hotuba ya mhe. jakaya mrisho kikwete, rais wa … · 2014. 11. 12. · kati ya mwaka 2002 hadi 2006...
TRANSCRIPT
-
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA
MAADHIMISHO YA SIKU YA MWALIMU DUNIANI TAREHE 11 OKTOBA, 2006
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh. Margaret Sitta (Mb);
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Henry Shekifu (Mb);
Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Yahya Msulwa;
Waheshimiwa Viongozi wa chama na Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania;
Walimu wote, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima mliyonipa ya kunialika
kushiriki nanyi katika sherehe hizi za maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani.
Nawashukuru kwa mapokezi mazuri mliyonipa na burudani murua za kwaya na
muziki wa Boka Boma Music Band.
Nawapongeza wale wote walioshiriki kuandaa maadhimisho haya yaliyofana.
Nimefurahishwa sana na niliyoyaona kwenye mabanda ya maonyesho. Pongezi za
pekee kwa Chama cha Walimu Tanzania kwa kuendelea kuwaunganisha walimu
nchini, na ninawapongeza walimu wote kwa kuadhimisha siku yenu leo
hii. Nawaahidi ushirikiano wangu na ule wa wenzangu wote Serikalini.
-
Ndugu viongozi, ndugu wananchi;
Leo tunawapongeza walimu kwa kuadhimisha siku yao duniani. Hii ni siku
muhimu kwa walimu. Ni siku ambayo walimu duniani kote hutafakari mahali walipo
na kule waendako katika kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu. Na sisi wadau wengine
ni fursa ya kuonyesha shukrani na pongezi zetu, kama Taifa, kwa walimu wote nchini
kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulijenga na kuliendeleza Taifa letu.
Nchi yetu ni kubwa na maeneo mengi yanapishana kwa viwango vya
maendeleo, lakini Mwalimu yuko katika kila kona ya nchi hii. Walimu ndio huwafunda
na kuwalea raia na viongozi wa kesho wa taifa letu.
Vilevile, walimu ndio wanaotutengenezea viongozi katika fani mbalimbali za
taaluma na ujuzi. Walimu ndio wanaotujengea nguvu kazi ya kutumainiwa ya Taifa
letu. Walimu ndio wanaoijenga haiba ya taifa. Nakubaliana nanyi kabisa kwamba
walimu ndio chimbuko la taifa na utaifa. Miongoni mwa walimu ndio
wametoka viongozi wengi wa nchi yetu wakiwemo Wabunge na Mawaziri. Hata Rais
wetu wa kwanza Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais
wetu wa pili Mzee Ali Hassan Mwinyi walikuwa walimu.
Ni ukweli uliodhahiri kwamba, aina ya walimu tunaokuwa nao, inaamua aina
ya Taifa tunalolijenga. Kwahiyo basi, kwa Serikali na jamii yote kwa jumla, kutambua
na kuheshimu nafasi ya Mwalimu katika ujenzi na maendeleo ya Taifa letu, ni jambo
muhimu sana.
Ahadi yangu kwenu ni kwamba tutaendelea kuutambua, kuuheshimu na
kuuenzi mchango wa walimu kwa Taifa letu. Tunatambua kuwa wengi wenu
mnafanya kazi katika mazingira magumu. Serikali haitachoka kuzifanyia kazi kero za
walimu na kutafuta njia mbalimbali za kuwasaidia.
-
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Walimu;
Mimi na wenzangu Serikalini tunalipa kipaumbele cha juu suala zima la Elimu
nchini. Mipango na malengo yetu katika Sekta ya Elimu inaongozwa na Malengo ya
Milenia ya Elimu, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2005 na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania
(MKUKUTA). Nia yetu ni nini basi?
Moja, ni kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wote.
Mbili, ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa na haki katika utoaji
elimu;
Tatu, kuona kuwa ubora wa elimu inayotolewa unaongezwa na
kuimarishwa;
Nne, kuhakikisha kuwa rasilimali tunazotenga kwa ajili ya utoaji elimu
zinatumika kwa ufanisi na kutimiza malengo tunayoyakusudia.
Tano, tunaimarisha asasi za uongozi na uendeshaji wa Sekta ya elimu;
Sita, tunaongeza ushirikishwaji wa Wadau mbalimbali wa elimu,
ikiwemo sekta binafsi katika upangaji sera na mipango ya elimu;
Ndugu zangu, kwa bahati nzuri, haya vilevile ndiyo malengo ya mipango
mikubwa ya elimu inayotekelezwa hivi sasa, yaani Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Msingi (MMEM) 2002 – 2006 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES)
2004 – 2009. Serikali inafanya kila juhudi ili kuhakikisha kuwa mipango hii
inafanikiwa. Lakini bila ushirikiano wa walimu hatuwezi kufika popote. Nichukue
-
fursa hii kuomba ushirikiano wa walimu wote nchini katika utekelezaji wa MMEM na
MMES.
Kuendeleza Ubora wa Elimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Malengo ya Milenia ya Elimu kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule
ifikapo mwaka 2015 yanasisitiza juu ya ubora wa Elimu itolewayo kwa watoto wote.
Mwalimu ndiyo raslimali muhimu katika kuyafikia malengo yetu tuliyojiwekea katika
Sekta ya Elimu likiwemo lile la ubora wa elimu. Hivyo basi, kauli mbiu yenu ya “Kila
Mwanafunzi Anahitaji Mwalimu Bora” ni sahihi. Ni kauli muafaka kwa kipindi hiki
tulicho nacho.
Ndugu zangu;
Kama nilivyosema hapo mwanzo, Serikali inamtambua Mwalimu na kuthamini
sana nafasi yake katika kuchangia maendeleo ya elimu na ya nchi kwa ujumla. Kwa
ajili hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa walimu wanaandaliwa vizuri,
wanaendelezwa kazini, wanaandaliwa mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kujali
maslahi yao.
RISALA
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Ninawashukuru sana kwa risala yenu nzuri na iliyowasilishwa vizuri. Nafurahi
kwamba risala imebainisha vyema mafanikio na matatizo yanayowakabili walimu na
-
kutoa mapendekezo muafaka juu ya hatua za kuchukua. Vilevile mmetaja maeneo
yanayohitaji mazungumzo na maelewano na Serikali na wadau wengine ili tuweze
kuyafikia malengo ya kielimu tuliyojiwekea. Napenda kuwahakikishia kuwa
tumesikia, tumeelewa na tuko tayari kufanya kila tuwezalo kufanya yale yanayoihusu
Serikali.
Uboreshaji wa Mishahara ya Walimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Natambua haja na umuhimu wa kuboresha maslahi ya walimu, hasa mishahara
yao. Tumeanza kuchukua hatua. Katika mwaka huu wa fedha, tumeongeza mishahara
ya walimu, kama ilivyokuwa kwa kada mbalimbali za utumishi wa
umma. Tutaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wa umma pamoja na walimu
kadri uchumi wetu unavyokua na hali inavyoruhusu.
Kwa kuzingatia hilo, tarehe 18 Mei, 2006 Serikali iliunda Tume ya Kuboresha
Mishahara ya Watumishi wa Umma pamoja na walimu. Tume ilianza kazi rasmi tarehe
01 Julai, 2006 na kazi yake kubwa ni kufanya uchunguzi kuhusu hali ya Mishahara ya
Watumishi wa Umma ilivyo sasa na kutoa mapendekezo ya namna ya kuiboresha
zaidi. Tume hiyo imeshakutana na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa
walimu wa Shule za Msingi, Sekondari, na vyuo vya Ualimu.
Kwa upande wa Walimu, tume hiyo inapitia maeneo yafuatayo kwa lengo la
kushauri namna ya kuboresha mishahara ya walimu:
Misingi gani itumike kupanga mishahara ya walimu;
Serikali ifanye nini kuboresha mishahara ya walimu;
-
Mwalimu wa Shule ya Msingi, Sekondari na Chuo ana majukumu gani
anayoyafanya kuanzia asubuhi hadi jioni;
Kazi ya mwalimu inaweza kulinganishwa na ipi nyingine katika
Utumishi wa Umma na kwa nini;
Mambo gani mengine yazingatiwe katika kuboresha mshahara wa
mwalimu.
Tume hii tayari imeanza kupokea maoni na ushauri kuhusu uboreshaji
wa mishahara ya walimu. Ni matarajio yangu kuwa muda iliyopewa utatosha kabisha
kuwasilisha mapendekezo muafaka Serikalini. Naomba tuwe na subira Tume imalize
kazi yake. Nawaahidi kuwa Serikali itaifanyia kazi ipasavyo taarifa ya Tume hiyo.
Ucheleweshaji wa Mishahara ya Walimu
Mmelielezea kwa uchungu tatizo la ucheleshwaji mishahara ya walimu.
Naelewa machungu yenu, na nawaunga mkono. Tatizo hili sasa lina kila dalili ya kuwa
sugu na kuota mizizi lisipokomeshwa. Bila ya shaka mnakumbuka kwamba Serikali
ilikwishatoa maelekezo kuwa ifikapo tarehe 25 kila mwezi mishahara ya walimu iwe
imelipwa. Hata hivyo, bado maelekezo haya hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Sababu
mbalimbali zimekuwa zikitolewa lakini bado hazikidhi haja. Sielewi kwa nini watu
wanajaribu kuhalalisha kutotimiza ipasavyo wajibu wao kwa jambo linalowezekana.
Wakati mwingine maelezo yanayohalalisha kutojali na uzembe kwa upande wa
wenzetu tuliowapa dhamana ya kushughulikia mishahara ya walimu. Bado mimi
naamini tukijipanga vizuri na kutimiza ipasavyo wajibu wetu tunaweza kulipa
mishahara ya walimu ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi. Ingekuwa vyema basi Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
-
HAZINA wakakaa pamoja na kuzungumzia vikwazo na kutafuta njia bora zaidi ya
kulipa mishahara ya walimu kwa wakati. Katika mazungumzo hayo, wazingatie suala
la walimu wapya na kuchelewa sana kulipwa mishahara yao.
Ningependa kupata taarifa kuwa baada ya kikao hicho kero hii itakuwa
imepatiwa ufumbuzi wa kudumu. Usumbufu wanaopata walimu kufuatilia stahili yao
unapunguza ari na tija yao kazini. Pia hupunguza mapenzi kwa kazi yao. Ualimu ni
kazi ya heshima. Tusimfikishe mahali Mwalimu anakopa kila mwezi ili aishi
wakati akingojea mshahara wake.
Upandishaji wa Madaraja kwa Walimu
Ndugu zangu,
Nimesikia pia kuhusu tatizo la ucheleweshaji wa upandishwaji wa madaraja
kwa walimu, ambalo nalo linachukua sura ya kuwa sugu. Pia lipo tatizo la
ucheleweshaji wa marekebisho ya mishahara baada ya kupandishwa madaraja. Wakati
mwingine mtu anapandishwa madaraja mawili au hata zaidi wakati ambapo hata kwa
daraja la nyuma alilopandishwa mshahara haujarekebishwa. Kupandishwa daraja
wakati ukifika na kurekebishiwa na kurekebishiwa mshahara kwa wakati ule ni haki ya
mtumishi. Kutofanya hivyo ni uonevu. Ni matatizo ambayo napata ugumu
kuelewa. Isitoshe hakuna maelezo ya msingi kwa nini jatatizo haya yasiishe. Naomba
sasa iwe ilani ya mwisho. Safari ijayo tupate taarifa ya mabadiliko. Hatuwezi
kuzungumza jambo hilo hilo kila mwaka.
Naomba kuitumia nafasi hii kuwakumbusha wahusika kuzingatia muongozo wa
Serikali wa mwaka 2005 kuhusu kushughulikia malalamiko ya watumishi wa umma
kuhusu kupandishwa vyeo na kuyashughulikia mapema iwezekanavyo.
-
Ni vyema mamlaka zinazohusika na upandishaji wa vyeo vya walimu zikiwemo Tume
ya Utumishi wa Umma - Idara ya Huduma ya Walimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi na halmashauri za Wilaya na Miji kuhakikisha kuwa zoezi la walimu wote
wenye sifa kupandishwa vyeo stahili linakamilika kabla ya tathmini ya utendaji wa
kazi kwa njia ya uwazi (OPRAS) kuanza.
Madeni ya Walimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Ndugu Walimu;
Mmelielezea pia tatizo la malimbikizo ya madeni ya walimu. Tunatambua kuwa
hili ni tatizo la siku nyingi na kuna walimu wengi ambao hawajalipwa kwa muda
mrefu stahili zao mbalimbali hasa fedha za uhamisho, matibabu, mapunjo ya
mishahara, gharama za masomo na posho za kikazi na likizo.
Ndugu zangu Walimu, mkakati wa kulipa madeni ya walimu tunao na
mchakato wa kufanikisha azma hiyo unaendelea. Mpaka sasa madeni ya walimu wa
shule za msingi yaliyowasilishwa ni kiasi cha shilingi Bilioni 9.9. Hatua za uhakiki wa
madeni hayo zinakamilishwa.
Nawasihi wale wanaofanya kazi hii waongeze kasi ili waimalize mapema
iwezekanavyo na malipo yafanyike ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2006/07.
Fedha yake ipo, kinachosubiriwa ni kupatikana kwa taarifa hizo za uhakiki.
Kwa upande wa walimu wa Sekondari na Vyuo chini ya Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, madeni yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.1 yaliwasilishwa
Serikalini. Baada ya uhakiki, madeni ya zaidi ya shilingi milioni 855 yameonekana
-
hayana matatizo (queries) na yatalipwa wakati wowote kuanzia sasa. HAZINA
imekwishatenga fedha hizo na nimeambiwa wako katika maandalizi ya mwisho ya
kulipa.
Nyumba za Walimu
Ndugu Walimu,
Nalitambua vyema tatizo kubwa la upungufu wa nyumba za walimu nchini,
hasa vijijini. Kama mlivyosema katika risala yenu, nyumba zilizopo zinakidhi asilimia
19.4 tu ya mahitaji. Nakubaliana nanyi kwamba tatizo hili ni mateso makubwa kwa
walimu. Lakini, napenda kuwahakikishia kuwa hili ni jambo linalonisononesha na mie
pia. Serikali inalitambua na imeendelea kulichukulia hatua za kukabiliana
nalo. Mikakati ya muda mfupi wa kati na mrefu ili kupunguza makali yake imewekwa
na inaendelea kutekelezwa.
Katika utekelezaji wa MMEM, kwa mfano, jumla ya nyumba 12,590 zimejengwa
kati ya mwaka 2002 hadi 2006 katika shule za msingi. Aidha, kwa mwaka wa fedha
2006/07 nyumba 2,000 zinatarajiwa kujengwa katika shule za msingi. Kwa upande wa
shule za sekondari, jumla ya nyumba 908 zimejengwa katika mwaka wa kwanza wa
utekelezaji wa Mpango wa MMES, unaoisha mwaka 2009. Kwa mwaka wa fedha
2006/07 jumla ya nyumba 1,000 zinatarajiwa kujengwa na fedha za ukamilishaji wa
majengo hayo tayari zimetumwa mashuleni. Aidha, kama mjuavyo, katika Mpango wa
MMES, kwa nia hiyo hiyo ya kupunguza tatizo hilo, kila yanapojengwa madarasa
mawili hujengwa nyumba moja ya mwalimu.
-
Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi
wa nyumba za walimu. Tumedhamiria kufanya hivyo ila kasi yetu inapunguzwa na
uwezo wetu ukilinganisha na mahitaji mengi ya nchi pamoja na hili la nyumba za
walimu. Tunawahakikishia kuwa tutaendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba za
walimu. Serikali pia itaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wahisani
wa nje, , mashirika ya Serikali na yasiyo ya Kiserikali na watu binafsi katika ujenzi wa
nyumba za walimu. Kwa ajili hiyo, kwa mfano, Shirika la Maendeleo ya Jamii (TASAF)
limejenga nyumba za walimu 264 kati ya mwaka 2001 na 2005. Najua wanaendelea
kufanya hivyo.
Tumeanza mazungumzo na wahisani wetu wakubwa juu ya haja ya kuwa na
mpango maalumu wa kujenga nyumba za walimu nchini. Wazo hilo linapokelewa
vizuri ila bado tunasubiri uamuzi wa kiutekelezaji. Kwa nafasi hii, nawashukuru
wadau wote wanaochangia kwa hali na mali katika kupunguza tatizo la nyumba za
walimu.
Ubora wa Elimu na Muda wa Mafunzo ya Walimu
Ndugu Walimu,
Nimefurahi sana kuona kwamba suala la utoaji wa elimu bora shuleni na
uhusiano wake na muda wa mafunzo ya walimu na mafunzo kazini mnalitambua na
kulipa nafasi yake stahiki. Ni jambo muhimu kwamba sote tunashiriki kuchuna bongo
zetu na kuchangia katika jitihada za kutafuta njia ya kuboresha elimu tunayoitoa kwa
watoto wetu. Kwa ufahamu wangu, Elimu Bora ni matokeo ya majumuisho ya mambo
mengi, mwalimu akiwa muhimili mkuu wa ubora huo.
-
Kimsingi ufanisi kwa upande wa Elimu Bora unamtegemea mwalimu
anayemudu maudhui ya somo, mahiri katika matumizi ya njia za kufundisha na
kujifunzia masomo yaliyoko kwenye mtaala. Kadhalika, hutegemea mwalimu mwenye
utambuzi wa mahitaji ya walengwa, mazingira bora ya kujifunzia na walimu kuwa
mfano wa kuigwa.
Aidha, natambua pia kwamba mazingira bora ya kufanyia kazi kwa walimu
yana nafasi ya aina yake katika uwezeshaji wa mwalimu kutumia taaluma yake na
vipaji vyake alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Uzoefu ndani na nje ya nchi na utafiti wa kielimu unaonesha wazi kuwa Ubora
wa Mwalimu hutegemea sana mafunzo endelevu baada ya kupata Mafunzo ya Awali
(tarajali). Tunaweza kuwaweka walimu miaka 2, 3 au hata zaidi katika mafunzo ya
ualimu, lakini kama hakuna mafunzo ya kufuatilia ni vigumu kupata aina ya walimu
tunaowataka. Hivyo hatuna budi kuweka mkazo stahiki kwa mafunzo kazini kwa
walimu wetu.
Ndugu Walimu, naomba tutambue pia kuwa unapokuwa na mipango ya kuleta
mabadiliko makubwa katika elimu, aghalabu huna budi kutumia njia mbadala na
wakati mwingine za dharura kupata mahitaji ya msingi au kutatua matatizo muhimu.
Mpango wa muda mfupi wa kuandaa walimu ni mfano mmojawapo. Huu ndiyo
ulikuwa msingi wa kuendesha Mafunzo ya Ualimu Ngazi ya Cheti katika sehemu mbili
(yaani Chuoni na Shuleni) wakati wote wa utekelezaji wa MMEM. Baada ya mahitaji ya
haraka ya walimu kupungua, hivi sasa Serikali imerudi tena kwenye kutoa mafunzo ya
Ualimu kwa miaka miwili.
Kwa kutumia njia hii mbadala kwa mwaka mmoja tumeweza kuboresha uwiano
wa mwalimu kwa mwanafunzi kutoka 1:56 (2004) hadi kufikia 1:52 (2006) kitaifa
-
pamoja na kwamba bado zipo tofauti baina ya mikoa na wilaya. Kinachotakiwa sasa ni
kuendeleza mafanikio yaliyopatikana. Kazi iliyo mbele yetu ni kuimarisha mafunzo
kwa walimu wetu hawa ili kunoa ubora wao.
Kazi hiyo tunaendelea nayo. Tumekwishatumia shilingi milioni 880.5
kugharamia walimu wa Sekondari 655 na wakufunzi 370 kujiendeleza kwenye Vyuo
Vikuu.
Pia, nimejulishwa kuwa walimu 21,519 wa Daraja B na C wameendelezwa
kitaaluma na walipimwa Mei, 2006. Vilevile, Walimu 26,017 wanaendelea na mafunzo
na watafanya mitihani yao ifikapo Mei, 2007. Nimeambiwa pia kuwa Walimu 42,000 wa
daraja A wamehudhuria Mafunzo ya Ualimu kazini katika matumizi ya njia shirikishi.
Kwa hiyo, tunaendelea kufanya juhudi. Nia yetu ni kuhakikisha kwamba Kila
Mwanafunzi anapata Mwalimu aliye Bora, aliyeandaliwa vyema, kama ambavyo kauli
mbiu yenu inavyosema.
Kutokana na umuhimu wa kuendeleza walimu kitaaluma na kitaalamu natoa
wito kwa mamlaka zote zinazohusika na masuala ya walimu kuhakikisha kuwa fedha
zote zinazotengwa kwa ajili ya mafunzo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Waratibu wa Elimu ya Sekondari
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Elimu ya Sekondari ni muhimu katika maendeleo ya Elimu nchini na katika
kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tunashukuru kwamba Elimu ya Sekondari
inapanuka kwa kasi kubwa nchini. Hii inatupa changamoto ya kuendelea na jitihada za
-
kuiboresha. Hivyo, katika kuiboresha Elimu hiyo, tumeamua kusogeza huduma karibu
na walimu. Utaratibu wa kuwa na Waratibu wa Elimu ya Sekondari katika ngazi ya
wilaya ni hatua ya awali ya kufikia azma hiyo.
Vifaa vya Kufundishia na Kujifunzia
Ndugu zangu, Walimu,
Napenda sasa kuzungumzia suala la upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na
kujifunzia. Elimu bora na Mwalimu Bora huchangiwa sana na upatikanaji wa nyenzo
na vifaa vya kufundishia. Vilevile, kuwa na mwanafunzi bora kunategemea upatikanaji
wa vifaa vya kujifunzia pamoja na walimu bora na mazingira mazuri ya shuleni na
nyumbani.
Tunatambua ukubwa wa matatizo ya upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na
kujifunzia hasa katika kipindi hiki ambapo shule zinaongezeka na ubora wa elimu ni
agenda yetu muhimu. Tunaendelea na juhudi za kulikabili tatizo hili. Tumenunua
vitabu vya kiada vya kutosha sasa na kupunguza uwiano wa mwanafunzi kwa kitabu
kwa shule za msingi kutoka 1:20 mwaka 2000 hadi 1:3 mwaka huu.
Tutaendelea kutoa Ruzuku ya Uendeshaji kwa shule za msingi kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Katika mwaka huu wa fedha,
tumetenga jumla ya shilingi bilioni 44.8 kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na
kujifunzia. Hata shule za Sekondari zisizokuwa za Serikali nazo tumeamua
kuzichangia. Tumetenga shilingi milioni 250 kwa ajili hiyo. Serikali itaendelea
kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote ili kufikia lengo la
kutoa elimu bora kwa watoto wetu.
-
TATIZO LA UKIMWI
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT,
Ndugu Walimu,
Nimefarijika sana kuona kuwa, katika risala yenu, mmeongelea suala la
UKIMWI. UKIMWI bado ni tishio la maisha ya Watanzania wote ikiwa ni pamoja na
walimu. Ugonjwa huu unatishia kuhatarisha na kudhoofisha juhudi tunazozifanya za
kupunguza pengo la upungufu wa walimu. Kila mwaka, UKIMWI unatupokonya
walimu wengi. Hatuna budi kuongeza juhudi za kupambana na maradhi haya hatari.
Nawaomba walimu muamue kukataa kuambukizwa UKIMWI.
Ugonjwa huu unaepukika, na nitashangaa sana kama yupo mwalimu asiyejua
njia za kuepuka UKIMWI. Ukweli ni kwamba jamii inawategemea walimu kuwaandaa
watoto wao wajiepushe na UKIMWI. Siamini kuwa wapo walimu wasiojua A,B,C za
kujikinga na UKIMWI: Abstain, Be faithful or Use condom. Sio mambo mapya.
Wasiokuwa na ndoa, wasubiri; wenye ndoa, wawe waaminifu – hata wenye wapenzi
hivyo hivyo. Na wale watakaoshindwa kabisa wahakikishe wanapofanya tendo la ndoa
wanafanya hivyo kwa usalama na usalama huo unafahamika. Nawasihi tuzingatie haya
kwani tatizo hili ni kubwa na linalotishia maangamizi.
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT,
Serikali inao Mpango wa Elimu ya UKIMWI katika Shule za Msingi, Sekondari,
Vyuo na sehemu za kazi. Kupitia mpango huu, walimu hupata uelewa wa mambo
mbalimbali kuhusu UKIMWI ikiwa ni pamoja na elimu ya matumizi ya dawa za
-
kurefusha maisha. Ninaelewa kuwa si walimu wote wanaopata mafunzo hayo
vyuoni. Hata hivyo, tunawategemea hao wachache kuwaelimisha wengine
wanaporudi vituoni mwao ili nao wajumuike katika mapambano haya ya kufa na
kupona.
Kwa kuwa Chama cha Walimu kinawakilisha walimu walio wengi, ninashauri
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi wakae pamoja na CWT kuona ni jinsi gani
wanaweza kushirikiana kukabiliana na janga hili.
Pengine niitumie nafasi hii kuwaarifu kuwa mke wangu, ambaye ni Mwalimu
mwenzenu, ameamua kutumia muda wake wa kuwa likizo bila malipo kujishughulisha
na juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana. Nafahamu pia
kwamba anayo nia ya kutumia sehemu ya muda wake kuchangia katika mapambano
dhidi ya maradhi haya miongoni mwa walimu wenzake. Mimi na yeye tunatambua
kuwepo kwa wanaharakati wa mapambano haya miongoni mwenu. Ameamua
kushirikiana nanyi, kufanya kazi nanyi. Nawaomba mumpokee, mshirikiane naye.
Nadhani anaweza kuwa wa msaada kwa kiasi fulani.
Ndugu zangu,
Katika risala yenu mmeongelea pia masuala mengine ya maslahi na haki zenu
kama walimu. Yale yote yahusuyo matatizo ya Mfuko wa Bima ya Afya, Malipo ya
Pensheni, kuundwa kwa chombo cha majadiliano kati ya CWT na Serikali, nimeyasikia,
Waziri wa Elimu ameyasikia na viongozi wa Chama cha Walimu nao wameyasikia.
Bahati nzuri sana mnaye Waziri anayejua kwa undani kero na matakwa ya
Walimu. Yeye ni Mwalimu mwenzenu na kwa miaka kadhaa amekuwa mwanaharakati
mwenzenu wa kupigania haki za wafanyakazi (sijui baada ya kuwa Waziri wa Elimu
kama bado ni mwanaharakati).
-
Mnacho Chama imara cha Walimu Tanzania, na, nawahakikishia kuwa mnayo
Serikali inayosikia, inayosikiliza, inayojali na iliyo tayari kuchukua hatua. Tunayo
dhamira ya dhati ya kuboresha elimu kwa kuongeza walimu, kuboresha hali ya shule,
maslahi ya walimu, pamoja na mazingira yao ya kufanyia kazi. Tuendelee kuzungumza
na kushauriana.
Nimefurahi kwamba mmesema kwenye risala yenu pia kuhusu utekelezaji wa
kuundwa kwa chombo cha majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Walimu
Tanzania. Ni kweli Tanzania imeridhia mkataba wa Shirika la Kazi Duniani ILO No. 98
unaohusu haki za wafanyakazi kujadiliana na waajiri kuhusu maslahi na mazingira
bora ya kazi. Sheria ya majadiliano ya Watumishi wa Umma ilipitishwa na Bunge
mwaka 2003 na ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali mwaka 2004.
Sheria hiyo inatumika ila haijaeleza wazi ni nani mwenye mamlaka ya kuunda
chombo/baraza la majadiliano (joint staff council). Kufuatia hali hiyo ziliandaliwa
kanuni ambazo zinatoa mwongozo kuhudu uundaji wa chombo cha majadiliano, na
kanuni hizo zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali mwaka 2005. Kwa umuhimu wa
suala hilo, naiagiza Menejimenti ya Utumishi wa Umma kukamilisha kanuni hizo ili
zianze kutumika.
Hata hivyo mie na nyie hatuna haja ya kungoja kanuni ndio tujadiliane masuala
ya maslahi ya Taifa letu. Tuendeleeni.
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Walimu,
-
Nimesema mengi. Naomba nimalizie kwa kuwapongeza tena walimu wote
nchini kwa kazi nzuri mnayoifanya. Natambua mazingira magumu mnayofanyia kazi
ila napenda kuwahakikishia dhamira yetu ya kuchukua hatua kuyaboresha. Nawasihi
walimu wa ngazi zote nchini kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu taaluma yenu na
kuendelea kuwa kioo cha maadili mema kwa watoto tuliowakabidhi kufundisha na
kwa Watanzania kwa ujumla. Hatma ya taifa hili ipo mikononi mwa Walimu.
Nawashukuru tena kwa kunikaribisha kushiriki nanyi katika kilele cha Sherehe
za Siku ya Mwalimu Duniani kwa mwaka huu wa 2006.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!