bida'a

35
BID'AH - SHAYKH 'ABDULLAAH SWAALIH FAARSIY. KITABU HIKI KIMEKUSANYWA NA SAID KHAMIS ABBASI (MROPE) Kwa ushirikiano Na Al-Hidaaya Dar es salaam-Tanzania

Upload: muhtasim-aziz

Post on 16-Apr-2015

180 views

Category:

Documents


1 download

DESCRIPTION

Al farsy

TRANSCRIPT

Page 1: Bida'a

BID'AH - SHAYKH 'ABDULLAAH SWAALIH FAARSIY.

KITABU HIKI KIMEKUSANYWA NA SAID KHAMIS ABBASI (MROPE)

Kwa ushirikiano Na Al-Hidaaya

Dar es salaam-Tanzania

Page 2: Bida'a

YALIYOMO

1. Utangulizi

2. Dibaji

3. Bid'ah za Adhana

1. Kunadi Swalah

2. Kuongeza maneno kabla ya Adhaana

3. Kuongeza maneno kabla ya kuqimu

4. Kutia vidole machoni

5. Kuadhini wakati wa kuzika

4. Misikiti

1. Kaburi kuitwa ndani ya Msikiti

5. Misuwaki

1. Kupiga mswaki ndani ya msikiti wakati anafunga Swalah

6. Wudhuu

1. Kutamka nawaytu

2. Kusoma du'aa za kila kiungo

7. Swalah

1. Kuanza Swalah kwa

2. Kupeleka mikono upande wa kushoto

3. Kelele za Aamiyn

Page 3: Bida'a

4. Kutia Sayyidna katika kumswalia Mtume

5. Kelele za du'aa baada ya Swalah

6. Kutia mikono karibu ya kwapa katika kuomba du'aa

7. Kubakia Imaam kwenye Mihirabu

8. Kutia Faatihah

9. Kupeana mikono baada ya Swalah Fulani

10. Kuletwa khatibu na mtu anayesema maneno

11. Kupiga kelele za kumswalia Mtume na Maswahaba

12. Kusali Swalah tano pamoja Ijumaa ya mwisho ya Ramadhaan

13. Kuzaliwa Mtume baada ya Takbiyrah za 'Iyd

8. Qur-aan

1. Kukariri Qul Huwa Allaahu mara tatu

2. Kusoma Yaasiyn au sura nyengine watu wote kwa sauti moja

3. Kuisoma Suratul Faatihah kwa pumzi moja

4. Kusoma Sura makhsusi tu

9. Dhikri

1. Kudhikiri

2. Katika ubaya mkubwa wa kudhikiri

3. Palipotokea dhikiri

4. Kuchukua na kuvaa tasbihi

5. Kujenga mazawiya

10. Du'aa

1. Kuweka moto na kutia ubani

2. Kuomba kwa jaha ya Mtume na watu wakubwa

3. Kuombwa Mtume na kuombwa hao maiti wakubwa

Page 4: Bida'a

4. Katika du'aa za uzushi na mbaya (a)(b)(c)

5. Katika du'aa za uzushi

6. Dalailul Khayraat

7. Madihi

8. Burdai

11. Ugonjwa

1. Kwenda kutazamia

2. Kuwewliwa

3. Kupungwa

4. Kuvaa hirizi

5. Kunywa kombe

6. Kuchomolewa

12. Mauti

1. Kuandika juu ya sanda

2. Kwenda na jeneza pamoja na Tahliyl

3. Kuadhini wakati wa kuzika

4. Kulaqinia

5. Khitmah

6. Halili

7. Kupikiwa vyakula

8. Kuchinjiwa

9. Kufanyiwa Hawli

10. Kufanyiwa ziyara

11. Kufanyiwa 'Aqiyqah

12. Bid'ah za Eda

13. Kujengea makaburi

Page 5: Bida'a

14. Kuweka makumbusho vitu vya hao waliokufa

13. Kufunga

1. Kukhusisha kufunga mwezi wa Rajab

2. Kuikaribisha Ramadhaan

3. Kuimwaga

4. Kukesha masiku ya kuamkia sikukuu

14. Mawlid

1. Kusoma Mawlid

2. Zeffe (Zafa)

3. Kupiga

4. Kupiga dufu na mazumari Msikitini

15. Kushughulika mwaka wa Nayruzi

16. Kuoa

1. Kutazamia manazili (Saa ya kuolea)

2. Kusema mwezi fulani ukorofi kuoa

17. Kutazamia kwa Msahafu na Tasbihi

Page 6: Bida'a

UTANGULIZI

1. Naanza kushuka kalamu

Nandika jina Adhimu

Natanguliza Isimu (Jina La Mungu)

Bisumilahi awali

2. Allahu jina la Mungu

Ndiye wa Tangu na Tangu

Mwenye ardhi na mbingu

Wa Milele na Azali (Daima)

3. Rahmani Mola Wetu

Na amuumbapo mtu

Muumba wa kila kitu

Humjibu Filhali (Pale pale)

4. Rahimu anarehemu

Jamiina kuluhumu

Viumbe Vyake dawamu

Hawatupilii mbali

5. Sala na Salamu Zake

Bora wa Mitume Yake

Zende kwa Mtume wake

Na kwa wake wote Ali (Wafuasi)

6. Jamii ya Maswahaabah

Na kila mwenye mahaba

Azwaji na Qaraba (jamaa)

Na huyu wake Rasuli

7. Rabi yangu Matulubu

Si Nukuta Si Irabu

Kutunga kusoharibu

Yote yawe ni ya kweli

Page 7: Bida'a

8. Nawe umeniwezesha

Bila ya kubabaisha

Mengi nimebainisha

Haki ikawa batili

9. Vingi Nilivyovitunga

Mabaya nikayapinga

Nikazifichua kunga (Siri)

Mema nikayakubali

10. Basi Ninakushukuru

Unizidishie Nuru

Mola Rahimu Ghafuru

Kiza kiniondoke Mbali

11. Na hao ninowambiya

Kwani yote ni ya njia

Wayafwate yote piya

Ya Diyn yako Jalili

12. Hiki kitabu kingine

Ni kama vile vyengine

Cha BID’AH wakione

Kwa Zake kubwa fadhila

13. Alhamdu Lillahi

Namshukuru Ilahi

Jioni na asubuhi

Shukuru nyingi kamili

Page 8: Bida'a

DIBAJI

BISMILLAHIR-RRAHMANIR RAHYM

Bid’ah iliyokusudiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukatazwa na kutukanwa ni kuitwa katika Diyn na kuitikiwa kuwa ni ‘Ibaadah, jambo ambalo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema litiwe katika Diyn wala hajalifanya, na hali ya kuwa anao uweza wa kulifanya.

Wewe ukisema: “Lakini jambo hili ni zuri.” Basi umo katika khatari kubwa na Diyn yako. Kuona kuwa Mtume hakulifanya jambo zuri hilo mpaka amekufa wala hakulijua kuwa ni zuri akapata kutuhimiza kulifanya.

Itakuwa Mtume kashindwa na hao. Na huu ni uwongo kabisa na ni muhali na utovu wa adabu na ukosefu wa fikira. Mtume Alisema:

((Hapana amali yoyote ya kukupelekeni Peponi ila nimekujulisheni na kukuamrisheni.))

Hadiyth hii Imepokewa na Is-haak Bin Rahawayh(Rahyah) kama ilivyo katika sahifa 224 ya Juzuu ya mwanzo ya Al-Matalibul-‘Aliyya Bi Zawaidil-Masaaniyd-th Thamaaniyyah na akapokea Al-Haakim, kama ilivyo katika sahifa 110 ya Arradul Muhkamil Matiyn.

Na akahadharisha sana Mtume kufuata ya kuzaliwa yakatiwa katika mambo ya Diyn. Akasema:

((Tahadharini na mambo ya kuzuliwa kwani kila chenye kuzuliwa kikatiwa katika Diyn ni upotofu (tu).))

Hadiyth hii wameipokea Maimamu hawa: Abu Daawuud na At-Tirmidhiy na wakasema kuwa ni Hadiyth madhubuti. Na akaitaja Imaam An-Nawawiy katika kitabu chake: “Arba’iyn Nawawy” katika Hadiyth ya 28.

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Hadiyth ya 5 ya Arba’iyn Nawawy:

((Atakayezua akatia katika Diyn yetu hii ambacho hakiko, atarejeshewa mwenyewe (apigwe nacho usoni).))

Na akasema tena Mtume kama ilivyo katika Hadiyth hii hii ya 5:

Page 9: Bida'a

((Atakaye fanya amali ambayo haina amri yetu basi atarejeshewa mwenyewe.))

Hadiyth zote mbili wamezitaja Maimamu hawa Al-Bukhaariy, Muslim na wengine.

BID'AH ZA ADHAANA

1. Kunadi Swalah

Hakusunisha Mtume kabisa jambo hili kwani usiku alivyosema Mwenyezi Mungu katika Aayah nyingi: ”Sakana” (wakati wa mapumziko) sio wa kufanyiwa makelele wagonjwa na watoto wachanga na wafanyaji ‘Ibaadah zao kwa utulivu. Hao wanadi Swalah wanadhani kuwa wanapata thawabu kumbe wanapata dhambi wapate iqaabu, aliyewatuma nani wazue yao?

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisunisha Swalah ya Alfajiri iwe na adhaana mbili. Si makelele ya kunadi maneno mengine. Alisunisha kuadhiniwe nusu saa hivi kabla ya Alfajiri ili wenye Witri zao wamalize upesi, wanaokula daku wafanye upesi nao.

Ukifika wakati anaadhini Muadhini mwengine kujulisha kuwa wakati wa Alfajiri umeingia.

Na inataka wawe waadhini mbali mbali ili ijulikane ile sauti ya anayeadhini kabla ya kuingia wakati na anayeadhini baada ya kuingia. Na haya ndiyo yaliyomo katika vitabu vyote vya Fiqh. Havisemi kabisa habari ya Tarhiyb -kunadi Swalah, seuze kwa makelele ya microphone ya sasa.

Madiynah wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiadhini Bilaal (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kabla ya wakati. Na akiadhini Ibn Ummi Makhtuum baada ya kuingia wakati.

Na katika vitabu vilivyobainisha u-bid’ah huu ni sahifa 248 ya Juzuu ya pili ya Al-Madkhal na Sahifa 137 ya Talbiys Ibliys.

2. Kuongeza Maneno Kabla Ya Adhaanah

Kama kusoma aayah ya mwisho wa Suratil-Israa: ”Waqulil HamduliLlaahi...”. Umetajwa u-bid’ah wake hata katika sahifa 131 ya Juzuu ya kwanza ya Al-Fataawal Kubraa ya Ibn Hajar. Na huko kuleta huyo Muadhini Swalaatun Nabiy kwa sauti kubwa ni uzushi uliozuliwa Misri wa Ismailia (Wazee wake Agha Khan) walipokuwa wakitawala huko. Kisha yakathibitishwa na Swalaahud-Diyn kwenye karne ya sita alipovunja ufalme wao.

3. Kuongeza Maneno Kabla Ya Kukimu

Page 10: Bida'a

Kama ”AlhamduLlaahi Was-swalatu Was-salaamu…” umebainisha u-bid’ah huu hata katika sahifa 63 ya Juzuu ya kwanza ya sherhe ya Rub'ul ‘Ibaadah, inayoitwa Bushral Kariym.

4. Kutia vidole machoni wakisikia “Anna Muhammadar RasuuluLlaahi”

Mtume katuamrisha tumjibu Muadhini kama anavyosema ila katika Hayya ‘Alambili. Lakini hakusema kabisa kuwa akifikia Muadhini “…Anna Muhammadar RasuuluLlaahi” tutie vidole machoni na kusema hayo maneno waliyoyazua. Natuutenge uzushi tufuate aliyotwambia Mtume.

Hata Al-Haddaad katika Sahifa 60 ya “Uquudulmas” amebainisha kuwa haya, haya kusuniwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aliyazua haya Shaykh mmoja wa Yeman aliyekuwa akiitwa ‘Aliy bin Hussayn aliyezaliwa mwaka 577 akafa 623.

5. Kuadhini Wakati Wa Kumzika Maiti

Umetajwa u-bid’ah wake katika sahifa 24 ya Juzuu ya kwanza ya Fataawal Kubraaya Ibn Hajar. Na bid’ah hii ilizuliwa na huyu ‘Aliy bin Hussayn Al-Yamaniy aliyezaliwa mwaka 577 akafa 623. Anajionea mwenyewe huko kwa aliyoyazua na mengineyo, Alikuwa mwingi wa uzushi.

MISIKITI

1. Kaburi Kutiwa Ndani Ya Msikiti

Amewalaani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaofanya hivi kama ilivyo katika sahifa 209 ya Juzuu ya pili ya Mukhtasar Sharhil Jaami’is-Saghiirna vinginevyo. Bali Al-Bukhaariy na Muslim pia.

Wakaamrisha Maimamu ivunjwe Misikiti ya namna hii kama ilivyo katika sahifa 93 ya Juzuu ya kwanza ya Zawaajir ya Ibn Hajar.

Page 11: Bida'a

WUDHUU

1. Kutamka Nawytu

Maadam akili yako huwezi kufanya jambo lolote bila ya kuazimia jambo hilo, (kulitilia niyah). Akatakiwa kila Muislam akifanya jambo awe hadhiri. Awe kalikusudia jambo hilo. Si kufanya bila ya kutambua anafanya nini, ili alipwe na Mwenyezi Mungu, kwa hiyo azma yake analolifanyia ili alipwe kwa niyah hiyo. Ndiyo maana Mtume akasema:

((Amali zote zinalipwa kwa niyah uliyoitilia.))

Lakini kabisa hakuwa Mtume akitamka akasema: “Nawaytu...” si katika kutawadha wala kuswali wala kutoa Zakaah wala kufunga wala kuhiji wala...

Na vitabu vya Hadiyth vimejaa tele, na atafute humo mtu kama anaona. Na maadam hataona basi hapana jambo hili.

Basi kwa nini anafanya asilolifanya Mtume? Ataona mote humo kuwa Mtume akianza Swalah kwa “Allaahu Akbar” si Nawaytu Uswally… na akianza Hijjah kwa.. “Labayka bi Hajj” si “Nawaytu Hajja”

Na vitabu vyetu vyote takriban vinaandika: “Niyah ni moyoni (si kutamka).”

Khalafu wengi huongeza, “Inapendeza kuitamka hiyo niyah” Hawathubutu kusema “Imesuniwa.” Kwani Mtume hakusunisha haya. Waliyethubutu kusema hivi ni wanavyuoni wetu wa mwisho. Na kwenye miaka hii hii ya mia mia tu. Hatutayawacha yaliyosemwa na hao wa mwanzo tuwashike hawa.

Lakini wasikie wanavyuoni wetu wakubwa kabisa na wa mwanzo kabisa waliokufa kiasi miaka alfu leo. Kama Abu Is-haaq Shirazy katika sahifa 69 ya Juzuu ya mwanzo ya Muhadhdhabu. Ameandika:

“Pana katika watu wetu waliosema kuwa anuwie moyoni na atamke kwa ulimi. Na haya ni maneno ya upuuzi.” Na akasema hivi Imaam Ghazaaliy katika sahifa 24 ya Juzuu ya kwanza ya Al-Wajzy.

Bali hata baadhi ya ‘Ulamaa wetu wa zama za nyuma kama Ibn Hajar Al-Asqalaaniy katika sahifa 55 ya Juzuu ya mwanzo ya Talkhiysul Habiyr, ameandika:

Page 12: Bida'a

“Wala haisuniwi kutamka niyah kwani haikupokewa kwa Mtume wala Maswahaba wala Maimamu wanne.” Na akasema kama haya As-Saqqaf katika sahifa 54 ya “Tarshiyhul-Mustafiydiyn” Sharh ya “Fat-hul Mu’iyn”.

2. Kusoma Du’aa Za Kila Kiungo Cha Kulia Na Cha Kushoto

Ni uzushi tu hata akasema mwenye Minhaj mwisho wa mlango wa udhu:

“Nimeondosha du’aa za viungo kwani maneno hayo ni ya uzushi.”

SWALAH

1. Kuanza Swalah Kwa...

Kuanza kwa “Audhu, Qul-A’udhu bi Rabbin Naas, Nawaytu”. Yote haya ni bid’ah. Mtume Akisema:

“Cha kufungulia Swalah ni Allaahu Akbar”

Hadiyth hii Imepokewa na Maimaam wote wa Hadiyth.

2. Kupeleka Mikono Upande Wa Kushoto Ikabili Moyo

Haya ni maongezeo. Hadiyth za Mtume zinasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiweka mikono chini ya kifua (sawasawa) sio kuzidi kushotoni wala kuliani, na vitabu vyetu vya Fiqh vya mbele huko vikisema hivi tu. Hiyo ni miongezo.

Tanbihi: Kadhalika imethibiti katika Hadiyth kufunga mikono juu ya kifua kama ilivyopokewa na Abu Daawuud, Ahmad, Ibn Khuzaymah na wengineo.

3. Kelele Za Aamiyn

Katika mwisho wa Al-Hamdu na kwenye Qunuut, na itikiwe Aamiyn kwa sauti ya kiasi. Mwenyezi Mungu Anasema katika Aayah ya karibu na mwisho wa Suratul-Israa:

{{Usitoe sauti kubwa katika kuomba kwako.}}

Page 13: Bida'a

Na akasema haya katika Aayah 205 ya Suratul-A’araaf na akasema katika Aayah ya 55 ya hii hii Suratul-A’araaf:

{{Mwombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo; yeye hapendi wanaopindukia mipaka.}}

Na watu wanaopindukia mipaka. Imaam hupiga kelele na Maamuma wakamshinda. Wanaona wanatengeneza, kumbe wanaharibu.

Na Mtume akasema: ((Hamumsemezi kiziwi.)) Hadiyth hii Imepokewa na Maimam wote wa Hadiyth.

Tanbihi: Sauti iwe yenye kusikika vizuri kama katika Hadiyth inayoonyesha kuwa ni katika mambo yenye kuwatia Mayahudi wivu kwa Waislam ni sauti ya Aamiyn na kutoleana Salaam, kama ilivyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy, Ibn Maajah, Ahmad na wengineo. Vilevile Qunuut ya Swalah ya Alfajiri haijathibiti kwa mapokezi sahihi.

4. Kutia Sayyidna Katika Kumswalia Mtume

Ilipoteremka Aayah ya 56 ya Suratul-Ahzaab iliyotuamrisha tumswalie Mtume. Maswahaba walimwambia Mtume tusemeje katika kukuswalia. Akasema semeni:

((Allaahumma Swalli ‘Alaa Muhammadin wa ‘alaa aali Muhammadin kamaa Swallayta ‘Alaa Ibraahiym wa ‘alaa aali Ibraahiym.))

Hakutia “Sayyidna” katika jina lake wala katika jina la Ibraahiym. Wewe kwa nini unatia “Sayyidina” (Bwana wetu)? Ukisema ndiyo adabu kumwita mtu mkubwa Bwana. Basi Mtume hajui heshima hiyo ya kumuita Ibraahiym Bwana? Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu kamwambia Mtume katika Aayah ya 123 ya Suuratun-Nahl kuwa mfuate Ibraahiym. Fuata mwendo wake.

Uko khatarini kweli kweli ukimwona Mtume hajui kufundisha. Endelea tu na ushupavu.

Na ukitazama vitabu vyetu vyote vya Fiqhi vinapotaja kumswalia Mtume havitii “Sayyidna”, laa katika tamko la Nabii Muhammad wala Nabii Ibraahiym, ila baadhi chache tu ya vitabu vya wanavyuoni wa nyuma.

Kimoja ni Baabu. Nacho kimetungwa pande hizi wala haijulikani huyo aliyokitunga. Utaacha vitabu vya ‘Ulamaa wanaojulikana umfuate asiyejulikana? Unajitia katika matata sana. Wacha ukaidi ufuate yenye maana. Na huyu akamwita Sayyidna, Nabii Muhammad tu.

5. Kelele Za Du’aa Baada Ya Swalah Na Wakati Mwengine

Page 14: Bida'a

Vitabu vyetu vyote vya Diyn vinakataza haya. Katika Fat-hul Mu’iyn kama ilivyo katika sahifa 89 ya Juzuu ya pili ya I’aanatu Twaalibiyn utaona imeandikwa “Ni Haramu kusoma kwa sauti kubwa Msikitini”.

6. Kutia Mkono Karibu Ya Kwapa Wakati Wa Kusoma Du’aa

Uzushi tu si maongozi ya Mtume

7. Kubakia Imaam Kwenye Mihrabu Na Maamuma Kwenye Safu Zao

Wanoleta nyiradi. Hakuwa Mtume akiyaleta haya kabisa. Vitabu vyote vya Hadiyth vinasema kuwa Mtume akishakutoa salamu hukaa kiasi cha kusema:

“Allaahumma Anta Salaam wa Minkas Salaam Tabaarakta yaa Dhal Jalaali wal Ikraam”

Na kiasi cha kuondoka wanawake walio nyuma, kisha huyo anaondoka, na kila mmoja anasoma du’aa zake na huku anakwenda zake.

Na vitabu vyetu vya Fiqhi vya kutegemewa vikasema haya kama sahifa 104 ya Juzuu ya pili ya Tuhfatul-Muhtaaj. Imesema hivi:

“Na bora kwa Imaam akishakutoa salamu ainuke aende zake ikiwa hapana wanawake.” (Nyuma yao).

Na yakisemwa haya haya katika sahifa 183 ya Juzuu ya kwanza ya Nihaayatul-Muhtaaj. Bali na kwenye sherhe za Rubul-‘Ibaadah zote mbili zimesema vivi hivi. Kama sahifa 86 ya Juzuu ya kwanza ya Bushral Kariym na sahifa 177 ya Hashiya ya Al-Kurdy na sahifa 52 ya Mataalibul-Muhimmat Fiy Ahkaamil ‘Ibaadat na vyenginevyo. Vikasema:

“Na kila mmoja anasoma uradi wake na huku anakwenda zake.”

8. Kutia Fat-ha Baada Ya Swalah Na Kabla Ya Kila Du’aa

Maneno yaliyomo katika Suratul-Faatihah ni Sura bora kabisa. Na Mtume akaamrisha isomwe ndani ya kila Swalah za Fardhi na za Sunnah. Lakini hakutwambia tuisome baada ya Swalah wala hakuwa mwenyewe akifanya hivyo. Na sisi juu yetu kumfuata Mtume, kama tunavyoambiwa katika Qur-aan mara kwa mara.

Haya mambo ya kuifanya Suratul-Faatihah ndio kianzio cha kila du’aa na kisafishio chake - wala haisomwi kwa taratibu na hishima - ni uzushi uliozuka katika mwaka wa arba mia wa Kiislamu, kama ilivyobainishwa katika sahifa 136 ya Juzuu ya pili

Page 15: Bida'a

ya “Dhakhyratul Maad” Sharh ya uradi wa Al-Haddaad ya Basawadan, na katika sahifa 161 ya Juzuu ya pili “Lawaqihul Anwaril Qudsi” ya Shaarany na katika sahifa 161 ya Juzuu ya mwanzo ya “Subulus-Salaam” Sharh ya Buluughul-Maraam.

Na ni Hadiyth ya uongo hiyo inayosema kuwa Mtume kasema “Suratul-Faatiha inayokamatana na hayo aliyoyakusudia huyo mwenye kusoma”.

Yamebainishwa haya katika sahifa 105 ya “Alluu-luul Marsuu Fil-Ahadiythil Mawdhuu”. Na sahifa 298 ya “Al Maqaasidul-Hasanah.” Basi kusema “At-Faatihah Biniyyati…” uzushi tu.

9. Kupeana Mikono Baada Ya Swalah Fulani

Baada ya Swalah ya Alaasiri na Alfajiri na Ijumaa. Uzushi tu hakusema Mtume. Mtume kasema Waislamu wapeane mikono kila wakikutana.

Na huko kusema mukipeana mikono baada ya Swalah hizi pengine mutapata bahati ya kupambana na Nabii Al-Khidhr ni maneno yasiyokuwa kweli. Al-Khidhr amekufa kama walivyokufa wanaadamu wengine waliopita zamani, kama ilivyo katika sahifa 432 ya Juzuu ya kwanza ya “Al-Isaabah” na ndivyo alivyosema Mwenyezi Mungu katika Aayah ya 144 ya Suratul-Al-‘Imraan na Aayah ya 8 ya Suratul-Anbiyaa.

Na kuwa kupeana mikono huku ni bid’ah kumetajwa katika vitabu vingi. Katika hivyo ni sahifa 446 ya Juzuu ya nne “Sharhul Muhadhdhab” na sahifa 56 ya “Tarshiyhul Musta’idyn” Sharha ya Fat-hul Mu’iyn.

10. Kuletwa Khatwiyb Na Mtu Na Huku Anasoma

Kwenye Swalah ya Ijumaa na ‘Iyd ni uzushi pia ulioigwa kwa Wakiristo. Khatwiyb wao ndio huletwa hivyo. Na kwenye Bunge, Spika analetwa hivyo - kuiga kanisani. Na Mtume - kama tutakavyoona – alisema: ((Mtawaiga Mayahudi na Manasara.))Mpotee.

Ubid’ah wa kumleta Khatwiyb umetajwa Katika sahifa 461 ya Juzuu ya pili ya Tuhfana Sahifa 59 ya Juzuu ya pili ya Nihaayah. Na kuwa yametokea haya katika karne ya tisa.

11. Kupiga Kelele Za Kumswalia Mtume Na Maswahaba

Uzushi pia na tumebainisha makatazo ya Mtume juu ya haya kwenye mlango wa Swalah nambari mbili.

12. Kuswaliwa Zote Swalah Tano Baada Ya Swalah Ya Ijumaa Ya Mwisho Ya Ramadhaan

Page 16: Bida'a

Na kuitakidi kuwa zinalipa Swalah zote zilizomfutu za mwaka mzima uliopita au miaka iliyopita; ni upotevu. Vitabu vya Hadiyth vimebainishwa uharamu wa Swalah hii. Katika hivyo ni:

a) “Tuhfatul-Muhtaaj” sahifa 348 Juzuu ya pili.

b) “Fat-hul Mu’iyn” sahifa 271 ya Juzuu ya kwanza ya “Ianatut Talibyn”.

c) “Fataawa Ibni Hajar” sahifa 217 Juzuu ya kwanza.

d) “Faydhul-Illaahil-Maalik” Sharh Umdatis Saalik sahifa 138 ya Juzuu ya kwanza.

e) “Qurratul-‘Ayn Fiy Fataawal-‘Ulamaail-Haramayn” sahifa 76 na chungu ya vitabu vyengine.

13. Kuswaliwa Mtume Baada Ya Takbiyr Za ‘Iyd

Hakufanya Mtume haya wala hakusema, kama yaliyobainishwa haya katika sahifa 115 ya Juzuu ya pili ya Hashiya ya “Ash-Shabramallisy” juu ya “Nihaaya” kuwa haya hayakusuniwa.

QUR-AAN

1. Kukariri Qul Huwa Allaahu Mara Tatu

Ni uzushi aliouzua Al-Harawany aliyezaliwa mwaka 305 akafa 402

Umetajwa u-bid’ah huu katika sahifa 151 ya Juzuu ya pili ya “An-Nashr Fil Qiraatil ‘Ashr” na katika sahifa 451 ya “It-haaf Fudhaalaail Bashar Fil Qiraatil Arba’a ‘Ashar”

Vile vile kuikariri mara hidaashara (Ikhlaas Ihdaa ‘Ashara Marrah) ni uzushi pia. Si makaburini wala mahala pengine.

2. Kuisoma Yasiyn Watu Wote Kwa Sauti Moja

Ni uzushi uliozuliwa na Isma’iyl Al-Jabarty na watu wake katika Al-Yaman.

Na hiyo Hadiyth ‘Yasiyn inampatia mtu aliyoyakusudia’ si Hadiyth ya Mtume. Uongo tu, kama ilivyobainishwa haya katika sahifa 447 ya “Al-Maqaasidul-Hasana” na sahifa 544 ya Juzuu ya pili ya “Kashful-Khafaa” na sahifa 259 ya “Asnal Matwaalib”.

Na vile kusoma sura nyengine kwa sauti moja kama vile wanapokhitimisha.

Page 17: Bida'a

ANGALIA: Ilivyo ndivyo ni vile kusoma kwa Hizb. Mmoja anasoma, wengine wanasikiliza. Akikosa anatengenezwa, khilafu anasoma mwengine, mpaka wakati unakwisha.

3. Kusoma Al-Faatihah Kwa Pumzi Moja

Na kuwa anayefanya hivi ataingia Peponi. Aliyezua uongo huu ni adui wa Mtume kwani vitabu vyote vya Hadiyth vinasema kuwa Mtume akisita kila Aayah katika Aayah zake saba. Na ndivyo vinavyosema vitabu vya Qiraa, basi mtu huyo anataka watu wasimfuate Mtume. Usifanye hivyo muige Mtume.

4. Kuzisoma Kila Siku Sura Makhsusi

Kama “Yasiyn” na “Sab‘ul Munjiyaat” kwa kushiriki hizo Hadiyth zisizokuwa sahihi zinazotaja utukufu wake. Wataingia katika yale masikitiko ya Mtume yaliyoko katika Aayah ya 30 ya Suratil-Furqaan inayosema: {{Watu wangu wamepuuza hii Qur-aan.}}

DHIKIRI

1. Kudhikiri

Haikuwa kabisa wakati wa Mtume watu kukusanyika wakasimama kudhikiri au kukaa, wakawa wanafanya makelele hayo na vishindo hivyo.

Hayo ni mambo yaliyozuliwa baada ya zile karne tatu tukufu, kama alivyosema Mtume katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Ulamaa wa Hadiyth wote kuwa: ((Bora wenu ni hawa walio katika zama zangu, kisha wa mia ya pili, kisha wa mia ya tatu.))

Basi wakubwa wa dhikiri wote wamekuja baada ya hizo karne tatu. Na wakawa wanaitakidiwa mabora ya watu hata kuliko Maswahaba. Na maneno haya kuyapinga Mwenyezi Mungu katika Aayah ya 10 ya Suratul-Hadiyd.

Hebu tutazame hao wakubwa wa dhikiri. Wakubwa wa hizo zikiri hizo ni hawa:

a. Abdul-Qaadir Jaylaniy, kazaliwa mwaka 470 akafa 561.

b. Ahmad Rifa’iy, kazaliwa mwaka 512 akafa 578.

c. ‘Aliy Shaadhily, kazaliwa 593 akafa 656.

Page 18: Bida'a

Na wakitajwa hawa ndivyo wacheza dhikiri hushtuka wakasema “Qaddasa Allaahu Ruuhahu”. Lakini wakitajwa Maswahaba hakuna anayeshituka kwa utajo wao wala wakitajwa Maimaam wa Fiqhi wala Hadiyth. Na haya ndiyo kinyume cha mambo. Walio kitu sio kitu!

Tumesoma mara nyingi kwa maneno ya Qur-aan na Hadiyth za Mtume ndiyo ya kufuatwa:

1. Adhukuriye Jalali

Siyo Dini ya Rasuli

Yahitajia Suali

Wapi ilikozuliwa

Haruki akikohowa

Waima imezuliwa

Mashekhe kusailiwa

Ibada ya kukohowa?

2. Nauliza kwa yakini

Hudhukuriwi Manani

Leo mwaliza rohoni

Wapi ilikozuliwa

Ijapo mtachukiwa

Sifa Zake kusifiwa

Kofi, shingo kudemuwa

Ibada ya kukohowa?

3. Huwaona na bendera

Tasubihi kuburura

Dini hii ni khasara

Wapi ilikozuliwa

Wanawake kuchukuwa

Na kutikisa maziwa

Yawaumiza vifuwa

Ibada ya kukohowa?

4. Mashekhe mnaosoma

Dhikiri sasa ni ngoma

Imesiri kuwa vyama

Wapi ilikozuliwa

Na vitabu kufunua

Kadiri itavyokuwa

Vya pepo, vyano kupewa

Ibada ya kukohowa?

5. Mwanzo kwa Shekhe Huseni Ndiko ilikopokewa

Page 19: Bida'a

Kwake ilikuwa Dini

Mbona kwenu mashindani

Wapi ilikozuliwa

Haikuwa kuchezewa

Kelele na kuzomewa

Ibada ya kukohowa?

6. “Dhanudiya lisalati”

“Yawmul-Jumuati”

Hii yenu tashtiti

Wapi ilikozuliwa

Jamii mnaijuwa

Ilahi kuhaliliwa

Dhikiri mwaipinduwa

Ibada ya kukohowa?

7. Kila bada ya kusali

Kwa kuletwa tahlili

Nyiradi zilo jalili

Sasa mwapandisha hali

Wapi ilikuzuliwa

Dhikiri huamriwa

Ya Mola Kuhimiwa

Bila ya sauti kutowa

Pepo na vyano kupewa

Ibada ya kukohowa?

2. Katika Ubaya Mkubwa Wa Dhikiri Ya Qaadiry

Kuligeuza tamko la Uislamu la Laa ilaaha illa Allaah Muhammadun Rasuulu Allaah likawa Laa ilaaha illa Allaah ‘Abdul-Qaadir Shayli Allaah.

Katika Ubaya Mkubwa Wa Dhikiri Ya Rifa’iy

Kuligeuza tamko la Uislamu hilo likawa Madad Alwaani illa Allaah.

Katika Ubaya Mkubwa Wa Dhikiri Ya Shaadhily

Maa thamma illa Allaah (Hapana chochote ila ni Mungu); unasikia upotofu huu? Kila kitu ni Mungu.

3. Palipotokea Dhikiri

Page 20: Bida'a

Haya mambo ya kukusanyika pamoja wenye Dini na kuleta kelele za visomo yanatokana na dini ya Budhism (ya watu wa Tibet na pande hizo), kama yalivyobainishwa haya katika sahifa 570 ya “Majallatul-Azhar” ya mwezi wa Rajab 1383 (Disemba 1963) Juzuu ya tano ya mwaka thalathini na tano.

4. Kuchukua Na Kuvaa Tasbihi

Na haya piya yamechukuliwa kwa hawa hawa kama ilivyobainishwa humo. Na kwa Mabaniani na Wakiristo kama tunavyoona na kama alivyobashiri Mtume kwa masikitiko akasema: ((Mutafuata (walio wabaya katika nyiye) mwendo wa watu wa dini zilizokuwa kabla yenu, shubiri kwa shubiri.))

Mtume hakuwa akitumia tasbihi kamwe wala Maswahaba wake. Na yalipoanza kuzuka haya - kwa vijiwe tu kwanza - walipinga sana Maswahaba.

5. Kujenga Mazawiya Ya Kuabudia Na Kudhikiria

Ni mambo ya hao pia ni Wakiristo. Monestry na Nunnery, yamebainishwa haya katika sahifa 48 ya “Al-Baith Fiy Inkaaril-Bidai Wal Hawaadith”.

Na zinapita munkari humo - maadam wanakaa wanaume wanaojipa Uwalii wa kutooa - kama zinavyopita katika hizo Monestry kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Aayah ya 27 ya Suratil-Hadiyd.

DU’AA

1. Kuweka Moto Na Kutia Ubani Kabla Ya Kuomba

Hii ni taathira iliyoletwa na watu waliokuwa wakiabudu moto wakisilimu (Persians).

2. Kuomba Kwa Jaha Za Mitume Na Watu Wakubwa

Mwenyezi Mungu Amesema katika Aayah ya 180 ya Suratil-A’araf: {{Mwenyezi Mungu Ana majina Yake Mazuri (Sifa zake Nzuri), mwombeni kwa majina hayo.}}

Akayapambanua zaidi haya katika Aayah ya 110 Suratil-Israi kwa kusema {{Mwombe Mungu useme: Yaa Allaah Yaa Ar-Rahmaan (Yaa Rahiym na kama haya).}}

Watu wa nyuma wa baada ya zile karne tukufu wakatia uzushi wa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa jaha ya Mtume, wakazua kwamba Mtume kasema: “Ombeni kwa jaha yangu”

Page 21: Bida'a

Uwongo. Mtume hakusema hivi. Kama yalivyo bainishwa haya katika sahifa 30 ya “Ahaadiythu-Dhwa’iyfah Wal-Mawdhuu’ah” ya Al-Albaaniy.

Mfano wake alivyosema mwenye Barzanjy. “Tunakuomba kwa sharafu ya Mtume”.

Kisha wakazidi kugeuza wakaomba kwa jaha za Mitume wengine. Kisha wakazidi wakaomba kwa jaha ya Maswahaba kama Ahlil-Badr (Halaal-Badiri) Kisha watu wengine.

3. Kuombwa Mtume Khasa Na Kuombwa Hao Maiti Wengine

Kisha wakapotoka khasa wakamwomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama hiyo du’aa yao: “Nidiriki Ee Mjumbe wa Mungu” sio kumwomba Mungu akudiriki lakini Mtume. Mwenyezi Mungu Anasema katika Aayah ya 36 Suratuz-Zumar:

{{Mwenyezi Mungu hawezi kumkifia (Kumkifu) mja wake Wake.}} (Sharti atafute wengineo). Wakapanda zaidi wakawaomba Mitume wengine. Na yote haya ni shirki.

Kisha ikawa “Pata sote”. Wanaombwa killa maiti. Ikaletwa hiyo du’aa inayoitwa Wasiylah. Akaombwa Al-Haddaad na wenginewe kama hivi:

“Wewe Al-Haddaad ndiwe mwenyewe wa kukidhi haja zetu, nani mwengine isipokuwa wewe?”

Unausikia upotofu huu uliopindukia mipaka huu. Na la kweli nawambiwe. Liwalo lote naliwe.

Sema

Mola kanituma Nenda uikambe

Uisiche Usubi Wala uwambe

Watu wakifumba Wewe sifumbe

Sema waziwazi Wayafahamu

Mambo yote ni ya Mungu

Page 22: Bida'a

Atakalo ndilo huwa Ndiye pweke mwenye Quwa (Nguvu)

Mwenye Amri na Shani

Wakikushituwa Wewe sishituke

Yupi awezaye Kupitisha lake

Wakiwa na lao Mungu ana yake

4. (a) Katika Du’aa Za Uzushi Na Mbaya (Du’aa Ya Usiku wa tarehe 15 Sha’abaan)

Ni du’aa inayosomwa usiku wa kuamkia kumi na tano Sha’abaan inayosema kinyume cha alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur-aan na kwa dhahiri kabisa katika Suratil-Furqaan kuwa “Kutangaza mambo yake ya mwaka huo kuwapa Malaika kunakuwa usiku wa Laylatil-Qadri katika Ramadhaan”.

Du’aa hiyo inapinga maneno ya Mungu, inaona Mungu kakosea kwani du’aa hiyo inasema kuwa hayo huwa mwezi kumi na tano Sha’abaan.

Basi soma tu du’aa inayompinga Mungu! Ungojee marungu.

Na hizo Hadiyth zinazotajiwa usiku huu na funga yake si sahihi kama yaliyobainishwa haya katika sahifa 184 ya Juzuu ya kwanza ya Fataawa za Ibn Hajaril Al-Haytamy alisema “Na Hadiyth zote hizi zilizotangaa za kutaja utukufu wa usiku huu ni batili”. Hazina asli. Ingawa zimetiwa katika vitabu vya baadhi ya watu wakubwa kama Al-Ghazaali.

Na aliyezua du’aa hii ya nusu Sha’abaan ni ‘Abdallaah Bin Asad aliyekufa 733.

(b) Katika Du’aa Za Uzushi Na Mbaya (Du’aa Ya Usiku wa Ijumaa Ya Mwanzo Wa Rajab)

Ni du’aa inayosomwa usiku wa kuamkia Ijumaa ya mwanzo ya Rajab na ikaambiwa kuwa ikisomwa na Swahaba aliyekuwa mbaya na jina lake ‘Abdallaah bin Sultan. Na kwa kusoma du’aa hii siku moja tu kila mwaka alisamehewa madhambi yake yote na Malaika wakahudhuria maziko yake. Na Mtume akaamrishwa ahudhurie.

Hapana shaka kuwa du’aa namna hizi zinatungwa na maadui wa Waislamu wanawatoa khofu ili wazame katika maasi waharibikiwe duniani na Akhera.

(c) Katika Du’aa Za Uzushi Na Mbaya (‘Du’aa Ya Mwisho Wa Mwaka’)

Ni du’aa inayoitwa “Du’aa ya mwisho wa mwaka” ambayo imeandikwa katika sahifa 243 ya “Dalailil-Khayrat” kuwa akiisoma du’aa hii siku hiyo atafutiwa dhambi zake zote za mwaka mzima uliopita.

Page 23: Bida'a

Ndizo hizo du’aa za kuwapa nguvu watu kufanya maasi.

5. Katika Du’aa Za Uzushi

Du’aa ya mwanzo wa mwaka, du’aa ya siku ya ‘Ashuraa. Hakuweka Mtume du’aa maksusi kwa siku hizi. Tusimfundishe, yeye ndiye wa kutufundisha.

6. Dalaailul-Khayrat

Ambayo imekusanya chungu ya sifa zilizopinduliwa mipaka juu ya Mtume ambazo kazikataza kama yalivyobainishwa haya katika sahifa 473 ya “Siyaanatil Insaan”. Na imekusanya pia mambo yasiyokuwa ya haki kama yalivyobainishwa haya katika sahifa 37 ya “Shar’iah Wal ‘Aqiydah.”

7. Mad-h

Kimechaguliwa siku hizi kusomwa katika khitima na wanawake. Hiki kimekusanya zaidi sifa za kupindukia mipaka za kumsifu na za uongo.

‘Kama kuwa ulimwengu usingeumbwa ila kwa ajili ya Mtume.’

Kuwa haya ni uwongo yamebainishwa katika vitabu vingi vya kubainisha Hadiyth za uwongo kama “Tadhkiyratul-Mawdhu’aat” sahifa 86 na “Risaalatus-Saghany”sahifa 7 na vinginevyo.

Mwenyezi Mungu Ametaja katika Qur-aan sababu nyingi za kuumba ulimwengu wala hakusema hata pahala pamoja kuwa kaumba kwa ajili ya Nabii Muhammad.

Alisema:

i. Kwa ajili Aabudiwe

Kama ilivyo katika Aayah ya 56 ya Surat-Dhaariyat.

ii. Kwa ajili ya kuonyesha uweza Wake

Kama ilivyo katika Aayah ya 12 ya Suratut-Twalaaq.

iii. Kwa ajili ya kubainisha haki na kulipwa kila mmoja jazaa Yake

Kama ilivyo katika Aayah ya 22 ya Suratul-Jaathiyah.

iv. Kuufikisha muda Wake Aliouwekea

Page 24: Bida'a

Kama ilivyo katika Aayah ya 8 ya Suratur-Ruum.

v. Kuwajuulisha walimwengu wepi walio wema na wepi walio wabaya

Kama ilivyo katika Aayah ya 7 ya Surat-Huud.

Na mna ndani yake ya uwongo yaliyo khatari katika itikadi. Kama vile kusema Mtume kafika kwenye ‘Arshi ya Mwenyezi Mungu wakakaa faragha yeye naye. Na vitabu vya Miiraji vya kutegemewa vinasema kuwa haya ni uwongo; hata “Addardiyr” yetu imesema kuwa haya ni uwongo.

8. Burdai

Ina baadhi ya haya haya yasiyokuwa ndiyo yaliyomo katika hiyo Madihi. Ndiyo hayo hayo yaliyomo katika Burdai lakini afadhali hii kidogo.

Lakini hii Burdai ina ubaya mwengine - wa kuvunja hishima za Mitume - kama zile Abyati:

Wakulluhum mir RasuuliLlaah multamis Ghurafam minal bahr aw rishqam minad daym

Na nyinginezo. Hali ya kuwa Mtume kuambiwa: {{Fuata uwongofu wa hawa.}}kama ilivyo katika Aayah ya 90 ya Suratul-An’aam. Na Nabii Ibraahiym ndiyo zaidi kama alivyoambiwa katika Aayah ya Suratin-Nahl: {{Fuata mwendo wa Ibraahiym.}}

Na yeye anasema “Hao wanamuomba Mtume awagaie ilimu yake na...”

Na mna ndani yake kumwomba Mtume badala kumwomba Mwenyezi Mungu kama vile kusema: “Ya akramal Khalqi Maliy Ma-naluudhu Bihy Siwaka”.

Na watu wakafanya ndiyo nyiradi kubwa hizi!

UGONJWA

1. Kwenda Kutazamia

Kutazamia aliyemroga khalafu asadiki hayo anayoambiwa na huyo mtazamiaji (Mtabiri). Mtume kasema: ((Atakayemwendea Mtazamiaji akamuuliza akamjibu akamsadiki, Mwenyezi Mungu hatazikubali Swalah zake muda wa siku arobaini.))Hadiyth hii wameitaja Maimamu hawa: Ahmad Bin Hanbal, Abu Daawuud, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah. Kwani Mwenyezi Mungu kayakataza haya kama ilivyo katika Aayah 102 ya Suratul-Baqarah.

Page 25: Bida'a

2. Kuwewliwa

Mwanawake mgonjwa kumiminiwa maji ya kuoga (kukoga) na mwanamume. Ati dawa! Huko ni kutafuta shakawa (Shaqawa) ya kuzini na kuziniwa. Wasikubali walio wanaume kweli kuchezewa.

3. Kupungwa

Majini na Mashetani wanawachezea wanaadamu tangu zamani za mbele kabisa huko, kama ilivyosema Qur-aan katika Aayah ya 6 ya Suratul-Jinn. Lakini tumeambiwa tusiwaendekeze (tusiwatendekeze). Tukijikurupushe na mataabisho yao, tusiyajali. Mwisho watakwenda zao kama walivyotwambia katika Sura ya mwisho ya Qur-aan: “Suratun-Naas”.

Lakini imekuwa Waislamu wanakubali kuchezewa na wao, wakawapanda vichwani wakawachezesha ngoma. Wakapungwa kwa magharama, Na hao wakubwa wa Dhikri na wapiga matari ndio wanaopunga hao pepo wanowaita kuwa mapepo wa Kiislam. Wanawaita Rohani, wengine Tari, wengine Vura, wengine Pepo wa Mawlidi.

Msikie Shaykh mkubwa wa zamani Shaykh Muhyud-Diyn anavyosema juu ya haya mapungaji:

1. Talii katika vyuwo

Unionye wapungwawo

Ila ni huo wambwawo

Uso mbele wala nyuma

Ufunue ukisoma

Majini wacheza ngoma

Urongo unaosemwa

Uwongo wa maayari

2. Bure mnawapa mali

Wapitisha zao feli

Akanushao si kweli

Kwanza wapunga Kitanga

Hao hawana uganga

Wari wanaowapunga

Amedumu na ujinga

Na wapunga Kitimiri

3. Yakiri maneno yangu

Kwani kweli ni uchungu

Kuwa radhi Ndugu yangu

Nambie ndivyo yalivyo

Kwa hivi yakwelezavyo

Watu ndivyo wanenavyo

Ikiwa wanena sivyo

La kweli huwakasiriki.

Page 26: Bida'a

4. Hali ya hawa waganga

Makoikoi na Pangwa

Madungumaro na Ringwa

Na katika wanafiki

Jamii mabaramaki

Wajiwapo sisadiki

Ndio khasa mazandiki

Hawa wapunga Matari

5. Dalili tawambiani

Wakiwapo ugangani

Huzidi ufirauni

Kidhabu pepo wa Rewa

Kama mwataka ambiwa

Ile siku wanojiwa

Na kuzidishwa kuzuwa

Na pepo wa madogori

6. Radhi mukitaka yangu

Wazuieni kwa pingu

Mwenye kuamini Mungu

Na wale wakanushawo

Viumbe mupulikawo

Jamii wapungwa hawo

Huwepuka watu hao

Si Islamu; KAFIRI.

Shaykh Muhyud-Diyn aliyezaliwa Barawa kiasi cha miaka 200 (1206) hivi; akasomesha katika nchi hizi miaka mingi; kisha akawa Chief Qaadhi wa Sayyid Sa’iyd Bin Sultaan na Sayyid Maajid, Unguja. Akafa 27 Sha’abaan 1286 (Disemba 1869). Alitunga nyimbo hii ya kuutuaja Upungaji.

Na mimi naongezea ngoma za pepo ambazo hazikuwa katika zama zake:

Kisomali na Kigala Habshia na Ruhani

Kinubi, Kibuki, Vura Si hakika asilani

Kumbwaya imesharura Kirima kiko njiani

Na Rubamba taabani Vinamaliza umri

Kibuki kimeshtadi Huko Unguja ya sasa

Kinafanya kubwa tadi Na kukamata riyasa

Kila siku chafaidi Pungo na kila anasa

Na ulevi ndio khasa Humo wanaogelea

Page 27: Bida'a

4. Kuvaa Hirizi

Ameyakataza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mambo ya kuvaa hirizi akasema kuwa: ((Mwenye kuvaa hirizi amemshirikisha Mwenyezi Mungu.))Hakuamini Mungu anaamini hirizi. Kama alivyosema katika Aayah ya 104 ya Surat-Yuusuf: {{Wengi katika ushirikina.}}

KUFUNGA

1. Kukhusisha Kuufunga Mwezi Wa Rajab

Ima wote au ile siku ya mwezi saba wa ishirini wake au siku tatu za kumi la mwanzo wake na kati yake na mwisho wake au siku yo yote ile yake. Wakaitakidi kuwa Mtume kasema hivyo.

Hakuna Hadiyth moja iliyosihi katika hayo, kama walivyobainisha ‘Ulamaa wa Hadiyth wakubwa. Na mmoja katika hao ni Ibn Hajar Al-Asqalaaniy katika kitabu chake alichokiita: “Tab-yinul ‘Ajab Bimaa Warada Fiy Fadhaail Rajab” Na inatosha kuitazama sahifa ya tatu tu ya kitabu hiki. Bali vitabu vya Hadiyth vya kutegemewa vyote havikusema haya.

Utukufu wa Rajab ni ule ule utukufu wa miezi minne myenziwe inayoitwa “Ash-hurul Hurum”. Mfunguo pili na tatu na nne na Rajab. Na huo Mfunguo tatu na Mfunguo nne ni bora zaidi kuliko Rajab. Kwa nini vishindo vikawa vya Rajab tu? Na Mtume katu hakufanya hivi.

Hakuufunga wote wala hakuzifunga hizo siku wanazozikhusisha wao, wala hakufunga miezi mitatu hiyo mfululizo. Bali hakupata kufunga mwezi wote mfululizo ila Ramadhaan. Na akifunga siku nyingi katika Sha’abaan, sio Rajab. Kwanini hawamwigi Mtume? Wanafanya yao wenyewe! Na Mtume kishasema katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Ulamaa wa Hadiyth wote kuwa anayemsingizia uwongo mahala pake Motoni.

Basi nawatahadhari hao Makhatibu wa Ijumaa na mwengineko kutaja Hadiyth za uwongo hizo. Umeona alivyosema Ibn Hajar na wengine kuwa hakuna hata Hadiyth moja iliyosihi juu ya fadhila za kufunga mwezi wa Rajab.

Page 28: Bida'a

2. Kuikaribisha Ramadhaan

Kwa kuimbia mwisho wa Sha’abaan vyuoni na Msikitini: “Marhaban ya Shahra Ramadhaan” au “Karibu mgeni…”na nyinginezo. Upumbavu huo na kichekesho. Bali likizo kwa wanaojua.

Uzushi tu huu. Huo mwezi wa Ramadhaan unawasikia wanavyoukaribisha hivyo??

3. Kuiaga

Kwa “Muwadaa” au kwa kulia Makhatibu mimbarini “Assalaamu ‘Alayka yaa Shahra…”

Hawawachi watu vituko vituko hivi? Vitawatia katika vituko vikubwa siku ya Qiyaamah. Mwenyezi Mungu mwenyewe kasema katika Aayah ya 124 ya Suratul An‘aam:

{{Mwenyezi Mungu Anajua mahala pa kuweka Utume Wake.}}

Akauweka kwa Nabii Muhammad, akatufundisha ya khayr yote aliyotufundisha. Basi imewakhusu nini wao kutia yao! Haya! Atayetafuta nyingi nasaba itamfika mingi misiba.

4. Kukesha Usiku Wa Kuamkia ‘Iyd Kwa Visomo Msikitini

‘Iyd kubwa au ndogo. Hapana kabisa Hadiyth sahihi ya Mtume inayohimiza haya wala hakuyafanya Mtume kabisa kama ilivyobainishwa katika “Attaghiyb wat-Tarhiyb” sahifa 275 ya Juzuu ya pili na sahifa 328 ya Juzuu ya pili ya “Sharhul-Ihyaai” ya Zaynul-‘Iraaqiy.

Page 29: Bida'a

MAWLID

1. Kusoma Mawlid

Mawlid ni uzushi (Bid’ah) uliyozuka baada ya kupita hao watu mabora aliowasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama tulivyobainisha katika Dhikiri namba moja. “KUDHIKIRI” Hata mjukuu wa huyu aliyetunga Mawlid ya Barzanjiy akaifanyia sharh yake akiita “Al-Kawkabul-Anwaar” aliandika katika sahifa 4 maneno haya “Jua kuwa kusoma Mawlid ni bid’ah (uzushi) kwani halijapokelewa jambo hili kwa hao Ulamaa waliokuwa karne tatu tukufu za mbele huko zilizosifiwa na Mtume”. Basi inatosha shahada hii ya huyu mjukuu khasa wa huyu mwenye Barzanjiy. Imekuwa “Washahida shaahidun min ahlih” yaani akashuhudia shahidi wao wenyewe.

Basi wacha kushughulikia mambo yasiyokuwa ndiyo, khasa ilivyokuwa yanatokea ndani yake mambo mabaya kabisa yasiyokuwa ndiyo. Kama mchanganyiko wa wanaume na wanawake unaotokea wakafanya mambo yasiyokuwa ndiyo. Na mambo haya si kificho, hakuna asiyejua.

Na ubaya wake mkubwa zaidi kule kuwadhanisha watu kuwa hilo ni jambo zuri lilohimizwa na Mtume, kumbe kinyume nyume. Usitoe pesa lako kwa jambo lilokwenda kinyume na alivyosema Mtume.

2. Zeffe (Zafa)

Nani asiyejua namna Zeffe inavyoutia aibu Uislamu? Fujo la wanaume na wanawake, mbali fujo la wahuni. Fujo la wanaocheza ngoma za uchafu, na chakacha na dansa na nyinginezo. Yuko mwenye akili yake timamu akayaona mazuri haya?

3. Kupiga Dufu (Daf) Na Mazumari

Kupiga daf msikitini ni haramu kwa wanavyouni wote wanaotegemewa kama ilivyo sahifa 273 ya Juzuu ya tatu ya “I’anatut-Twalibyn” Alisema: “Halipigwi Daf msikitini, seuze kupiga mazumari” Ati Gasba; Gasba ndiye nduguye zumari na zumari ndiye nduguye Gasba. Ila huyu mfupi huyu mrefu.

Ama kupigwa nje ya Msikiti kwa jambo la arusi na la furaha (kwa wanawake) haikatazwi maadam hapana mchanganyiko wa wanaume na wanawake.

Page 30: Bida'a

Ama kwa jambo linaloitikadiwa kuwa la Dini basi hakuna yeyote mwenye kutegemewa aliyesema ni jambo zuri hilo seuze kusema ni Sunnah. Mufti mkubwa wa Hadhramauti wa zama hizo – Sayyid ‘Abdur-Rahmaan Mashhuur - Alisema katika sahifa 322 ya kitabu chake: “Bughyatul-Mustarshidyn”: “Na kwa kila hali mambo hayo ima haramu au karaha au Sivyo ilivyo bora”.

Basi uko wapi huo uzuri hapa? Seuze Usunnah? Si Sharifu wa Hadhramauti huyu? Na Mufti huko pia? Na ndiye Sheikh wa Sayyid Mansab, Sayyid Ahmad bin Sumeit na Shaykh ‘Abdallaah Bakathiyr na walimfuata vyema kwani ndiyo haki. Hawakuhudhuria kwenye matari wala hawakuya kubalisha mpaka wameondoka ulimwenguni.

Na huyu mufti alizaliwa Hadhramaut mwaka 1250 akafa 1320.

KUUSHUGHULIKIA MWAKA WA NAYRUZI

Mwaka huu hauna ukhusiano chembe na Uislamu. Basi imekhusu nini “kisomwe hiki”, “kiliwe hiki”, “kichinjwe hiki?” Na huyu mnyama atakayechinjwa apitishwe majiani na vijuzuu vya Qur-aan anapita akisomeshwa! Mpaka afikishwe hapo pa kuchinjiwa! Pa kuitikadi kuwa sharti achinjwe hapo!

Na wanaitakidi kuwa kama hatachinjwa hivyo Shatwaan wa mwaka huo atawadhuru. Basi ikiwa hii ndiyo itikadi, mnyama huyo itakuwa haramu kuliwa kama ilivyo katika vitabu vyetu vya Dini. Kama sahifa 206 ya Hashiya “Fat-hul Mu’iyn” inayoitwa “Tarshiyhil Mustafiydiyn” na sahifa 349 ya Juzuu ya pili ya “I’aanatut-Twaalibiyn” na vitabu vyengine

KUOA

1. Kutazama Manazili (Saa Ya Kuolea)

Uzushi na haramu. Kama tulivyobainisha uharamu wa kutazamia haya katika “Ugonjwa” namba 1, na vitabu vyetu vya Fiqhi vimebainisha uharamu wa kutazamia saa za kuoa kama sahifa 234 ya “Fataawa Bni Ziyaad” iliyoko katika “Bughyatul-Mustarshidiyn.”

Page 31: Bida'a

Na huko kuweka kufunga ndoa Ijumaa saa kumi na mbili ya asubuhi ni katika hizo bid’ah na uzushi. Hakusema Mtume haya katika Hadiyth sahihi kama ilivyo katika sahifa 480 ya “Al Maqaasidil-Hasanah” ya As-Sakhawiy na sahifa 106 ya “Allu-ulu-ul Marsuu.” Bali Hadiyth ya uwongo kama ilivyo katika sahifa 261 ya “Asnal-Matwaalib Fiy Ahaadiythi Mukhtalifatil Maraatib.”

2. Kusema Miezi Fulani Ukorofi Unakolea

Kama mfungo mosi mfunguo pili mfungo nne, mfungo tano, mfungo nane. Uzushi kabisa, hakusema Mtume haya. Mtume alioa katika miezi yote hiyo na kuozesha, na sisi juu yetu kumfuata Mtume.

a. Katika Mfunguo Mosi aliwaoa mabibi hawa: ‘Aaishah na Ummu Salamah

b. Mfunguo pili: Mabibi hawa: Zaynab na Maymuunah

c. Mfunguo nne: Ummu-Habiybah

d. Mfunguo tano: Swafiyyah

KUTAZAMIA KWA MSAHAFU NA TASBIHI

Pia haya haramu. Msahafu haujawekwa kutazamia. Umewekwa kusomewa nakufuata yaliyomo ndani yake; hata katika sahifa 186 ya Hashiya ya “Sawi” Juzuu ya tatu juu ya Jalalayn umetajwa uharamu wa jambo hili.

Na ukatajwa hapa hapa uzushi wa kulalia “Manami”. Ati wakati wa kulala usome sura fulani utie nia ufahamishwe usingizini natiyjah (matokeo) ya jambo hilo uliloliazimia ni zuri au baya.

Bwana Fulani alisomea hiyo “Manami” kwa nia ya kubainishiwa lipi bora:

a. Kuuliza shamba lake kubwa alipe deni na kitakachosalia anunue shamba dogo la kuendeshea maisha; au

b. Alitie rahanini kwa ribaa?

Akaoteshwa “Litie rahani kwa ribaa”.

Basi nani aliyemuotesha kufanya baya hili la kumwangamiza duniani na Akhera? Shaytwaan huyu ndiye aliyemchezea usingizini kama anavyowachezea umachoni.

Page 32: Bida'a

KUSWALI KWENYE MAKABURI NA MASHARTI YA KUOMBA SHAFA’AH

Kuswali Kwenye Makaburi Na Masharti Ya Kuomba Shafa’ah

الصالة عند القبور وشروط الشفاعة

Afisi Ya Kutoa Da’wah Ya Kiislamu Mjini Rabwah, Riyaadh

الجالیات بالربوة بمدینة الریاضالمكتب التعاوني للدعوة وتوعیة

Shukrani zote ni za Allaah.

1 - Suala La Kuswali Katika Makaburi

Kuswali katika makaburi ipo katika namna mbili:

Aina ya kwanza ni kuswali kwa kumkusudia aliyezikwa ndani ya kaburi. Hii ni shirki kubwa ambayo inamsababishia mtu kwenda nje ya msingi wa Uislamu, kwa sababu kuomba ni tendo la ibada, na hairuhusiwi kufanya tendo la ibada yoyote kwa yeyote isipokuwa tu kwa Allaah. Allaah Anasema (tafsiri ya maneno):

{{Mwabuduni Allaah wala msimshirikishe na chochote.}} [An-Nisaa: 36]

{{Hakika Allaah Hasamehi (dhambi ya) kushirikishwa na kitu, (kukifanya ni mungu nacho ukakiabudu, ukakiomba…). Lakini Yeye Husamehe yasiyokuwa hayo kwaAmtakaye. Na anayemshirikisha Allaah, basi bila shaka yeye amekwsihapotea upotofu ulio mbali (na haki).}} [An-Nisaa: 116]

Aina ya pili ni kuswali kwa Allaah katika kaburi. Hii inajumuisha idadi ya mambo kadhaa:

i - Kuswali Swalah (Janaazah) Katika Sehemu Ya Kaburi, Ambayo Inaruhusiwa

Mfano: iwapo mtu anafariki na wewe hujapata nafasi ya kumswalia ndani ya Msikiti, basi inaruhusika kwako wewe kumswalia baada ya kuzikwa.

Ushahidi wa hili ni kwamba hili ndilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilolifanya. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba mwanaume mweusi au mwanamke mweusi alikuwa akisafisha Msikiti, na yeye akafariki. Mtume

Page 33: Bida'a

(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza kuhusiana naye na kuambiwa: “Amefariki.” Akasema: ((Kwa nini hamkuniambia? Nionesheni kaburi lake.)) Hivyo akaenda kaburini na kumswalia Swalah ya Janaazah. [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy]

ii - Kuswali Swalah Ya Janaazah Katika Kaburi, Ambayo Inaruhusiwa

Mfano: mtu anafariki na wewe hujapata nafasi ya kumswalia ndani ya Msikiti, basi inaruhusika kwako wewe kumswalia kaburini baada ya kuzikwa.

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu) amesema: “Inaruhusika kuswali Swalah ya Janaazah kwa maiti ndani ya kaburi kama ilivyokuwa ni ruhusa kuswaliSwalah ya Janaazah baada ya kufariki, kwa sababu imethibitika kwamba mwanamke mmoja alikuwa akisafisha Msikiti na akafariki. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza kuhusiana naye na wakasema: “Amefariki.” Akasema: ((Kwanini hamkuniambia? Nionesheni kaburi lake.)) Hivyo wakamuonesha na akamswalia, kisha akasema: ((Makaburi haya yamefunikwa na giza kwa waliozikwa, lakini Allaah Amewahasahilishia kutokana na maombi yangu juu yao.)) [Imesimuliwa na Muslim]

iii - Kuswali Katika Sehemu Za Kaburi – Mbali Ya Swalah Ya Janaazah – Hii Hairuhusiki Na Wala Haina Nguvu, Iwapo Ni Swalah Ya Faradhi Au Naafilah

Ushahidi wa hayo ni kama ifuatavyo:

(a) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ardhi yote ni Msikiti isipokuwa sehemu za makaburi na vyooni.)) [Imesimulimwa na At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na kusahihishwa na Al-Albaaniy ndani ya Swahiyh Ibn Maajah].

(b) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Awalaani Mayahudi na Manasara, kwani wamefanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu za ibada.)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim].

(c) Kuswali katika makaburi inaweza kuwa na maana ya kuabudia makaburi, au kuiga wale wenye kuabudia makaburi. Hivyo, kwa sababu makafiri walikuwa wakisujudia jua pindipo linapopanda na kuzama, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuzuia kuswali pale jua linapopanda au kuzama, kwa uchache yawezekana kumaanisha kwamba kunapelekea kuabudia jua badala ya Allaah, au kujinasibisha na makafiri.

iv - Kuswalia Mbele Ya Kaburi, Ambayo Ni Haramu, Kwa Mujibu Wa Kauli Sahihi

Page 34: Bida'a

Mfano: unaswali, na eneo la kaburi au kaburi katika muelekeo wa Qiblah chako, lakini huswali katika eneo la kaburi, isipokuwa unaswali katika eneo jengine ambalo lipo karibu na eneo la kaburi, bila ya ukuta au kizuizi baina yako na kaburi.

Ushahidi wa hili kuwa ni haramu:

(a) Imesimuliwa kwamba Abu Marthad Al-Ghanawi amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Usikae katika makaburi, au kuswali kuyaelekea makaburi.)) [Imesimuliwa na Muslim]. Hii inamaanisha kwamba ni haramu kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi au mbele ya makaburi au mbele ya kaburi moja.

(b) Sababu ya kuwa kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi ni sababu ile ile [inayojibu] ni kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea makaburi. Itakavyokuwa kwamba mtu anaelekea mbele ya kaburi au eneo la kaburi katika namna ambayo inaweza kusemwa kwamba anaswali kuyaelekea makaburi, basi hili linakuja chini ya kizuizi, na iwapo inaangukia chini ya makatazo basi hairuhusiki, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiswali…)) Kizuizi kwa hapa ni katika kuswali, hivyo iwapo mtu ataswali kuelekea kaburi, basi anaunganisha utiifu na uasi, na wala hairuhusiwi kujiweka karibu na Allaah katika namna hiyo.

Angalizo: Iwapo kuna ukuta baina yako na eneo la kaburi, basi kanuni kuu [inaeleza] ni kwamba inaruhusika kuswali katika namna hii na wala haikatazwi. Vivyo hivyo, iwapo kuna mtaa au mwendo mkubwa ambao unamaanisha kwamba huwezi kunasibishwa kuswali kuyaelekea makaburi, basi hili linaruhusiwa. Na Allaah Anajua zaidi.

Angalia Al-Mughniy 1/403; Ash-Sharh Al-Mumti’ cha Ibn ‘Uthaymiyn, 2/232.

2 – Kuomba Shafa’ah1[1]

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ataomba Shafa’ah siku ya Hukumu na wengine pia miongoni mwa Waumini.

Lakini hapa tutaongeza jambo ambalo halikutajwa hapo nyuma, ambalo ni kwamba kuna masharti yaliyounganishwa katika kuomba Shafa’ah:

i - Ruhusa ni lazima itolewe kutoka kwa Allaah kwa mwenye kuomba, kuweza kuomba Shafa’ah.

ii - Allaah ni lazima Akubali kwa yule ambaye anaombewa hiyo Shafa’ah. 1[1] Shafa’ah kwa mnasaba wa makala hii ina maana ya Muumini kuweza kumuombea Muumini mwenziwe mbele ya Allaah kwa ajili ya kumsamehe na badala yake kumshushia rahma zake Allaah. [Mfasiri]

Page 35: Bida'a

Ushahidi kwa masharti haya mawili ni aayah ambazo Allaah Anasema (tafsiri ya maneno):

{{Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautofaa chochote isipokuwa baada ya Allaah kutoa idhini kwa Amtakaye na kumridhia.}} [An-Najm: 26]

{{Na (hao Malaika) hawamuombei (yeyote) ila yule Anayemridhia (Mwenyewe Allaah), nao kwa ajili ya kumuogopa wananyenyekea.}} [Al-Anbiyaa: 28]

Ama kwa fikra na mawazo potofu ya Shafa’ah ambayo wanaoabudu masanamu wanafikiria kuwa miungu yao watawafanyia, hii ni Shafa’ah isiyokubalika. kwani Allaah Haruhusu Shafa’ah isipokuwa pale Atakaporidhia kwa wote: mwenye kuomba Shafa’ah na yule mwenye kuombewa Shafa’ah.

Angalia Al-Qawl Al-Mufiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd cha Shaykh Muhammad bin ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu), uk. 336-337.

Ukweli kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Waumini wataombea Shafa’ah haithibitishi kuwaomba wao kuomba Shafa’ah, kama baadhi ya watu wanavyofanya pale wanapomuomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaombea Shafa’ah hata baada ya kifo chake.

Wabillahi tawfiq

2011.