa inaongoza kwa Umaskini wa Kipato
62.3% na kuwa Mkoa mpya wa Geita kiwango cha umasikini Mkoa
wa Mwanza kinaonekana kupungua kutoka 43% (2000/01) hadi
35% (2011/12). Aidha, kwa mkoa wa Geita, sababu mojawapo ya
umasikini wa kipato (44%) ni kiwango kikubwa cha uzazi (wastani
wa watoto 7 kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa). Hivyo,
shughuli za kiuchumi zinaelemewa na ongezeko kubwa la idadi ya
watu (population explosion).
Aidha, wilaya za Kwimba na Sengerema umaskini wa kipato ni
39% na Misungwi 50% mwaka 2011/12. Wilaya za Mijini ambazo
ni Nyamagana na Ilemela umaskini wa kipato ni 17% na 15%.
Hivyo wananchi wengi vijijini kutegemea kilimo, ufugaji na uvuvi
usio na tija, havitoshi kupunguza umaskini wa kipato kwa kasi
inayotakiwa. Hivyo, zitahitajika jitihada za makusudi kuongeza tija
katika shughuli za msingi za kiuchumi vijijini.
-
15
Mheshimiwa Spika, umasikini katika mkoa wa Kigoma
unachangiwa na miundombinu hafifu ya usafirishaji ambao
unapunguza fursa za masoko. Pia Kigoma inabeba mzigo mkubwa
wa wakimbizi na hivyo kusababisha ziada inayozalishwa kutumika
zaidi kulisha wakimbizi na kupunguza ustawi wa Kaya katika mkoa
husika.
Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara umaskini huenda umepungua
kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara na uchumi
kufuatia ugunduzi wa gesi asilia na ujenzi wa Kiwanda cha Saruji.
Aidha, ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka kwa mikoa hii ni chini
ya wastani wa Taifa wa 2.7%. maana yake ni kuwa
kinachozalishwa kinatumika katika kustawisha uchumi katika kaya
zao.
Mheshimiwa Spika, kwa mkoa wa Pwani, Wakazi wake wengi
wanafanyia shughuli zao za kuongezea kipato katika Jiji la Dar es
Salaam ambalo lina fursa nyingi Kiuchumi. Kadhalika, Pwani
imepata fursa nyingi za Wakazi wake kujiongezea kipato chake
kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya barabara, maji na
umeme ambazo ni vichecheo vya kuinua kipato cha Mwananchi
mmoja mmoja.
-
16
Hoja Na. 6 Wizara ya Fedha na Mipango iangalie upya kuondoa
misamaha ya kodi kwenye taasisi za dini kwa kuwa zinatoa
huduma za kijamii kama shule, hospitali, n.k.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja
na waheshimiwa wabunge, utaratibu niliopendekeza kwa taasisi za
kidini kulazimika kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazonunua
au kuagiza nje na kodi hiyo kurejeshwa baada ya ukaguzi
kufanyika na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa
malengo yaliyokusudiwa umeonekana unaweza kukwamisha au
kuchelewesha utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi za
kidini na kusababisha athari katika upatikanaji wa huduma
muhimu kwa jamii. Kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi
mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu na afya,
napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza katika hotuba ya bajeti
na badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali za
udhibiti wa misamaha ya kodi kama ifuatavyo:
i. Taasisi za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka wa kalenda, na kuthibitisha kama vifaa vilivyopewa msamaha mwaka uliopita vilitumika kama sheria inavyotaka;
ii. Kuwasilisha majina ya watu walioidhinishwa na Shirika au
Taasisi kuandika barua za kuomba msamaha wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu.
-
17
Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo na zimetumika kutekeleza miradi iliyotarajiwa. Pia wanapaswa kuandika barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha waliomteua kutoa mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje;
iii. Kila wanapoomba msamaha wanapaswa kupata barua kutoka
kwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa na Mkuu wa Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo ili kuthibitisha kuwepo kwa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa msamaha;
iv. Magari yanayoagizwa kwa msamaha yawe na namba na rangi
maalum za utambuzi mfano: TEV 222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake; na
v. Taasisi ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa
kodi itafutiwa usajili na Serikali.
Mheshimiwa Spika, utaratibu na hatua mbalimbali za udhibiti
wa misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara, watumishi wa umma
na taasisi zisizo za kiserikali utatangazwa katika gazeti la Serikali
na kupitia vyombo vya habari.
-
18
Hoja Na.7: Uwezo wa TRA kukusanya Kodi ya Majengo
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika,
TRA ni mamlaka ambayo ina uzoefu wa kutosha katika ukusanyaji
kodi za Serikali na ina vituo vya ukusanyaji kodi katika Wilaya na
Mikoa yote Tanzania;
TRA inatekeleza majukumu yake kupitia sheria mbalimbali ambazo
zinarahisisha ukusanyaji wa kodi kwa kupitia utaratibu wa kisasa
wa Benki pamoja na njia za kielektroniki. Aidha, Kamishna Mkuu
anaruhusiwa kama ataona inafaa, kuazima baadhi ya watumishi
wenye uzoefu wa utozaji kodi ya majengo toka maeneo mengine
ya serikali ikiwemo serikali za mitaa kwa lengo la kujenga
ushirikiano na kuongeza ufanisi; na
Kwa kutumia uzoefu na mifumo iliyopo ya TRA, ni wazi kuwa kodi
ya majengo itakusanywa kwa ufanisi mkubwa na kwa uwazi zaidi,
tofauti na sasa ambapo wananchi wengi hawalipi kodi hiyo.
Kuhusu Viwango vya Kodi ya Majengo
Waziri wa Fedha na Mipango ataweka viwango vya kodi ya
majengo baada ya kushauriana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI ili kuweka uwazi na kujumuisha maoni ya wadau wote
muhimu zikiwemo Halmashauri husika; na
Kodi ya majengo itatozwa kwa kuzingatia mazingira ya maeneo
husika ambapo TRA itakuwa na jukumu la kutoza, kukusanya na
-
19
kuwasilisha makusanyo hayo kwenye akaunti maalumu kwa
manufaa ya serikali za mitaa.
Mapato kutokana na kodi ya majengo yataingizwa katika mfuko
mkuu. Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na TAMISEMI
watashauriana kuhusu mgawanyo wa fedha hizo kwa kuzingatia
bajeti za Halmashauri husika.
Hoja Na.8: Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika
Huduma za Utalii
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Kabla ya hotuba ya bajeti ya 2016/17 nchi zote wanachama wa
Jumuiya Afrika Mashariki zilikuwa zinatoza VAT kwenye huduma
ya utalii isipokuwa Tanzania ambayo imependekeza kutoza katika
bajeti yake ya mwaka 2016/17;
Mwaka 2014 Serikali kupitia Bunge ilitunga sheria ya VAT. Sheria
hii ilitungwa ili kutatua upungufu uliokuwepo katika sheria ya VAT
ya mwaka 1997;
Msamaha wa VAT kwenye huduma za utalii ulifutwa mwaka 2014
baada ya kukubaliana na wadau ambao waliiomba Serikali mwaka
moja toka Novemba 2014 ili kulinda mikataba iliyoingiwa kabla
ya kutunga sheria ya VAT ya mwaka 2014;
-
20
Idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama kwa kipindi
2011 hadi 2014 katika nchi za Tanzania, Kenya na Afrika Kusini
zinaonyesha kwamba Tanzania licha ya kutotoza VAT kwenye
huduma hii bado imetembelewa na watalii wachache kuliko nchi
hizo kama ifuatavyo:
Serikali inapendekeza kutoza VAT kwenye huduma za utalii kwa
sababu VAT sio kigezo kikubwa kinachoangaliwa na Mtalii wakati
anafanya maamuzi kufanya utalii. Baadhi ya vigezo muhimu
vinavyoangaliwa ni vivutio, usalama, huduma kwa watalii na hali
ya usafiri.
Hoja Na.9: Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo la
watoa huduma kutoza bei kwa kutumia fedha za kigeni kama Dola
ambalo linapelekea kushuka kwa thamani ya shilingi?
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Dollarization ni matumizi ya sarafu ya kigeni katika nchi moja
sambamba na sarafu ya nchi hiyo;
Mwaka
Idadi ya Watalii
Tanzania Hakuna VAT
Kenya Kuna VAT
Afrika Kusini Kuna VAT
2011 867,994 1,750,000 8,339,000
2012 1,077,058 1,619,000 9,188,000
2013 1,095,884 1,434,000 9,537,000
2014 1,140,156 1,261,000 9,549,000
-
21
Matumizi makubwa ya fedha za kigeni katika uchumi
husababishwa na mambo kadhaa yakiwemo vita vya muda mrefu
katika nchi, kuongezeka kwa mfumuko wa bei na kuporomoka kwa
thamani ya sarafu ya nchi husika ikilinganishwa na sarafu ya
kigeni. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, kushuka kwa
thamani ya shilingi yetu kulitokana na kuimarika kwa Dola ya
Kimarekani, kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za kigeni kwa
ajili ya bajeti ya serikali pamoja na mapato madogo ya fedha za
kigeni yasiyokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje;
Kwa ujumla, mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa
bidhaa na huduma nje ya nchi hayawiani na uuzaji wa bidhaa na
huduma nje. Kwa mfano katika mwaka 2015, thamani ya mauzo
ya bidhaa na huduma nje ilikuwa Dola za Kimarekani milioni
9,450.0 ikilinganishwa na Dola milioni 12,528.2 zilizotumika
kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Hali hii inasababisha
kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na
huduma;
Mwenendo wa thamani ya Shilingi umekuwa ni chanzo kikuu kwa
wafanya biashara nchini kupanga bei za bidhaa na huduma zao
kwa fedha za kigeni. Hivyo basi, namna nzuri na endelevu ya
kupunguza au kuondoa matumizi ya fedha za kigeni katika
matangazo ya bei au malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali
kwenye soko la ndani ni kuimarisha thamani ya Shilingi yetu na
kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei. Hali hii itawezekana kwa
kuendelea kutekeleza sera madhubuti ya fedha na kuhakikisha
-
22
kunakuwa na ongezeko la uzalishaji wa chakula pamoja na
kuboresha usambazaji wa chakula nchini. Hii inajumuisha pia
kuboresha miundombinu itakayowezesha kilimo cha umwagiliaji na
kusafirisha chakula kirahisi kutoka sehemu zenye ziada kwenda
sehemu zenye upungufu;
Aidha, kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mauzo nchi za nje
kutapunguza nakisi katika urari wa biashara ya bidhaa na huduma
nchi za nje na hivyo kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa thamani
ya Shilingi. Hivyo basi, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni
(dollarization) ni suala la muda wa kati linalohitaji kuimarisha sera
madhubuti za uchumi jumla ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka
mifumo thabiti itakayoleta ongezeko la haraka la uzalishaji wenye
tija na hivyo kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje;
Si nia ya Serikali kurejesha sera ya udhibiti wa umiliki wa fedha za
kigeni (administrative de-dollarisation) kwani madhara yake ni
makubwa na baadhi ya nchi zilishajaribu zikashindwa na hivyo
kurudisha sera ya soko huria. Udhibiti wa umiliki wa fedha za
kigeni utaleta ushawishi kwa watanzania kutunza fedha za kigeni
katika mabenki ya nje kinyume na sheria (capital flight). Hii
itasababisha upungufu mkubwa wa fedha za kigeni na hivyo
kufanya nchi kushindwa kulipia mahitaji yake kutoka nje. Pia, hali
hii itasababisha kushamiri kwa soko lisilo rasmi (parallel market) la
fedha za kigeni cf. IMF (2015) Dollarization in SSA: Experience
and Lessons;
-
23
Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu kuhakikisha kwamba
matumizi ya fedha za kigeni katika uchumi wetu yanafanyika kwa
kufuata utaratibu uliowekwa kisheria. Sheria ya Benki Kuu ya
mwaka 2006, sehemu ya tatu, kipengele cha 26, inatamka wazi
kuwa shilingi ya Tanzania itakubalika na kutumika kama fedha
halali kwa malipo (legal tender) ndani ya nchi yetu. Hii
inamaanisha kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo
haiwezi kukataliwa na mtu yeyote kwa malipo halali ndani ya nchi
yetu. Hivyo, ni kosa kukataa kupokea shilingi ya Tanzania kwa
malipo halali nchini; na
Vile vile, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992
(The Foreign Exchange Act, 1992) inaruhusu mtu yeyote kupokea,
kumiliki na kutumia fedha za kigeni kwa shughuli zake za
kiuchumi. Vile vile, Sheria hiyo inatamka kwamba mtu yeyote
anaruhusiwa kuwa na akaunti ya fedha za kigeni katika benki
iliyoruhusiwa na Benki Kuu kwa ajili hiyo.
Hoja Na.10: Serikali ipunguze kukopa katika mabenki ya ndani ili
kutoa fursa kwa sekta binafsi kupata mikopo.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Nakisi ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni asilimia 4.5 ya Pato la
Taifa ikilinganishwa na asimilia 3.7 mwaka 2013/14, asilimia 3.6
mwaka 2014/15 na asilimia 4.2 mwaka 2015/16. Kiwango cha
nakisi ya bajeti kimeongezeka kwa asilimia 0.3 ya Pato la Taifa
-
24
ikilinganishwa na mwaka 2015/16. Ongezeko hilo limetokana na
nia nzuri ya Serikali ya kutekeleza kwa dhati Mpango wa pili wa
maendeleo wa miaka mitano;
Kigezo kimojawapo cha uchumi mpana katika kuanzishwa kwa
Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni kuwa na
kiwango cha nakisi ya bajeti kwa Pato la Taifa cha asilimia 3 pindi
ifikapo 2021/22. Katika kutekeleza hili, Serikali imepanga
kupunguza kiwango cha nakisi hatua kwa hatua bila kuathiri
utekelezaji wa bajeti;
Katika mwaka 2016/17, Serikali imepanga kuziba nakisi ya bajeti
ya asilimia 4.5 ya Pato la Taifa kwa kukopa kutoka katika vyanzo
vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, asilimia 3.0 ya Pato la Taifa
itakopwa kutoka vyanzo vya nje na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa
itakopwa kutoka katika vyanzo vya ndani. Ukopaji huo hufanyika
kwa kuuza hatifungani kwenye soko la ndani la fedha badala ya
kukopa moja kwa moja kwenye benki za biashara; na
Kwa maana hiyo, kiasi kitakachokopwa kutoka soko la ndani
kinazingatia ukomo wa ukopaji ambao hauathiri utoaji wa mikopo
kwa sekta binafsi ambapo mikopo kwa sekta binafsi imekuwa
ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 kwa mwaka. Ongezeko hili
linawiana na lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kama
ilivyoainishwa katika Tamko la Sera ya Fedha. Aidha, kiwango cha
mikopo ambayo imekuwa inayotolewa na benki za biashara kwa
sekta binafsi ni zaidi ya asilimia 80 ya mikopo yote, wakati mikopo
-
25
inayotolewa na benki za biashara kwa Serikali ni chini ya 2%
Hoja Na. 11: Kuondolewa kwa misamaha ya kodi katika maduka
na migahawa ya vyombo vya ulinzi na usalama kunaondoa
motisha katika taasisi hizo. Ikiwa msamaha wa kodi utafutwa,
bidhaa na vifaa vilivyopo katika bohari za majeshi yetu
zitapelekwa wapi? Na zipo kiasi gani?
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Uamuzi wa Serikali wa kuwapa motisha watumishi wa vyombo vya
ulinzi na usalama bado upo palepale. Mapendekezo ya kuondoa
msamaha wa kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya
ulinzi na usalama ni kutokana na misamaha hiyo kutumika vibaya.
Ili kuondoa kasoro hiyo, Serikali imeamua kuweka utaratibu wa
kuwalipa posho watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili
wanufaike moja kwa moja kama walengwa. Kiasi cha posho
atakayolipwa askari kitakokotolewa baada ya mashauriano na
vyombo husika.
Serikali inakamilisha utaratibu wa bidhaa ambazo zimesamehewa
kodi katika maduka yote ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Utaratibu huo utakapokamilika wahusika watajulishwa.
-
26
Hoja Na.12: Kodi kwenye “transit goods” ni kinyume na taratibu
kwa kuwa kodi hiyo hulipwa na mlaji. Hii itasababisha waagizaji
wa mizigo kuhamia bandari nyingine za Beira na Mombasa.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Sheria ya VAT ya Mwaka 2014 imeweka viwango viwili vya kutoza
kodi ambavyo ni asilimia 18 kwa bidhaa na huduma zinazotumika
hapa nchini na asilimia 0 pale bidhaa na huduma inaposafirishwa
nje ya nchi (Exported);
Huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa kwenda nchi
za jirani kupitia Tanzania siyo “exports” bali zinatolewa na
kutumiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
maana kodi ya ongezeko la thamani (VAT) haitozwi kwenye transit
goods bali hutozwa kwenye huduma ambapo mtumiaji na mtoaji
wako Tanzania. Huduma hizi zinaweza kutolewa mahali popote
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na siyo bandarini tu,
na hivyo ni sahihi kabisa huduma hizi kutozwa asilimia 18;
Utafiti uliofanywa kubaini kama kutoza kodi ya VAT huduma hizi
kunaathiri biashara kwenye bandari umeonesha kwamba katika
kipindi cha Julai, 2015 hadi April, 2016 mizigo iliyopita kwenye
bandari ya Dar es Salaam imepungua kwa asilimia 15 ukilinganisha
na mizigo iliyopita katika Mwaka wa Fedha 2014/15 katika kipindi
kama hicho. Katika Bandari ya Mombasa ambapo huduma hizi
zimesamehewa kodi ya VAT mizigo imepungua kwa asilimia 25
-
27
katika kipindi hicho. Kwa ujumla biashara ulimwenguni kote
imeshuka katika kipindi hiki, na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi
jumla; na
Kwa misingi hiyo si sahihi kusema kwamba kutoza kodi ya VAT
kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa
kwenda nchi jirani ndicho chanzo cha kushuka kwa biashara katika
bandari zetu.
Hoja Na.13: Serikali iangalie upya mfumo wa “Single Customs
Territory” unaodaiwa kusababisha kupungua kwa mapato ya
bandari kutokana na baadhi ya nchi jirani kuepuka kutumia
bandari ya Dar es Salaam.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Mfumo wa “Single Customs Territory (SCT)” ulianza kutumiwa na
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mfumo huu
ulionesha manufaa makubwa katika kuwezesha biashara na
kudhibiti uvujaji wa mapato baina ya nchi husika. Mfumo huu
huruhusu wafanyabiashara wanaotumia bandari zetu kupitisha
mizigo kwenda nchi jirani kulipa kodi kwenye nchi zao kwanza na
pindi mzigo huo unapowasili bandarini na kujiridhisha kuwa kodi
husika zimelipwa, mzigo huo huruhusiwa na hivyo kuepusha
uwezekano wa kuingizwa nchini bila kulipiwa kodi. Utaratibu huu
pia hurahisisha uondoshaji wa kadhia forodhani. Mfano mzuri wa
mafanikio ya mfumo huu ni mizigo inayokwenda Rwanda kwani
-
28
imeongezeka kwa asilimia 16 kwa kipindi cha kuanzia Julai 2015
hadi Aprili 2016 ukilinganisha na kipindi kama hicho katika mwaka
wa fedha 2014/15. Pia muda wakusafirisha mzigo kutoka muda wa
kuingia na kutoka (from entry to exit) umepungua;
Mfumo huu wa SCT kwa mizigo inayokwenda Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeanza kutumika kufuatia
makubaliano kati ya serikali za nchi hizi mbili. Lengo lake ni
kuharakisha biashara kwa kupunguza muda wa kutoa na
kusafirisha mizigo kwenda DRC na kudhibiti mapato kwa nchi zote
mbili. Hivyo kushuka kwa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani
hakujasababishwa na SCT;
Kwa upande mwingine, dunia imeshuhudia kupungua kwa
biashara ya kimataifa katika kipindi hiki ambako kumesababishwa
na kudorora kwa uchumi wa China, kushuka kwa bei ya bidhaa
(commodities) na mafuta ikiwa pamoja na madini mbalimbali.
Hivyo, kupungua kwa mizigo inayokwenda nchi jirani na ile
inayotumika hapa nchini, hakujaiathiri Tanzania peke yake bali
hata bandari ya Mombasa mizigo ya nchi jirani yaani transit
ilipungua kwa asilimia 25 kwa kipindi cha kati ya Julai 2015 hadi
Machi 2016 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014/15.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na TRA/Serikali umebainisha
sababu za muda mfupi na muda mrefu zilizosababisha kupungua
kwa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na
mizigo inayokwenda nchi jirani na ile kwa ajili ya matumizi ya
ndani ya nchi (imports);
-
29
Sababu za muda mfupi ni pamoja na:- Maandalizi ya Uchaguzi
Mkuu kwenye Nchi za kanda yetu kama vile Tanzania, Uganda,
Burundi, machafuko nchini Burundi na Sudan Kusini, kushuka kwa
bei ya shaba katika soko la dunia kuliathiri uchumi wa Zambia na
hivyo kushuhudia kupungua kwa mizigo ya kwenda na kutoka
Zambia, na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na nchi ya
Msumbiji na Afrika kusini kwa mfano Msumbiji imejenga reli ya
standard gauge na kuboresha bandari na hivyo kuifanya bandari
kuwa na miundombinu bora ukilinganisha na bandari yetu. Hali hii
imeifanya bandari ya Beira kupendelewa zaidi na nchi jirani;
Sababu za muda mrefu ni pamoja na:- Ufanisi mdogo wa bandari
ya Dar es Salaam ukilinganisha na bandari zingine, miundombinu
hafifu ya kusafirisha mizigo hususan kwa njia ya reli na hivyo
kufanya njia pekee ya uhakika kusafirisha mizigo kuwa ni barabara
ambayo ni ghali zaidi ukilinganisha na reli; na
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kikamilifu kuondokana na
changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za
bandari na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni
pamoja na kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.
-
30
Hoja Na.14: Tamko la kufuta retention kwenye Taasisi za
kimkakati kama TPDC, Serikali ikishindwa kupeleka fedha kwa
wakati, itapoteza mapato mengi kwa sababu watashindwa
kusimamia kwa ufanisi mapato kutoka kwa wawekezaji.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu wa kubakiza sehemu ya mapato (Retention) ulikuwa na
lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli kwa
baadhi ya Wizara na Taasisi. Katika baadhi ya Wizara na Taasisi
hizo ufanisi wa ukusanyaji maduhuli umeongezeka;
Hata hivyo, kumejitokeza dosari katika utekelezaji wa utaratibu
huo, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa yasiyowiana na
majukumu ya msingi na kutochangia inavyostahili katika mfuko
mkuu wa Serikali; na
Ili kurekebisha dosari na kuhakikisha kuwa Taasisi husika zinapata
fedha kwa wakati, Serikali imeelekeza Taasisi hizo kuwasilisha
mpango kazi na mtiririko wa mahitaji ya fedha (action plan and
cash flow), vigezo ambavyo vitazingatiwa katika utoaji wa fedha
-
31
Hoja Na. 15 Ushuru wa Forodha kwenye Sukari ya Viwandani
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Katika ukurasa wa 71 kwenye kitabu cha Hotuba ya Bajeti
2016/17 niliyoisoma hapa Bungeni nilieleza kuwa, waagizaji wa
sukari ya viwandani watatakiwa kulipa ushuru wa asilimia 15
kwenye sukari wanayoagiza badala ya asilimia 10 wanayolipa sasa
katika mwaka wa fedha 2015/16. Hilo lililenga kutekeleza
maamuzi ya Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya
fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kupunguza msamaha
kwenye sukari ya viwanda hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia 25
kama ifuatavyo: mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa asilimia 15,
2017/18 kiwango kitakuwa cha asilimia 20 na 2018/19 kiwango
kitakuwa asilimia 25.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa maamuzi ya kuanza kutoza
ushuru wa forodha wa asilimia 15 kwenye sukari inayoingizwa
nchini kwa matumizi ya viwanda ulikuwa ni uamuzi wa pamoja wa
mawaziri wenye dhamana ya masuala ya fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ni Tanzania pekee ndiyo ingetekeleza
maamuzi haya katika mwaka wa fedha 2016/17. Nchi za
Burundi, Kenya na Uganda zimeomba muda wa kujiandaa ili
waweze kuanza kutekeleza hatua hii katika mwaka wa fedha
2017/18. Rwanda wanatumia mfumo tofauti ambapo sukari yote
hutozwa asilimia 25 badala ya kutumia ushuru wa forodha wa
asilimia 100 au Dola za Marekeni 460 kwa tani moja kwa
-
32
kutegemea kiwango kipi ni kikubwa zaidi. Sababu ya nchi hizi
kutotumia kiwango hicho cha ushuru wa forodha ni ukweli kuwa
bidhaa hizi hazizalishwi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, ili kujiandaa kwa utekelezaji wa hatua hii, Kenya imepewa
unafuu wa ushuru wa forodha kwa kuruhusiwa kuingiza sukari
ghafi kwa kutumia kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 100
au Dola za Marekani 460 kwa tani kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Baada ya kupokea maoni ya watengenezaji wa vinywaji pamoja na
kutafakari juu ya umuhimu wa bidhaa hiyo ambayo hutumika
kama malighafi ya viwanda vyetu, Serikali imeamua kusitisha
utekelezaji wa hatua hii hadi mwaka wa fedha 2017/18 kama
ilivyo kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hata
hivyo, Serikali itaendelea kuwataka watumiaji wa sukari hii
kuendelea kulipia kodi ya asilimia 25 kwanza na kurejeshewa
asilimia 15 baada ya kuthibitisha uhalali wa matumizi.
Hoja Na.16: Wizara ya Fedha na Mipango ijihadhari na madalali
wa mikopo (transaction agents) maana wataongeza gharama za
mikopo.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Ukopaji wa fedha unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo,
Dhamana na Misaada Sura 134. Sheria hiyo imetoa Mamlaka kwa
Waziri wa Fedha na Mipango kukopa mikopo ya ndani na nje kwa
niaba ya Serikali. Kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa katika
sheria hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango hujadiliana moja kwa
-
33
moja na wakopeshaji ambao wanaweza kuwa ni Nchi (Bilateral
Creditor), Benki moja moja au kundi la mabenki;
Hata hivyo, kutokana na muundo (structure) wa soko la fedha la
ndani au la kimataifa, wakati mwingine Waziri wa Fedha anaweza
akateua taasisi nyingine kumsaidia ili kurahisisha upatikanaji wa
fedha kutoka soko la fedha husika. Mathalan, kwa sasa Benki Kuu
ya Tanzania inatumika kama wakala (Agent) wa Serikali katika
kuuza Hati Fungani na Dhamana za Serikali na kuiwezesha Serikali
kupata Fedha kutoka Soko la Ndani;
Kwa upande wa soko la fedha la kimataifa, mikopo mikubwa
huchangiwa na taasisi nyingi za fedha yakiwemo mabenki na
wakopeshaji wengine. Taasisi hizo huteua benki au taasisi moja
miongoni mwao kuwa Wakala yaani Agent/lead arranger au lead
manager kuwasikilisha mabenki hayo katika majadiliano na
mkopaji. Huu ni utaratibu wa kawaida kwenye masoko ya fedha
ya kimataifa na hufanya hivyo ili kurahisisha majadiliano na
upatikanaji wa fedha kwa wakati;
Sifa za Wakala huyo anayechaguliwa na mabenki au wawekezaji
kwenye soko la fedha la kimataifa lazima ni pamoja na kuwa
uwezo wa kuitangaza nchi kikamilifu katika soko la fedha la
kimataifa hivyo kuifanya nchiyo kupata fedha na kwa gharama
nafuu ya soko, kwa upande mwingine, Wakala huyo anatakiwa
awe na taarifa za kutosha za mkopaji ikiwemo hali ya uchumi,
siasa na masuala ya kijamii ya nchi husika na uwezo wa nchi hiyo
-
34
kurejesha mikopo. Aidha, mkopaji lazima ajiridhishe na kukubali
kutumia Wakala huyo; na
Utaratibu huu hutoa uhakika kwa Serikali kupata mikopo kwa
masharti yanayokubalika baina ya pande mbili zinazo husika. Kwa
mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134.
Sheria hii imeweka utaratibu maalum wa kuufuata wakati wa
kukopa. Kwa mujibu wa Sheria hii kuna Kamati Maalum ambazo
huchambua masharti ya kila mkopo na kujadiliana na wakopeshaji
na baada ya majadiliano kukamilika, Kamati hizi ndizo zinamshauri
Waziri wa Fedha na Mipango kukopa mkopo husika.
Hoja Na.17: Serikali ishirikishe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti katika maandalizi ya bajeti.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Serikali imekuwa ikiishirikisha Kamati ya Bunge ya Bajeti na
Waheshimiwa Wabunge katika hatua mbalimbali za maandalizi ya
bajeti. Ushirikishwaji huo hufanyika katika hatua zifuatazo:
Maandalizi ya Mwongozo wa Mpango na Bajeti Kamati za Kudumu
za Bunge za Kisekta; na
Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambayo hushirikishwa kikamilifu katika
kuchambua makadirio ya bajeti ya Serikali; kupitia rasimu ya
mfumo wa bajeti; kupitia hoja za kibajeti zinazoibuka kwenye
-
35
sekta mbalimbali; kushauriana na Serikali kuhusu vyanzo vipya vya
mapato.
Hata hivyo, ili kulinda kazi ya Bunge ya kuishauri na kuisimamia
Serikali ni muhimu kwamba Bunge lisijiingize katika kazi za
kiutendaji katika maandalizi ya bajeti na badala yake Bunge
lichambue na kushauri kuhusu mapendekezo ambayo tayari
yanakuwa yameridhiwa na Serikali.
F: HITIMISHO
8. Mheshimiwa Spika, tuna dhamana ya kuleta mabadiliko makubwa
katika uendeshaji wa shughuli zote za umma na matumizi ya rasilimali za
Taifa ili kuwezesha kupiga hatua kubwa ya kuiondoa nchi yetu katika
umaskini. Katika hili, kila mwananchi atambue wajibu wake wa kufanya
kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika nyanja zote na
uzalendo kwa Taifa letu.
9. Mheshimiwa Spika, nirudie tena kuzielekeza Wizara, Idara
zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia hatua za kuimarisha ukusanyaji
wa mapato; usimamizi wa matumizi ya Serikali na hatua za kupunguza
gharama; na kulipa na kuzuia ongezeko la madeni ya Serikali. Serikali ina
dhamira ya dhati kabisa ya kuchukua hatua hizo na ninaomba Watanzania
wote watambue kwamba ni lazima kujinyima, kujituma na kuvuja jasho ili
kupata maendeleo na kupunguza utegemezi. Wajibu wa kwanza wa
kuiendeleza Tanzania ni wa Watanzania wenyewe. Tuna akili za kutosha,
-
36
rasilimali nyingi na fursa tele kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na
Uchumi wa Kipato cha Kati ifikapo 2025.
10. Mheshimiwa Spika, ninawaomba tena Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hatua zinazoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano
kuhakikisha kuwa tunaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya kodi na
yasiyo ya kodi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo yenye tija kwa
manufaa ya watanzania wote.
11. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.